Hali tete CCM Bukoba,Madiwani wamgeuka Kikwete, wafanya kinyume na maamuzi yake
.Hongo yatembezwa, madiwani watishwa kung’olewa
HATUA ya madiwani wanane wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika manispaa ya
Bukoba, kusaini hati ya tuhuma na kuiwasilisha barua hiyo kwa
mkurugenzi wa manispaa hiyo, kumtaka aitishe kikao ili wapige kura ya
kutokuwa na imani na meya anayetuhumiwa kujiingiza katika miradi ya
kifisadi imechukua sura mpya.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili
jana jioni kutoka mjini Bukoba, zilisema kuwa msimamo huo umewagawa
viongozi wa CCM mkoa wa Kagara na hivyo kuitisha kikao cha halmashauri
ya mkoa leo kwa ajili ya kuwajadili na kuwafukuza madiwani hao. Hata
hivyo uamuzi huo, huenda ukakigharimu chama hicho kutokana na madiwani
hao kusisitiza msimamo wao, wakisema wako tayari kufukuzwa kwa sababu
wanatetea maslahi ya wananchi wakipinga ufisadi.
Akizungumza kwa simu na gazeti
hili kwa masharti ya kuhifadhiwa jina lake, mmoja wa madiwani hao
alisema kuwa rushwa imekuwa ikitembezwa waziwazi kwa wajumbe wa vikao
mbalimbali vya CCM ili kuwalazimisha wakutane mara kwa mara kufikia
uamuzi huo. Chanzo hicho
kimedokeza kuwa katika kuwagawa madiwani hao ambao wameungana na wenzao
wa vyama vya CHADEMA na CCM ili kupunguza idadi ya akidi, diwani mmoja
alijaribiwa kuhongwa milioni 20 ili aondoe jina lake katika orodha hiyo.
“Mwenzetu mmoja kwa kweli amekuwa
jasiri wa ajabu, juzi aliitwa mahala akatumiwa watu wakiwa na fedha
taslimu milioni 20 lakini alikwepa mtego huo na kuwakimbia watu
waliotumwa, akisisitiza kuwa hawezi kutusaliti. Sasa kwa hali hii kama
CCM wanadhani wanaweza kukinusuru chama kwa kutufukuza na wajaribu
waone,” alisema. Naye diwani
mwingine alidokeza kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wilaya na mkoa ndio
wanatumika kuwarubuni madiwani hao kwa rushwa ili waondoe tuhuma hizo
dhidi ya meya, Anatory Amani.
Hivi karibuni, madiwani hao
walimgeuka Rais Jakaya Kikwete, wakipinga uamuzi wake wa kumtaka meya
kumaliza tofauti zake na mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki
kwa kile walichodai mgogoro huo si ugomvi kati ya wawili hao. Madiwani hao walipinga kauli hiyo wakisema suluhu ni kupinga ufisadi wa meya, kwani hakuna ugomvi binafsi kati yake na mbunge.
Akihutubia mkutano mjini Bukoba,
Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko kuu la kisasa katika manispaa hiyo
lazima uendelee na kwamba hakuna hoja ya kuendelea na malumbano
“yasiyokuwa na msingi”.
Madiwani hao 15 walisema malumbano
yaliyopo ni ya msingi kwa kuwa watu watakaobebeshwa deni la kurejesha
mikopo inayochukuliwa na meya ni wakazi wa Bukoba, si meya mwenyewe. Walisema
Rais ameonekana hafahamu kiini cha mgogoro, kwani kinachopingwa si
miradi, bali utaratibu ambao meya ametumia kuanzisha miradi hiyo
kifisadi bila kuzingatia maslahi ya wananchi.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja
5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhama ya
Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa
ipasavyo. Tuhuma nyingine ni
mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na
kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni
200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani.
Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa
ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari
ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka.
Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi
cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Barua ya madiwani hao,
iliwasilishwa jana asubuhi saa 2.30 na kupokelewa na Mkurugenzi wa
Manispaa hiyo, Shimwela L.E, ikiwa na saini za madiwani 16 kati ya 24
waliopo. Hata hivyo,
mkurugenzi huyo, alipotafutwa na gazeti hili alishindwa kukiri au
kukanusha kupokea barua hiyo, akisingizia kuwa kwa muda huo alikuwa
akitekeleza majukumu yake nje ya ofisi. “Unajua
Rais juzi aliacha maagizo mengi na baya zaidi ni lile la ugawaji wa
viwanja, hivyo asubuhi niliingia ofisini na kutoka kuelekea mitaani.
Nitakupa taarifa kesho kama barua hiyo imefika,” alisema.
Kwa mujibu wa kanuni za manispaa
hiyo yenye madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM,
ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya
madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.
Kanuni hizo pia zinaelekeza kuwa
mkugenzi atapaswa kuitisha kikao hicho ndani ya siku saba kuanzia tarehe
aliyopokea barua ya tuhuma hizo za madiwani na ndani ya muda huo
anapaswa kuwa amempatia mtuhumiwa tuhuma hizo ili aweze kuzijibu.
Alisema walikuwa wamesaini
madiwani 16 lakini waliamua kumtoa Balozi Kagasheki kwa vile ni waziri
na sehemu ya serikali, hivyo walibakia madiwani 15. Hata hivyo,
inajulikana kuwa hata Kagasheki anawaunga mkono itakapofika hatua ya
kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya. Madiwan
hao wanaompinga meya ni Richard Gaspar (CCM), Rabia Badru (CUF),
Murungi Kichwabuta (CCM), Winfrida Mukono (CHADEMA), Alexander Ngalinda
ambaye pia ni Naibu Meya (CCM), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa
CCM wa wilaya, Deusdedit Mutakyahwa (CCM), Robert Katunzi (CCM), Samwel
Ruhangisa (CCM) na Dauda Kalumuna (CCM).
Wengine ni Dismas Rutagwelela, Israel Mlaki wa CHADEMA na Conchester
Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho pamoja na
Ibrahim Mabruk, Felician Bigambo wa CUF.
Sosi : Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment