Tamko la CCM kufuatia mgogoro wa madiwani Bukoba (kuhusu utaratibu)
Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera jana tarehe 13/08/2013 katika 
kikao chake cha siku moja kilichofanyika mjini Bukoba imetangaza uamuzi 
wake wa kuwafutia dhamana ya CCM hivyo kuwavua Udiwani Madiwani wanane 
wa Manispaa ya Bukoba waliotokana na CCM.
 
Kwa mujibu wa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye
 vyombo vya dola hasa Wabunge na Madiwani uamuzi wa Halmashauri Kuu ya 
Mkoa sio wa mwisho.  Uamuzi huo unapaswa kupata Baraka za Kamati Kuu ya 
Halmashauri Kuu ya Taifa ndipo utekelezwe.
 
Hivyo basi, mpaka sasa Madiwani hao wanane waliosimamishwa wanapaswa 
kuendelea na kazi zao kama kawaida wakisubiri kikao cha Kamati Kuu ya 
Halmashauri Kuu ya Taifa kitakachoketi tarehe 23 Agosti, 2013 mjini 
Dodoma ambacho pamoja na mambo mengine kitapitia uamuzi huo wa 
Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera.
 
Pamoja na hilo, tumepokea barua za Madiwani hao za kukata rufaa kupinga 
uamuzi huo wa Halmashauri Kuu ya Mkoa kwa msingi wa madai ya kukiukwa 
kwa utaratibu katika kufikia uamuzi huo.
 
Tunawasihi wananchi wa Bukoba na Kata husika, wanachama na viongozi wote
 kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo suala hili linashughulikiwa na
 vikao vya Kitaifa.
 
Imetolewa na:-
 
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
14/08/2013
 
 
 
          
      
 
  
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment