Wednesday, 14 August 2013

Sakata ya ugaidi dhidi ya CHADEMA: Shibuda, Sofia Simba watajwa

Katika ile sakata ya kesi ya ugadi dhidi ya makada wa CHADEMA iliyofutwa hivi karibuni mkoani Tabora, mbunge wa CHADEMA Maswa Magharibi atajwa hadharani. Kwa habari kamili soma hapa chini.
Mapya yaibuka

• Makachero wahaha kuwaingiza Dk. Slaa, Mbowe matatani, wakwama
Na Mwandishi wetu

IMEBAINIKA kuwa baadhi ya maofisa wa polisi na makachero wao wamekuwa wanatumia vibaya majina ya viongozi wakuu wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama kisingizio cha kupika kesi za ugaidi dhidi ya viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika tukio la hivi karibuni, makada wa CHADEMA waliokuwa rumande wakikabiliwa na mashitaka ya ugaidi, ambayo hatimaye yalifutwa na mahakama, wametoboa siri kuwa miongoni mwa majina yaliyotumiwa na baadhi ya polisi na makachero waliowatesa ni ya Rais Jakaya Kikwete; na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wiki hii, makada hao - Evodius Justinian, Oscar Kaijage, Rajabu Kihawa, Seif Magesa na Henry Kileo, wamesema pia kuwa njama hizo za polisi na makachero wao, zililenga kuwalazimisha vijana hao wawahusishe viongozi wakuu wa CHADEMA (hasa Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa) na ugaidi na utesaji watu ambao umekuwa unaendelea.

Wengine ambao polisi walitaka watajwe ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.

Hata hivyo, vijana hao wanasema waligoma kuwahusisha, hata baada ya kuteswa kikatili.

Makada hao wanadai kwamba mateso waliyopata yaliratibiwa na viongozi wa Jeshi la Polisi, Advocate Nyombi na afande Pasua.

Mmoja wa makada hao, Kihawa, aliyekamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Dodoma, anadai kuwa alipokuwa anahojiwa, alilazimishwa aseme kuwa viongozi wa CHADEMA ndio wanahusika na utekaji na tindikali.

Akiendelea kusimulia mkasa huo, Kihawa alisema kuwa baada ya kauli hiyo, aliingizwa katika chumba namba 114, ghorofa ya pili, chenye kamera nyingi katika moja ya hoteli maarufu Mjini Dodoma (jina tunalihifadhi kwa sasa) akavuliwa nguo zote, akakalishwa kwenye chupa ya soda kisha akapigwa sana.

“Nilipoteza fahamu lakini nilipozinduka nilikuta nimevalishwa nguo, na nimekalishwa kwenye kiti na kuwekewa chakula karibu,” anasema, na kuongeza kuwa hakula chakula hicho, lakini alipotoka nje ya chumba hicho, kwenye ukumbi wa hoteli, aliwakuta vijana waliofukuzwa CHADEMA, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba na Habib Mchange wakinywa na kula.

Walinikejeli sana, wakasema wanashangilia ushindi,” alisema.

Kutoka pale nilichukuliwa na Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, akaniingiza chumbani akadai anampigia simu Waziri Simba, akamwambia, “mama, huyu kijana ninaye hapa. Ungeongea naye ili akubali kulegeza msimamo, au umpigie mwanao Jakaya anipigie, pengine atabadili msimamo wake kama tulivyokuwa tumekubaliana awali.”

Kihawa anadai kuwa mtu huyo aliyedaiwa kuwa Waziri Simba alimjibu Shibuda kuwa asingeweza kuzungumza yeye kwa kuwa alikuwa hajisikii vema, ila kwa suala la kuongea na Rais Kikwete, atafutwe Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana au Naibu Katibu Mkuu Bara, Mwigulu Nchemba, ili awaunganishe Shibuda na rais.

Kwa mujibu wa Kihawa, baada ya kupewa ushauri huo, Shibuda alijibu: “Mwigulu ni mropokaji, hawezi kuingizwa katika mkakati huu; na Kinana ni mgumu kuingilika katika suala hili.”

Anasema alisikia mazungumzo yao kwenye loud speaker ya simu ya Shibuda, na baada ya kukata simu Shibuda alimwambia kuwa alikuwa anazungumza na Simba, ambaye alidai ni ‘mama mdogo wa Kikwete.’

Kihawa anasema wakati anahojiwa hayo hapo hotelini, maofisa wa polisi walisimama kwa mbali wakimsubiri.

Wengine waliokuwapo wakishuhudia mahojiano hayo ni Meya wa Ilemela, Henry Matata na aliyekuwa Diwani wa Igoma, Adam Chagulani. Matata na Chagulani walishavuliwa uanachama na CHADEMA.

