Hotuba ya Mugabe baada ya uchaguzi 
 
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe anatarajiwa kutoa 
hotuba yake ya kwanza tangu kushinda uchaguzi mkuu wa Zimbabwe zaidi ya 
wiki moja iliyopita.
                     
Mugabe atahutubia umma wakati wa sherehe za 
kuadhimisha siku ya mashujaa mjini Harare kuwakumbuka wale waliofariki 
wakipigania uhuru wa taifa hilo.
Chama pinzani cha MDC, chake waziri mkuu Morgan Tsvangirai, kitasusia sherehe hizo.
                     
Chama hicho kimewasilisha malalamiko yake kuhusu
 uchaguzi mkuu ambao kinasema ulikumbwa na wizi wa kura kikitaka 
uchaguzi huo kurejelewa.
                     
Bwana Mugabe alishinda 61% ya kura kwenye 
uchaguzi huo uliokamilika tarehe 31 mwezi Julai, huku mpinzani wake 
Morgan Tsvangirai akichukua nafasi ya pili kwa 35% ya kura zilizopigwa.
                     
Chama cha Mugabe Zanu-PF kilishinda wingi wa 
viti vya bunge kikipata zaidi ya thuluthi mbili ikiwa ni viti 160 ya 
viti kati ya 210 vya bunge zima.
                     
Sherehe za kuadhimisha siku ya mashujaa 
Zimbabwe, ni sherehe za kujivunia kwa wazimbabwe wakati ambapo nchi hiyo
 ilijipatia uhuru wake miaka ya sabini.
                     
Hii leo Mugabe atatoa hotuba yake ya kwanza 
katika eneo la kumbukumbu la vita hivyo na ambako baadhi ya wapigania 
uhuru wamezikwa.
                     
Hotuba za Mugabe zinasifika zaidi kwa siasa zake
 kali za kizalendo, na ambazo zaidi hulenga mkoloni wake wa zamani 
Uingereza na pia anatarajiwa kujipiga kifua kufuatia ushindi wake mkubwa
 katika uchaguzi mkuu uliopita mwezi jana.
                     
Chama cha MDC kinasusia sherehe hizo katika kile
 kinachosema ilikuwa wizi mkubwa wa kura uliofanywa na chama cha 
Zanu-PF, kwa hivyo sherehe hii bila shaka itazongwa na siasa.
                     
Mugabe bado hajaapishwa kwa muhula wake wa saba 
akitawala Zimbabwe, kwa sababu ya kesi ya MDC mahakamani kupinga matokeo
 ya uchaguzi huo.
                     
MDC kilisema kina ushahidi wa kutosha kuonyesha 
kuwa wizi wa kura ulitokea na kwamba kulikuwa na visa vingine 
vilivyohujumu matokeo ya uchaguzi huo ikiwemo, rushwa , dhuluma na 
kuvurugwa kwa daftari la wapiga kura.
SOURCE;BBC 
 
 
 
          
      
 
  
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment