NCHEMBA ATUHUMIWA KUSHUSHA HESHIMA YA CCM
MATUKIO kadhaa ya kisiasa, mwelekeo,
kauli na mienendo ya baadhi ya wanasiasa waandamizi na wenye nguvu
katika Chama cha Mapinduzi (CCM) vimeibua mkanganyiko na hali tete ndani
ya chama hicho, Tanzania Daima Jumamosi limebaini.
Kwa muda sasa, kumekuwa na minyukano ya
ndani kwa ndani miongoni mwa viongozi waandamizi wa CCM, huku baadhi yao
wakilaumiana kwa “kuchafua na kuua” chama.
Baadhi yao wamefikia hatua ya kumlaumu
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kwa kuwapa madaraka makubwa
baadhi yao, na kushindwa kuwanyang’anya pale wanapoonyesha dalili za
“kuua” chama chao.
Gazeto hili linazo taarifa za baadhi ya
viongozi wastaafu wa CCM kupeleka ujumbe mzito kwa Makamu Mwenyekiti,
Phillip Mangula, wakionyesha kukerwa na kauli au mwenendo wa baadhi ya
viongozi waandamizi, hasa Naibu Katibu Mkuu, Mwigulu Nchemba.
Wanamtuhumu Nchemba kwa kushusha heshima
ya CCM mbele ya umma, na kuchangia matokeo mabaya katika uchaguzi wa
madiwani uliofanyika Arusha mwezi uliopita, ambako CCM ilishindwa na
CHADEMA katika kata zote nne.
Baadhi ya wazee na makada waandamizi
wanasema Nchemba ni “mzigo wa Kikwete,” kwa maana kuwa ndiye aliyempa
madaraka, na ndiye anayemsikiliza na kumpa jeuri.
Nafasi anayopewa Nchemba imeleta
mgongano wa chini kwa chini kati yake na Katibu wa itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye, ambaye kwa muda sasa amekuwa ndiye kipenzi cha Rais Kikwete
katika kutekeleza mikakati kadhaa na kutoa matamko yenye utata dhidi ya
viongozi au wanachama “wasiopendwa” ndani ya chama hicho, au dhidi ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa mujibu wa makada wanaokerwa na tabia
ya Nchemba, kiongozi huyo amegeuka kero kwa viongozi wenzake, ambao
wanasema ameingiza siasa za ujasusi wa waziwazi na mbinu nyingine chafu
za kisiasa zinazomfanya aibomoe CCM na kuiongezea umaarufu CHADEMA mbele
ya umma.
Source:Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment