Dk Ndalichako ‘achanachana
Arusha: Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani Nchini (Necta), Dk Joyce Ndalichako amesema karatasi za majibu
ambazo wamekuwa wakizipata kutoka kwa wanafunzi zinaonyesha kuwa, watoto
wengi wanahudhuria shuleni lakini hakuna wanachojifunza.
P.T
Dk Ndalichako aliyasema hayo jana
jijini hapa alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa mabaraza ya mitihani
ya Afrika, ambao umejikita kujadili suala la tathimini ya elimu kwa
nchi za Afrika.
Hii ni mara ya kwanza kwa Dk
Ndalichako kuzungumza tangu Serikali itangaze kufuta matokeo ya kidato
cha nne mwaka 2012 na kutaka yapangwe upya, suala ambalo lilipingwa na
wadau wengi wa elimu.
Alisema kuwa wakati nchi nyingi za
bara hili zikiwa zimejitahidi kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watu,
ubora wa elimu unaendelea kuwa tishio kwa watu wa bara hili kwa vizazi
vijavyo.
"Kama mabaraza ya mitihani, tumekuwa
tukiona karatasi za majibu kutoka kwa wanafunzi ambazo zinaonyesha kwa
uwazi kabisa kuwa watoto wanahudhuria shuleni lakini hakuna
wanachojifunza," alisema Dk Ndalichako.
Kwa upande wake Profesa Justinian
Galabawa, alisema ili kuendeleza elimu, lazima uamuzi wa kitaalamu
usiingiliwe na siasa kwa namna yoyote ile.
Alitolea mfano kitendo cha Serikali kufuta matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2012 akisema hakikuwa sahihi hata kidogo.
Alisema lazima vyombo vilivyopewa
mamlaka kisheria kama Necta viachwe vifanye kazi bila kuingiliwa kwani
kufanya hivyo kutaporomosha elimu.
Alisema pia lazima kuwa na sera ya
nchi ya kufanya tathmini ambayo ili ifanye kazi lazima ishirikishe wadau
wote na kila anayehusika kuitekeleza awe nayo.
"Jambo la kwanza ni lazima tuheshimu
wataalamu na wasiingiliwe na wanasiasa, taasisi zilizoundwa kisheria na
kupewa mamlaka ya kupima na kutambua watu ni lazima ziheshimiwe. Kama
mtoto amepata daraja la nne huwezi kumpa la kwanza," alisema Profesa
Galabawa.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Seif Ali Iddi alisema mkutano huo ni sehemu nzuri ya
Tanzania kujifunza kutoka kwenye nchi nyingine kujua ni nini watu
wengine wanafanya.
Alisema uzoefu utakaopatikana kutokana na mkutano huu utasaidia katika kujipima na kuendeleza elimu nchini.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo,
Philipo Mulugo alisema kwa siku ya kwanza tu wamebaini kuwa zaidi ya
asilimia 80 ya nchi za Afrika tayari wanatumia mfumo wa usahihishaji kwa
kutumia mashine maalumu (OMR) ambao bado baadhi ya watu nchini
wanaulalamikia.
Alisema baadhi ya nchi sasa wameanza
kusahihisha kwa kutumia kompyuta hata maswali ya kujieleza, hivyo
akawataka Watanzania waache kujirudisha nyuma.
P.T
chanzo: mwananchi
No comments:
Post a Comment