Watanzania wanataka kutunga katiba itakayoongoza nchi yao bila kuwepo
haja ya kufanya marekebisho. Lakini baadhi ya wanasiasa wanasemekana
kuwa wameanza kampeni kutafuta nafasi za uongozi bila idhini.
Lakini suala kubwa katika vichwa vya raia ni kama sheria mama ya nchi
inayoandaliwa sasa italeta mabadiliko bora zaidi au itaiweka nchi katika
kibano cha watu wasiopenda mabadiliko, ambao tayari wameanza kutamka
kuwa wanapinga mabadiliko yaliyo katika rasimu ya katiba.
Mfuasi wa CCM Zanzibar
Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaonekana kuwa bado ni maarufu
katika baadhi ya jamii na kinapendwa kiendelee kutawala angalau kwa
mwongo mmoja zaidi, lakini ukweli ni kwamba wimbi la upinzani kuhusu
pingamizi zake kwa mawazo mapya linainuka zaidi. Hapana shaka hakiwezi
kutawala milele.
Muda, nyenzo, fedha na raslimali watu mara nyingi vimekuwa haba
kuwawezesha Watanzania watekeleze mipango na malengo yao kwa ukamilifu.
Kwa mfano, takwimu za watu zilizopo sasa ni makadirio yaliyotokana na
sensa ambayo haikukamilika ya mwaka 2012 ambayo iliacha wakazi wa maeneo
yasiyofikika kwa urahisi bila kurekodiwa katika orodha za makarani wa
sensa.
Sababu hiyo hiyo ya kutofikika kwa maeneo hayo bado ni kikwazo katika
harakati za sasa ambazo zinahitaji wananchi wote washiriki kikamilifu,
ikiwa pamoja na utoaji wa maoni yao katika maboresho ya rasimu ya katiba
mpya.
Kutunga katiba upya na kuandaa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ni shughuli
za gharama kubwa na hapana budi zikamilishwe katika kipindi cha miaka
miwili kwa kuzingatia haki kwa raia wote na kwa njia ya kidemokrasia.
CCM yaamini itashinda 2015
Kweli Tanzania imefika mahali pagumu katika historia yake. Watu wake
lazima wauthibitishie ulimwengu kwamba bado wameungana na wanauenzi
muungano wa karibu nusu karne kati ya Bara, eneo ambalo lilijulikana
kama Tanganyika, na Visiwa vya Zanzibar, hasa ya mawazo tofauti kuhusu
siku zijazo za muungano baada ya kutangazwa kwa rasimu ya katiba.
Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere
Huo ni upande mmoja wa hali ya kisiasa katika nchi hii ya
Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume, waasisi wa taifa la
Tanzania. Upande mwingine, ingawa hakuna hakika ya nani atakuwa mshindi
katika kura ya maoni juu ya katiba mpya, kila chama cha siasa na
washabiki wake wanachukua tahadhari wasije wakajiangamiza wenyewe kwa
jinsi wanavyoendelea na harakati za sasa.
Matokeo ya katiba mpya huenda yakawa na athari kwa maendeleo yao katika
uwanja wa siasa, lakini pia muonekano wao kama viongozi makini,
wanaoaminika na wenye upeo mbele ya vijana ambao idadi yao inazidi
kuongezeka. CCM inaamini kuwa itaibuka na ushindi mkubwa 2015, lakini
kama matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni
katika kata nne za jiji la Arusha ni kielelezo cha yajayo, basi chama
kianze kufikiria kuachia ngazi kwa heshima.
Kwanini CCM inapinga serikali tatu?
Bendera ya chama cha upinzani CUF
Washindani wake wa karibu, CHADEMA na Chama cha Wananchi (CUF),
wanakipa taswira ya kuwa kiko ukingoni mwa mteremko mkali – licha ya
hayo yanayoelezwa kuwa "mafanikio ya CCM’" katika historia ya Tanzania.
Upingaji wa sera za CCM uko zaidi miongoni mwa kizazi cha vijana ambao
shauku zao zaidi ni kuhusu ajira, elimu ya utaalamu katika nyanja
mbalimbali na ya ufundi stadi, uhuru wa kijamii na maisha bora kuliko
musuala ya uwakilishi bungeni na katika serikali za mitaa.
Kwa mawazo yao, baadhi ya vijana wanasema, CCM ni chama cha watu
wanaotafuta nafasi za kujinufaisha wao binafsi bila kujali watu wengine ;
na watu ambao kila mara huzungumzia harakati za ukombozi wa Afrika
wakati wao wanahitaji ukombozi wa kifikra.
Wadadisi wanauliza, kwa mfano, kwa nini CCM inapinga kuwepo kwa serikali
tatu za Tanganyika, Zanzibar na Muungano ambao ndio mfumo unaotakiwa na
raia wengi.
Wachambuzi wa kisiasa wanaongeza kuwa kukataa mfumo wa serikali tatu
kama rasimu ya katiba inavyopendekeza ni kuhujumu Muungano wa Tanzania.
Wana wasiwasi kwamba huenda chama kina dondoo ya siri, lakini katika
enzi hizi za uwazi, ni Watanzania wachache wanaweza kurubuniwa na chama
ambacho kinaelekea kuishiwa ujanja wa kisiasa kuvutia watu wengi
wakiunge mkono.
Mwandishi: Anaclet Rwegayura
Mhariri: Josephat Charo
SOURCE:DW.DE
No comments:
Post a Comment