Wahusika walipohojiwa na Tanzania Daima jana, kila mmoja alikuwa na kauli yake kama ifuatavyo:

Tanzania Daima Jumapili: Afande Nyombi, vijana waliokuwa wametuhumiwa kwa kesi ya ugaidi kule Tabora, wamekutaja wewe kuwa ulishiriki kuwatesa ukiwalazimisha wawataje viongozi wakuu wa CHADEMA kuwa walishiriki kutenda ugaidi na utekaji. Unatoa ufafanuzi gani?

Advocate Nyombi: Mimi si msemaji wa Jeshi la Polisi, siwezi kusema chochote.

Tanzania Daima Jumapili: Msemaji atajuaje kama mliwatesa watu wakati wa mahojiano? Mbona huku ni kumwonea msemaji wa Jeshi la Polisi kusemea kila kitu hata mambo ambayo askari fulani ametenda kwa utashi wake?

Advocate Nyombi: Nimekwambia mtafute, msemaji katika hayo yote. Mimi siwezi kuongelea suala hilo, nakutakia Idd Mubaraka njema.

Tanzania Daima Jumapili: Afande Pasua, vijana waliotuhumiwa katika kesi ya ugaidi kule Tabora wamekutaja wewe kuwa ulishiriki kuwatesa, ukiwalazimisha wataje viongozi wa CHADEMA kuwa walishiriki kutenda ugaidi na utekaji. Unatoa ufafanuzi gani?

Afande Pasua: Kwani wewe uko wapi?

Tanzania Daima Jumapili: Nipo Dar es Salaam, hapa ofisini.

Afande Pasua: Njoo ofisini tuongee tuyaweke sawa unayouliza. Umesema unatoka gazeti gani?

Tanzania Daima Jumapili: Nimekwambia Tanzania Daima.

Afande Pasua: Mashtaka hayo kwanza yalikuwa ya serikali, mimi sifanyi kazi ya kubahatisha, mpigie msemaji wa Jeshi la Polisi mimi si msemaji. Alikata simu.

Henry Matata

Tanzania Daima Jumapili: Mstahiki Meya, vijana waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi wanadai walihojiwa mbele yako Dodoma. Je, unafahamu nini kuhusu suala hili?

Matata: Kijana Rajab Kihawa ndio namfahamu. Huyu alikuwa mfanyakazi wangu, ila tangu aache kufanya kazi hapa sijaonana naye. Lakini mimi nina ugomvi na wafanyakazi wote wa gazeti lenu na gazeti lenu. Nisingependa kuongea na nyie. Tangu nifukuzwe CHADEMA gazeti lenu linaongeza chumvi habari zinazonihusu. Mimi si meya kwa kura za CHADEMA. CHADEMA walinifukuza, CCM wakaona nafaa, wakanipa kura nikawa meya.

Tanzania Daima Jumapili: Ulikutana na Rajab Dodoma hotelini?

Matata: Nimekwambia sitaki kuongea na gazeti lenu.

bi Mheshimiwa, vijana waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi wamekutaja kuwa ulikuwepo wakati wanahojiwa Dodoma. Je, una kauli gani kwa yao hii?

Chagulani: Mimi nilikuwa Dodoma mwezi wa nne lakini nilikuwa Kondoa kwa ajili ya uhamisho wa mke wangu. Hayo unayonieleza siyajui.

Waziri Simba hakupokea simu, na alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu lolote.

Msemaji wa jeshi la Polisi, Advera Senso, alipoulizwa kama jeshi ndilo linawatuma polisi kutesa watu wakati linawahoji, alisema: “Mhalifu asitafute huruma ya jamii kwa kuzushia jeshi kwa uhalifu alioutenda yeye, na endapo ikibainika anasingizia uongo na hilo ni kosa pia, kwani Jeshi la Polisi linafuata taratibu za sheria.”

Shibuda alipoulizwa jinsi alivyohusika katika sakata hilo alisema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa alikuwa Agha Khan Hospitali akihangaikia mgonjwa wake.

“Niacheni kwa sasa kwa kuwa nahitaji utulivu wa akili niweze kushughulikia afya ya mgonjwa wangu. Nadhani hata kama ni wewe sijui katika mazingira kama haya ungeweza kweli kuongea?” alisema.

Msemaji wa Ikulu, Salva Rweyemamu, alipopigiwa simu kuulizwa ikiwa wanayo taarifa ya watu wanaotumia vibaya jina la rais katika matukio ya kihalifu aliomba jambo lolote linalohusiana na kazi, lisubiri kwa kuwa alikuwa katika mapumziko ya sikukuu.

“Ndugu yangu, unajua leo ni sikukuu na ni usiku, nitafute wakati mwingine, maana siwezi kuzungumzia mambo ya watu wa CHADEMA muda huu. Niache nipumzike kidogo halafu tuwasiliane siku ya kazi,” alisema.
Source: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment