NA: Charles Misango
ALIJULIKANA shule nzima kama sio kata kwa kutandika wanafunzi
bakora. Alikuwa ni mwalimu aliyeogopwa na kila mwanafunzi, sio kwa
sababu ya bakora zake, bali kwa mtindo aliochagua kukuadhibia.
Kwanza ni tabia yake ya kuchapa bakora kwenye makalio ya mwanafunzi
akiwa amesimama, bila kujali kama ni mvulana au msichana. Lakini kubwa
zaidi, alichukia sana kusikia sauti ya kilio au kwikwi ya mwanafunzi
aliyekuwa akilambwa bakora.
Mwalimu huyu ili akusamehe au apunguze idadi ya bakora alizopanga
kukutandika, ulilazimika ama unyamaze au ugugumie kila mkono wake
uliposhuka makalioni.
Lakini zaidi alifurahi kusikia mwanafunzi akicheka na kusema ‘asante
mwalimu’ kila fimbo ilipomwingia barabara; kwamba mwalimu huyo
angejisikia furaha kubwa, kama baada ya kumaliza adhabu hiyo kumwambia,
“Nakushukuru mwalimu Makomba kwa zawadi tamu.”
Ilikuwa ni kumpandisha hasira ikiwa mwanafunzi aliondoka kimya kimya
au akianza kulia baada ya kutandikwa. Eti ilikuwa sawa na kudharau
adhabu yake! Ilionesha adhabu ile ilikuwa ya uonevu na kilio cha
mwanafunzi kilikuwa ishara kwake kuwa ipo siku naye atalipiza!
Nimelazimika kukumbuka vituko vya mwalimu huyu (sasa ni marehemu)
kutokana na ambacho wakulima wa Tanzania wamelazimishwa kwa miaka kadhaa
sasa kufanana na tuliokuwa wanafunzi chini ya mwalimu Makomba.
Serikali ama kwa nia njema au kwa kuzuga tu, kwa miaka mingi sasa
imekuwa ikiendeleza utaratibu wa siku nyingi wa kile wanachokiita
sherehe wakulima ya Nanenane.
Nakiri kwamba ingawa nilikuwa bado mdogo, lakini nakumbuka mwanzoni
mwa miaka ya sabini, sikukuu ya wakulima ilikuwa kubwa na yenye fahari
kwa wakulima.
Ilikuwa inasuburiwa kwa hamu kubwa na wakulima wengi lakini zaidi wale
wa pamba na mazao mengine ya biashara kwa sababu wakati huo ikifanyika
baada ya mauzo ya pamba.
Hata wale wa mazao ya chakula waliipokea kwa furaha kubwa kwa sababu
nao kwa wakati huo walikuwa wameuza mazao yao na kwa kweli walikuwa
‘wamefurika mapesa’.
Nakumbuka hotuba za wakulima hazikutolewa na wanasiasa, bali wao
wenyewe. Kila kijiji kilikuwa na risala yake iliyojaa maelezo ya ukweli
ya kipi wanakihitaji na kipi wanashukuru kwa kupewa na serikali kutokana
na mahitaji waliyoomba wakati wa sherehe za mwaka uliotangulia.
Ni sherehe zilizoambatana na maonesha ya mazao bora na mshindi kwa
kila kijiji alipewa zawadi ya zana za kilimo. Nakumbuka mkulima mmoja
katika kijiji cha Sanza, wilaya ya Manyoni, mkoani Singida aliyepewa
zawadi ya trekta na Mwalimu Nyerere baada ya kuwa mkulima bora wa
wilaya. Sijasahau namna mzee huyo alivyoruka juu kwa furaha huku akitoa
machozi.
Nakumbuka bado wakulima wengine waliozawadiwa majembe ya kukokotwa na
ng’ombe ngazi za vijiji, mbolea na baadhi kupelekwa kusomeshwa katika
vyuo vya kilimo vya ndani ya nchi. Sijasahau namna wakulima
walivyoshindana na wafugaji katika michezo ya mpira wa miguu, bao, ngoma
na mambo mengine mengi.
Ni sikukuu ambayo enzi hizo ilileta maana kamili ya sherehe ya wakulima.
Pamoja na kwamba kilimo kilitegemea jembe la mkono, wazazi wetu
waliipenda kwa sababu walithaminiwa, walitendewa haki na walijua
wanalima wakiwa na uhakika wa soko na bei.
Leo yametoweka haya yote. yamebaki masimulizi. Hakuna mkulima wa kweli wa kijiji anayeonja tena ladha na tamu ya Nanenane.
Sherehe hizi zimetekwa na wanasiasa na wachuuzi wa mazao.
Zimebaki kuwa miradi ya waroho na wenye uchu wa fedha za wanyonge, kupata mwanya wa kutafuna fedha za kodi ya wanyonge.
