Monday, 5 August 2013

Misitu sehemu ya maisha inayotoweka

Kila sehemu ya Tanzania wakulima wanahangaika kuliko ilivyowahi kutokea, wakishindana na mabadiliko ya hali ya hewa ili kulinda riziki zao na usalama wa chakula, lakini huenda wasipate wasifaulu na kuidhibiti hali hiyo.
Katika maeneo mengi ya vijijini wakulima wa Tanzania wana ufahamu wa mabadiliko ya hali ya hewa yanavyotishia maisha yao, lakini hawana ujuzi wa kutosha kuhifadhi mali asili ambazo ni muhimili wa shughuli zao za kilimo.
Taratibu za kienyeji ambazo zamani zilitumiwa kulinda ardhi na vyanzo vya maji, kwa mfano, wakati huu hazizingatiwi.
Viongozi wa vijiji wa siku hizi hawajali taratibu hizo wanapowaruhusu wawekezaji kufungua shughuli zao katika hifadhi za misitu. Maafisa utawala wengi katika wilaya na mikoa husema maneno matupu bila vitendo kuhusu masuala ya mazingira.
Hali inayofadhaisha zaidi, hata hivyo, ni pale ambapo maskini wanatumiwa na watu wenye tamaa ya mali kwa faida zao binafsi au wanajikuta wanalazimishwa na shinikizo la umaskini kufyeka misitu.
Misitu yafyekwa
Tatizo la maji Tanzania. Tatizo la maji Tanzania.
Maeneo ya vyanzo vya maji hufyekwa kila siku na mito inakauka kutokana na miti inayokatwa kwa ajili ya mbao na uchomaji mkaa au uchimbaji wa mawe kwa shughuli za ujenzi.
Serikali za mitaa zinafahamu kabisa uporaji huu lakini mara nyingi hazina ujasiri wa kuzuia walafi ambao ndio wanasukuma uvunaji haramu wa misitu, uchimbaji mawe na biashara za mkaa ambazo hufanywa bila liseni.
Wakati ambapo viongozi wanadai kwamba taifa hili la Afrika Mashariki karibu lipate ustawi kiuchumi, hawatilii maanani athari zinazolikabili kutokana na mazingira.
“Tunao viongozi wengi wasio ona faida za mbali zitokanazo na mfumo wa ikolojia. Hawatambui kuwa chanzo asilia cha maji kikiisha haribiwa hakiwezi kuundwa upya,” alinieleza mhandisi wa maji mjini Morogoro – mji ambao miaka michache iliyopita ulisifika kutokana na mandhari yake ya mimea na majani yasiyokauka na vijito vilivyotiririka mwaka mzima.
Hata milima haiko salama
Tatizo la maji Tanzania. Tatizo la maji Tanzania.
Mazingira hayo katika milima ya Uluguru ambayo iko karibu na mji wa Morogoro sasa yametoweka kutokana na kukosa uongozi wenye upeo wa kuona mbali. Na kadiri idadi ya wakazi wa mji huo inavyoongezeka, vilio vyao vya kutaka maji safi na udhibiti wa usafi pia vinaongezeka.
Wakoloni walitengeneza ramani za vyanzo vya maji na kuzuia watu wasiingilie maeneo hayo. Kwa mfano, utawala wa Kijerumani ulitengeneza ramani ya vyanzo vya maji ya mji wa Singida ulioko katikati ya nchi mwa 1910 ambapo ulikuwa haujapanuka zaidi ya kuwa kituo tu cha utawala.
Utawala wa Kiingereza ulifanya kazi hiyo hiyo kwa nchi nzima hadi miaka ya 1950.
Lakini badala ya kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji katika jamii ili kulinda vyanzo vya maji na misitu, wenye madaraka katika Tanzania huru kwa miongo mitano iliyopita waliachia uharibifu uendelee kwa kasi isyo na kifani.
Kulingana na takwimu rasmi zilizopo, ambazo zinahitaji zitazamwe upya kwa umakini, misitu wakati fulani ilihifadhi asilimia 80 za vyanzo vya maji nchini na asilimia 60 za mabwawa ya kuzalisha umeme.
Ikolojia haipewi nafasi
Mfugaji wa Kitanzania. Mfugaji wa Kitanzania.
Wakati hali halisi haiendi sawa na makadirio hayo, uwiano wa mifumo ya ikolojia katika sera za maendeleo haupewi msukumo wa kutosha kuondoa changamoto zinazoikabili nchi katika utoaji wa huduma za maji na nishati kwa wananchi.
Kampuni ya Umeme ya Tanzania (TANESCO) bado haina uwezo wa kufua umeme wa kutosheleza mahitaji ya watumiaji wa nishati hiyo.
Mamlaka za maji mikoani vile vile hazifanyi kazi kwa ufanisi kutokana ama na ukaukaji wa vyanzo vya maji au kukosa nishati ya kusukuma maji kwenda kwa watumiaji.
Kuni na mkaa ndicho chanzo kikubwa cha nishati inayotumiwa na watu wengi majumbani kwao mijini na vijijini.
Taarifa ya karibuni imeonesha kuwa asilimia 90 ya wakazi wa mijini nchini Tanzania hutumia mkaa zaidi ya nishati ya aina nyingine. Wauza mkaa wanayo mitandao yao ya kuupata na kuusambaza kote.
Miti inapofyekwa na kuisha eneo moja wanahamia mahali pengine na kuteketeza misitu iliyopo bila kujali kuwa misitu hiyo inastawisha mimea na viumbe wengine adimu.
Hakuna atakaye kuwajibika
Mahindi yanaanza kuadimika. Mahindi yanaanza kuadimika.
Mpaka sasa hakuna mamlaka ambayo yameonesha kuwa na uwezo wa kudhibiti leseni au vibali vya ukataji miti ambapo ni dhahiri kuwa rushwa ndiyo inatawala mpaka hapo sera za kuhifadhi misitu ya Tanzania zitakapodhihirisha kuwa zina uwezo wa kutekeleza kazi hiyo.
Inashangaza kusikia kuwa TANESCO inataka bei za umeme zipandishwe kwa zaidi ya asilimia 80 ambapo kila mtu angefurahi kuona matumizi ya umeme yanawafikia watu wote ili kuokoa misitu.
Uzalishaji mkaa ndio chanzo kikubwa cha kutoweka kwa misitu ya Tanzania lakini kampuni ya taifa ya umeme inajifanywa haioni tatizo hilo.
Kuongezeka kwa bei za umeme maana yake ni kwamba changamoto za mazingira zitaongezeka pia kutokana na uharibifu wa misitu, ikiwa pamoja na maporomoko ya ardhi wakati wa mvua, mabwawa yanayotumika kufua umeme yatajaa tope na mgao wa umeme utazidi mpaka hapo Tanzania itakapopata vyanzo vingine mbadala vya umeme usio na athari zozote.
Sera za Tanzania kuhusu mazingira na nishati hapana budi zilenge kuboresha na siyo kuongeza ukali katika maisha ya watu.
Mwandishi: Anaclet Rwegayura/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khele
SOURCE:DW.DE

No comments:

Post a Comment