Friday, 16 August 2013

Daktari aliyemtibu sheikh Ponda Morogoro atiwa mbaroni.. chama cha madaktari chapinga

  • DAKTARI ALIYEMTIBU SHEIKH PONDA MOROGORO ATIWA MBARONI..
  • CHAMA CHA MADAKTARI CHAPINGA NA KUDAI HANA KOSA


Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda ambaye alikuwa amelazwa katika Taasisi ya Tiba na Mifupa (Moi), jana aliondolewa na kupelekwa katika Gereza la Segerea, Dar es Salaam.

Kitendo hicho kimelaaniwa vikali na familia yake na wafuasi wake, ambao wamepanga kufanya maandamano makubwa leo ...

Sheikh Ponda, ambaye alisomewa shtaka la uchochezi akiwa kitandani na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Tumaini Kweka ilidaiwa kuwa alitenda kosa hilo katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya Juni 2 mpaka Agosti 11, mwaka huu. Alisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Liwa.

Jana, Polisi waliimarisha doria kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kuanzia saa 1:30 asubuhi. Magari matatu ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU) yaliyobeba askari wenye silaha yalionekana yakiranda katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo.

Sheikh Ponda alitolewa wodini saa 4:20 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa askari baadhi yao wakiwa wamebeba silaha.

Alionekana akiwa ameshikiliwa na polisi kutokana na kukosa nguvu ya kutembea.

Akiwa amevalia shati lenye rangi ya udongo, kikoi cheupe na kandambili, Sheikh Ponda alipakiwa kwenye gari ndogo aina ya Landcruiser nyeupe lililokuwa na vioo vya giza.

Baada ya kupakiwa, safari ya kuelekea Segerea ilianza saa 4:45. Gari lililombeba lilitanguliwa na gari la FFU lililokuwa na askari wenye silaha likifuatiwa na magari mengine mawili ya FFU yaliyokuwa na polisi wenye sare na magari mengine mawili ambayo yalikuwa na askari kanzu.


Wakili ashangaa, familia yaja juu

Akizungumza baada ya tukio hilo jana, Wakili wa Sheikh Ponda, Juma Nassoro alisema hakuwa na taarifa za kuondolewa hospitali kwa mteja wake na kueleza kushangazwa na kitendo hicho akisema mteja wake alikuwa mgonjwa akiwa anahisi maumivu makali ya kidonda tangu juzi.

“Nimepigiwa simu mchana huu na mmoja wa wanafamilia, nimeshangaa sana kwa sababu nakumbuka jana (juzi Jumatano) Sheikh alishindwa kufanyiwa mahojiano na polisi kutokana na kuhisi maumivu na kizunguzungu,” alisema Nassoro.

Msemaji wa familia, Isihaka Rashid alisema hawakuwa na taarifa ya Sheikh Ponda kupata ruhusa ya kutoka hospitali na kwamba wakati anaondolewa alikuwapo mkewe na kijana mmoja kwani muda huo wanafamilia wengine walikuwa kwenye kikao.

“Nilifika hospitali asubuhi, hatukupewa nakala yoyote ambayo inaonyesha Sheikh Ponda karuhusiwa. Lakini baada ya tukio tulipokwenda kuhoji tukaambiwa wamemruhusu tukapewa na karatasi ya kuthibitisha kuwa ameruhusiwa,” alisema Isihaka.

Sheikh Ponda alifikishwa hospitalini hapo Jumapili iliyopita, akiwa na jeraha ambalo linadaiwa kuwa ni la risasi aliyopigwa na polisi katika mkutano wa Kongamano Mjini Morogoro. Rashid alisema familia imepatwa hofu juu ya usalama wa maisha yake kwa kuwa hali yake bado haijatengamaa kwani alikuwa amevimba mkono.

“Wamemchukua katika hali inayotia shaka kwa sababu hata dawa zake hawakumchukulia, cheti cha ruhusa ya daktari pia kimeachwa, gharama zake za matibabu yake ni Sh1.1 milioni. Tumeambiwa tuchague kama tunataka kulipia au vipi, kwetu tunaona kama wamemteka,” alisema Rashid.

Alisema kutokana na hali hiyo familia imeamua kulirejesha suala la kufuatilia usalama wa maisha ya Ponda mikononi mwa viongozi wa Jumuiya anayoiongoza ili walishughulikie na kwamba tayari wamewajulisha kwamba watatoa tamko leo kwenye Msikiti wa Mtambani uliopo Kinondoni.


Daktari matatani
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile amesema watamhoji daktari aliyemtibu Sheikh Ponda Mjini Morogoro. Hata hivyo, Kamanda Shilogile hakutaka kutaja jina la daktari huyo akisema atakuwa anaingilia kazi ya Kamati ya Haki Jinai ambayo ndiyo inayochunguza suala hilo.

Jeraha la Sheikh Ponda limezua utata baada ya mwenyewe kusema kuwa limetokana na risasi aliyopigwa na askari wa jeshi hilo huku polisi wakikana.

Daktari huyo anaaminika kuwa ni miongoni mwa mashahidi muhimu kwani anafahamu chanzo cha kidonda cha Sheikh Ponda.

Inaaminika kuwa alitibiwa katika zahanati ya Al Jamih iliyoko Msamvu baada ya tukio hilo, Ijumaa iliyopita.

Hata hivyo, Makamu wa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Rodrick Kabangira alipinga kitendo cha daktari kuhojiwa akisema Baraza la Madaktari Tanzania ndilo lilipaswa kumhoji.

“Tayari kuna utata wa jeraha lenyewe na ukweli ni kwamba ripoti ya huyo daktari ni muhimu kwa umma kwani ndiyo itathibitisha chanzo cha jeraha,” alisema.

Alisema hakuna kosa lolote kwa daktari huyo kumhudumia Sheikh Ponda isipokuwa kama atakuwa ameandika taarifa tofauti za jeraha hilo.

“Tatizo kubwa ni kwamba Serikali imekuwa ikiruhusu uchunguzi kwa tume ambazo hazitoi majibu halisi kwa wananchi. Ingetumika tume ya kimahakama au baraza ambalo lina mamlaka hata ya kumfutia usajili wake kama atakuwa amedanganya,” alisema.

Msajili wa Baraza la Madaktari Tanzania, Parot Luwena alisema madaktari hutakiwa kufanya kazi kwa misingi ya taaluma zao wala siyo kwa shinikizo, hivyo kama kuna masuala mengine ambayo polisi wanahitaji, wanapaswa kuzingatia sheria za nchi.


Polisi waonya waandamanaji
Polisi imesema kwamba itadhibiti maandamano yanayotarajiwa kufanyika leo kushinikiza kuachiwa kwa Sheikh Ponda.

Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema jana kuwa maandamano yoyote hayatavumiliwa na jeshi hilo.

“Tunapiga marufuku maandamano yoyote, watakaoyafanya wafahamu kuwa jeshi litayadhibiti,” alisema.

Ubao wa matangazo ya Makao Makuu ya Polisi limebandikwa tangazo la kuwataka polisi kuwa tayari kukabiliana na vurugu zozote zitakazotokea.

Tangazo hilo limesema hali ya usalama siyo nzuri na kwamba askari polisi wanatakiwa kujiandaa kukabiliana na vurugu.

-Mwananchi.

No comments:

Post a Comment