Wafuasi wa MDC wadai kushambuliwa na ZANU PF
 
 Siku moja baada ya Rais Robert Mugabe na Zanu PF kutangazwa kushinda 
uchaguzi Mkuu nchini humo, baadhi ya wafuasi wa upinzani kutoka chama 
cha MDC wanasema wameshambuliwa na wenzao wa ZANU PF.
Baadhi ya dola za Magharibi ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, zimetilia shaka iwapo uchaguzi huo ulifanyika kwa uwazi.
                     
Madai hayo yanakuja siku moja baada 
ya matokeo rasmi ya uchaguzi uliofanyika Jumatano kutolewa na kumpa 
ushindi rais Robert Mugabe. Chama chake Zanu-PF kilipata thuluthi tatu 
ya viti vya bunge.
                     
Watu 11 mjini Harare na wengine 20 kutoka mkoa 
wa Mashonaland, wanasema kuwa walishambuliwa na wafuasi wa Zanu-PF 
wanaojulikana sana baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
                     
Chama cha MDC kimesemna uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya wizi wa kura.
                     
Kiongozi wake Morgan Tsvangirai, ameahidi kuchukua hatua za kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi.
                     
Pia alisema kuwa chama chake cha MDC, 
hakitashirikiana na kile cha Mugabe na kuwa kitasusia kushikilia nafasi 
zozote katika taasisi za serikali.
                     
Vyama hivyo viwili, vimekuwa wanachama wa 
serikali ya Muungano tangu mwaka 2009,baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu 
wa mwaka 2008 kusababisha ghasia.
                     
Watu 11 waliodai kushambuliwa katika mtaa mmoja 
mjini Harare waliomba hifadhi katika makao makuu ya chama cha MDC mnamo 
Jumapili, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Brian Hungwe.
                     
Wanadai kuwa walishambuliwa na wafuasi wa 
Zanu-PF waliokuwa wanakwenda nyumba hadi nyumba wakiwaamuru wafuasi wa 
MDC kufunga virago vyao na kuondoka.
                     
Kiongozi wa chama cha MDC, Morgan Tsvangirai alisema uchaguzi huo ulikumbwa na visa vya wizi.
                     
Msemaji wa MDC, Douglas Mwonzora, alisema kuwa 
mashambulizi hayo yalipangwa. Lakini msemaji wa chama cha Zanu PF, 
Psychology Maziwisa, alikanusha madai kuwa wafuasi wa chama walikuwa 
wanawashambulia wapinzani wao.
                     
MDC kinaonya kuwa hakitaweza kuwadhibiti wafuasi wake ikiwa madai ya wao kushambuliwa yataendelea.
                     
Chama hicho kimeomba muungano wa nchi za Kusini 
mwa Afrika , Sadc, kuingilia kati na kuzuia hali kuzorota zaidi kiasi 
cha kutoweza jkudhibitiwa.
                     
Baadhi ya wakuu wa chama cha MDC, wametoa wito kwa wafuasi wao kutoitii serikali na kutenga chama cha Zanu-PF.
SOURCE:BBC 
 
 
 
          
      
 
  
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment