Shirika la kimataifa la kuhifadhi wanyama na mazingira, WWF, limezindua
ripoti juu ya umuhimu wa kuilinda mbuga ya wanyama ya Virunga iliyopo
mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Ripoti ya WWF iliyopewa jina la "Thamani ya kiuchumi ya Mbuga ya
Virunga" imeeleza kwamba mbuga hiyo inaweza kuipatia Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo zaidi ya dola za kimarekani bilioni 1 kwa mwaka
iwapo itatumika kwa njia endelevu.
Mbuga ya wanyama Virunga ilizinduliwa mwaka 1925 na hivyo kuifanya mbuga
ya zamani kuliko zote barani Afrika. Inahifadhi zaidi ya aina 3,000 za
wanyama, wakiwemo sokwe wa milimani walioko hatarini kutoweka. Mwaka
1979, mbuga ya Virunga iliorodheshwa kuwa eneo la turathi la shirika la
Umoja wa Mataifa la sayansi na utamaduni UNESCO.
Uchimbaji wa mafuta au ulinzi wa mazingira?
Sokwe mbugani Virunga
Kwa sababu hiyo, mashirika ya kulinda mazingira, likiwemo shirika la
WWF, yanaupinga uamuzi wa serikali ya Kongo wa kuyakaribisha makampuni
ya nje kuja kuchimba mafuta katika eneo la mbuga hiyo.
Raymond Lumbuenamo, ambaye ni mkurugenzi wa WWF nchini Kongo anatoa
ujumbe huu kwa serikali: "Mmesaini makubaliano ya kimataifa yanayokataza
uchimbaji wa mafuta au nishati nyingine kufanyika mbugani. Hivyo naomba
mheshimu sheria mlizojiwekea wenyewe." Mwezi uliopita, UNESCO iliyataka
makampuni ya mafuta ya Total na SOCO International, kubatilisha vibali
walivyokuwa wamepewa na serikali ya Kongo kwa ajili ya kuchimba mafuta
mbugani. Kampuni ya Total ilikubali kuheshimu mipaka ya mbuga ya
Virunga. Hivi sasa, SOCO International ndiyo kampuni pekee yenye mpango
wa kuchimba mafuta katika eneo la hifadhi ya kitaifa.
Serikali inataka maslahi ya mafuta
Kampuni ya Total haitachimba mafuta Virunga
Raia wa Kongo nao wanapinga uchimbaji wa mafuta mbugani.
"Pamekuwa na maandamano ya kuilinda mbuga ya Virunga. Wakati mwingine
wanajeshi waliingilia kati na kukataa maandamano. Lakini bado watu
wanasema ndiyo, tunaitaka mbuga hii," anaeleza Lumbuenamo wa WWF.
Shirika la WWF limezindua kampeni inayolenga kuilinda mbuga ya Virunga
dhidi ya uchimbaji mafuta. WWF inataka kuiwekea shinikizo kampuni ya
SOCO International ili iachane na mpango wake wa kuchimba mafuta huko
Virunga au katika eneo lingine lolote la turathi ya UNESCO.
"Tukifuata njia ya uhifadhi itakuwa ya kudumu, tukifuata njia ya mafuta,
litakuwa jambo la wakati mmoja tu," anasema Lumbuenamo. Hofu yake ni
kwamba serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo itaweka mbele tamaa
ya kupata maslahi ya haraka kutokana na mauzo ya mafuta na kusahau
kabisa jukumu lake la kuhifadhi mbuga ya Virunga, iliyo ya kipekee
barani Afrika.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/WWF
Mhariri: Josephat Charo
SOURCE:DW.DE
No comments:
Post a Comment