Tofauti na zamani ambapo watawala walionyesha kwa matendo thamani ya
mkulima, leo imebaki kama enzi ya mwalimu Makomba; kwamba mkulima wa
korosho ambaye mwaka mzima alilazimishwa kununua pembejeo kwa bei ya
kulangua iliyopangwa na makuwadi wa soko na kubarikiwa na watawala,
analazimishwa ashangilie kwa maandamano na nyimbo sikukuu ya Nanenane.
Mkulima yule yule ambaye amenyimwa uhuru wa yeye kupanga bei ya mazao
yake kulingana na gharama na nguvu kazi alizotumia katika uzalishaji,
lakini sasa analazimishwa kuuza kwa bei ndogo ambayo haiwezi kurudisha
hata bei ya pembejeo, analazimishwa kwenda uwanjani kulikopambwa mapambo
yaliyogharimu mamilioni ya fedha na kutwangwa jua, ili kusikiliza
hotuba za watawala.
Bila kujali unyonge na jasho lake, mkulima huyu ambaye pamoja na
kufanyiwa yote hayo, amenyimwa malipo ya pili baada ya kuuza kwa mtindo
wa stakabadhi gharani, kwa sababu eti mazao yake yameshuka bei katika
soko la dunia, anaambiwa aje kwenye sikukuu yake, kushuhudia namna ya
mashindano ya magari ya kifahari yaliyojipanga viwanjani na maelfu ya
maafisa wa serikali wanaolipwa posho za malaki.
Wanataka mkulima huyu ambaye ameshindwa kupeleka watoto wake shule kwa
kukosa ada kutokana na jua na viwavijeshi kuangamiza mazao yake bila
msaada wa serikali ashangilie na kuipongeza serikali. Kwamba badala ya
kulia na kusaga meno kwa kule kutojua kwake ataishi vipi kwa mwaka
mzima, wanataka acheke, aruke, acheze!
Watawala wanamwambia mkulima aliyenyang’anywa shamba lake ambalo
amelimiliki miaka na miaka bila fidia, kisa eti kapewa mwekezaji, kama
alivyotufanyia mwalimu Makomba, analazimishwa ashangilie eti ni sikukuu
yake!
Kama Mwalimu Makomba alivyotufanyia, watawala wetu walioshuhudia
mkulima akipigwa, kuswekwa ndani na kufunguliwa mashitaka ya uchochezi
kwa kule tu kupinga kwake kuporwa ardhi yake kwa fidia kiduchu wanataka
naye ashangilie na kuifurahia sikukuu ya nanenane.
Watawala wanataka mkulima wa Ukara kwetu kule, Msimbati, Kifulwe,
Nkojingwa na kwingine ambako mara ya mwisho kumwona kiongozi wa juu
ilikuwa miaka kumi iliyopita baada ya kutembelewa na mkuu wa wilaya;
kule ambako hawajui kama kuna suala la maji ya bomba, eti naye amshukuru
Mungu kwa kupewa siku ya kupumzika na kufurahia matunda ya kilimo
chake!
Nani anayemjali mkulima huyu hata amfanyie sherehe? Mkulima gani
katika sherehe anashangilia ikiwa, maisha yake yametoswa na haonekani
kuwa wa maana? Ni mkulima gani mwenye akili timamu anayeweza kuthubutu
kushangilia nanenane huku, watoto wake wakiwa wametawanyika mijini
wakiuza soksi za mitumba baada ya ng’ombe wa wafugaji wenye sauti na
nguvu za fedha kulisha mazao yake yote nay eye kuponea chupuchupu kuuawa
akijaribu kujitetea?
Ni mkulima gani makini anayeweza kufurahia nanenane ikiwa, binti zake
wamelazimika kuolewa baada ya kukosa ada ya kuwasomesha kwa sababu,
alilazimishwa kununua mbolea feki iliyoangamiza sio tu mazao bali na
kuharibu ardhi yake?
Nani na wa wapi mkulima yule atakayesikiliza hotuba na ngoma za
wanasiasa ambao wameishia kutoa matamshi ya kulaani mawakala wa
kishetani waliomuuzia mbolea lakini wasikamatwe na kushitakiwa ikiwa ni
pamoja na kulipwa fidia?
Hivi katika taabu na maumivu yote haya, yakiwemo ya mkulima kukosa
usafiri wa uhakika wa mazao yake, wizi wa walanguzi wa lumbesa, kupigwa
marufuku na kunyimwa uhuru wake wa kuuza mahindi, mtama, korosho, mchele
na mengine popote anapoona kuna maslahi, mnataka awe kama Mwalimu
Makomba alivyotuamuru kucheka na kumwambia ‘asante Mwalimu kwa bakora
tamu?’
Chanzo:TanzaniaDaima
No comments:
Post a Comment