TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kufuatia
 tamko la Kamanda wa Kanda Maalum wa Mkoa wa Dar es Salaam la kutoa onyo
 kwa Waislam na kusema kwamba wanamshikilia Sheikh Ponda kwa tuhuma 
mbili za, kwanza, kutokana na tukio la Morogoro na, pili, kukiuka 
masharti ya kifungo cha nje alichohukumiwa mwanzoni mwa mwaka huu, CUF –
 Chama cha Wananchi kinatafsiri tamko hili kama muendelezo wa kile 
kinachoonekana kuwa ni hujuma dhidi ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Hatuoni
 sababu ya Kamanda Suleiman Kova kutoa onyo kwa Waislamu kwa jambo 
ambalo Waislamu wameshatoa tamko kupitia Amiri wao, Sheikh Mussa 
Kundecha, na kuiomba serikali kuunda tume huru ya kuchunguza tukio hilo.
Tangu
 litolewe tamko hilo, hakuna Muislamu yoyote aliyefanya jaribio lolote 
la kutaka kulipa kisasi kwa polisi au kwa mtendaji yoyote wa serikali. 
Sasa kuna haja gani ya kutoa onyo kwa jambo ambalo Waislamu 
wameshakubali maelekezo ya viongozi wao?
Pili, kutangaza 
kumshikilia Sheikh Ponda akiwa hospitalini, ambako anapatiwa matibabu, 
kwa kisingizio au kwa tuhuma za tukio la Morogoro au kukiuka masharti ya
 kifungo cha nje ni hoja zisizo na mashiko.
Juu ya suala la Morogoro, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi imeunda tume ya kuchunguza tukio hilo, na tayari 
  
 
 
  
tume hiyo  imeshaanza kazi ya kukusanya taarifa kwa watu mbalimbali mjini Morogoro.
Sasa
 wewe Kamanda wa Kanda Maalum unahusikaje kwenye jambo hilo la Morogoro?
 Au umepewa maagizo ya kumkamata Ponda na Tume iliyoundwa toka Makao 
Makuu?
Iwapo umepewa 
amri, je Tume hiyo imeshakabidhi ripoti yake kwa IGP Saidi Mwema na 
imependekeza Ponda akamatwe kwa tukio hilo kwamba yeye ndiye muhusika 
alimpiga risasi Sheikh Ponda?  (Hapa nina maana amejipiga risasi 
mwenyewe?). Hivi Kova ni Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu?
Suala la kukiuka masharti ya kifungo cha nje, hivi Kova unayafahamu hayo masharti na umepata agizo lolote toka kwa Hakimu au Mahakama ilimuhukumu Sheikh Ponda, kwamba umkamate kwa kuwa amekiuka masharti?
Maswali yote haya yanakupa majibu na mtazamo sahihi kwamba Kova unafanya kazi ya kumuhujumu Rais.
CUF
 – Chama cha Wananchi kinaitafsiri kauli ya Kamanda Kova kama imelenga 
kutoboa jahazi lililobeba hasira za Waislamu katika suala hili la 
kupigwa risasi Sheikh Ponda.
Kauli
 hii inapaswa kulaaniwa na wapenda amani wote. CUF -Chama cha Wananchi 
kinamshauri Kamanda Kova kwa sio lazima kujibu kila jambo unaloulizwa na
 waandishi wa habari, na ikiwa lazima kujibu, basi upime kile unachojibu
 kwa maslahi ya nchi na usijibu tu kwa maslahi yako.
Mwisho kabisa CUF – Chama cha Wananchi kinamtaka IGP Saidi Mwema kutoa ufafanuzi juu ya kauli tata za Kamanda Kova.
Imetolewa na:
Abdul Kambaya
Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Sheria na Uenezi, CUF
 
No comments:
Post a Comment