MABINTI WA KIZARAMO NA MAFIGA MATATU-DHANA ILIYOPOTOSHWA NA WAHUNI
Inaamini kwa watu wengi kwamba,
wasichana wa Kizaramo wanapowekwa ndani, hufundishwa kwamba, wakiingia
kwenye ndoa ni lazima wawe na mafiga matatu.
wanaoamini hivyo wanabainisha kuwa
mafiga hayo matatu ni ishara ya wanaume watatu, yaani MUME, HAWARA MPYA
na BWANA WA ZAMANI. lakini pia wapo wanaodai kwamba mafiga hayo matatu
ina maana ya kuolewa mara tatu katika maisha yake. Hii ikiwa na maana
kwamba, mwanamke wa kizaramo ni lazima aolewe na kuachwa mara tatu
maishani mwake.
Tafsiri hiyo ni uhuni tu wa watu
wachache wanaotaka kupotosha watu, lakini hakuna ukweli wowote kuhusiana
na madai hayo. Ni kweli kwamba wasichana wanawali wa Kizaramo
hufundishwa kuhusu mafiga matatu pale wanapokuwa wamewekwa ndani kwa
ajili ya kufundwa kwa mujibu wa mila na desturi za kizaramo. Lakini
mafiga hayo matatu huwakilisha watu tofauti na sio mume, hawara mpya
wala bwana wa zamani, ni uzushi tu na uhuni wa watu wachache wanaopenda
kudhalilisha mila za wenzao.
Mafiga matatu yanaozungumziwa,
huwakilisha, watu muhimu kwenye maisha ya ndoa ya mwanamke yeyote. Figa
la kwanza ni MUME, figa la pili ni NDUGU WA MUME, yaani mawifi na
mashemeji zake, figa la tatu ni WAZAZI WA MUME, yaani wakwe.
Msichana wa kizaramo anapokuwa katika
kufundwa, huelekezwa namna anavyotakiwa kuishi na watu hao, yaani mafiga
hayo matatu. Anafundishwa namna ya kumtendea mume wake katika mazingira
tofauti, hufundishwa namna ya kuishi vizuri na wakwe zake, na namna
anavyoweza kuwakabili mawifi na mashemeji zake kwenye mazingira yote.
Ni kawaida ya Wazaramo kuwafundisha
watoto wao wa kike namna ya kuweza kuishi na ndugu za watakaokuwa waume
zao. Msichana wa Kizaramo anatakiwa kufahamu namna ya kutumia mafiga
hayo bila figa lolote kuondoka, kwa sababu kama litaondoka figa moja,
hataweza kubandika chungu katika mafiga yaliyobaki. Hii ina maana
kwamba, bila kuwa na uelewano na na wote hao watatu, ndoa yake inaweza
kuwa katika matatizo.
Ukweli ni kwamba, wasichana wa Kizaramo
ambao wamezingatia kweli kile walichofundishwa, wakati wanafundwa,
hutokea kuwa wanawake waadilifu sana, kuliko inavyodhaniwa. kuna
ushahidi wa kutosha kwa wanawake wengi wa kizaramo ambao wameolewa huko
Bara, ambao wamewashangaza wengi kwa nidhamu yao ya hali ya juu.
Source:Jamii Forums
No comments:
Post a Comment