Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh
Ponda Issa Ponda amesema alichanganyikiwa kiasi cha kushindwa kujielewa
kwa muda baada ya kupigwa risasi.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na Mwananchi kwenye wodi binafsi ya Taasisi ya
Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi) alikolazwa jana, Sheikh Ponda alisema
kutokana na hali hiyo hakumbuki matukio yaliyofuata baada ya hapo.
“Sikumbuki
hata nilipata huduma ya kwanza hospitali gani kwa sababu sikuwa katika
hali ya kawaida. Mambo mengine yaliyotendeka kabla ya kujeruhiwa
ninayakumbuka vizuri,” alisema Ponda ambaye inasadikiwa kwamba alipigwa
risasi ya begani, Ijumaa iliyopita mjini Morogoro.
Alisema
alihutubia katika Kongamano la Waislamu kwa muda mfupi akizingatia muda
uliokuwa umetolewa kumaliza mkutano huo na baada ya hapo alishuka na
kupanda kwenye gari binafsi ambalo lilizingirwa na polisi ndipo akaamua
kushuka na kuanza kutembea kabla ya kujeruhiwa.
Mahojiano maalumu na Sheikh Ponda
Swali: Je, watu waliokupa huduma ya kwanza mara baada ya kujeruhiwa walikuta risasi iliyokujeruhi?
Jibu:
Nilipigwa risasi kwa nyuma ikatokea mbele kwa hiyo haikubaki mwilini
wala haikuonekana ilipoangukia kwa wakati huo maana kulikuwa na
purukushani.
Swali: Ulipata wapi huduma ya kwanza?
Jibu:
Kwa kweli kwa sasa siwezi kukumbuka nilihudumiwa wapi kwa sababu mara
baada ya kujeruhiwa sikuwa katika hali yangu ya kawaida,
nilichanganyikiwa.
Swali: Utathibitisha vipi kama ulipigwa risasi?
Jibu:
Bahati nzuri ni kwamba tukio hili lilitokea kweupe wapo wengi
walioshuhudia, kwa hiyo wanaweza kusaidia kuthibitisha na ushahidi
mwingine ni jeraha hili.
Swali: Nini msimamo wako baada ya tukio?
Jibu:
Nitaendelea kuzungumzia haki za Waislamu na siwezi kurudi nyuma. Pamoja
na kwamba wananiona mimi ni mtu mchochezi lakini wanaeneza chuki dhidi
yangu kwa njia wanazojua wao. Nitaendelea, risasi haitaninyamazisha.
Swali: Umehusishwa kufanya uchochezi Zanzibar, unalizungumzia vipi hilo
Jibu:
Zanzibar nilichozungumza ni kuhusu kesi dhidi ya viongozi wa Kundi la
Uamsho. Watu wamewekwa ndani kwa miezi tisa sasa, kwa mujibu wa sheria
za nchi yetu, kesi wanayoshtakiwa ina dhamana, sasa nikauliza kwa hao
viongozi, kwa nini hawazingatii sheria?
Kesi zina muda mrefu hazitolewi
uamuzi, nikawasisitiza wazingatie misingi ya sheria kwa kuwa hivyo
wanavyowatendea wananchi wajue kwamba hawastahili kupewa tena ridhaa ya
kuongoza nchi, nilifikisha ujumbe wangu.
Swali:
Kuna tukio la kumwagiwa tindikali mabinti wawili wa Uingereza
lililotokea Zanzibar, ambalo wewe pia unahusishwa, hili
unalizungumziaje?
Jibu: Sijaona huo ushahidi ambao
wanahangaika kunihusisha na tukio hilo, nahusishwa vipi? Matukio ya
kumwagiwa tindikali yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara huko kabla
sijakwenda kuhutubia. Vyombo vya dola vifanye kazi yake vyema ili
kubaini ukweli wa jambo hili.
Pia Mwananchi ilizungumza na mke wake, Sheikh Ponda, Hadija Ahmad ambaye alikuwa ameketi pembeni ya kitanda alicholazwa mumewe.
Swali: Unazungumziaje tukio hili la kujeruhiwa kwa mumeo?
Jibu:
Hili ni dhumuni la Serikali, lililenga moja kwa moja kumdhuru ili
kunyamazisha harakati zake za kutetea wanyonge. Ni tukio la kupangwa,
halijatokea bahati mbaya. Serikali inamfuatilia sana hivyo ililenga
kumnyamazisha.
Namshauri Rais (Jakaya Kikwete),
kuhakikisha kwamba haki za wanyonge zinawafikia, asije akafikiri hili
lililotokea kwa Sheikh Ponda ni suluhisho, ni vyema kufanya mazungumzo
ili kuweka mabadiliko.
Mtu
wa karibu wa Sheikh Ponda alisimulia jinsi walivyomsafisha kiongozi
huyo kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam na kukwepa vizuizi vya polisi
ambao walikuwa wakiendelea kumsaka.
“Msafara ulikuwa na
magari mawili. Moja lilitumika kwa uangalizi, lingine lilimbeba Sheikh
Ponda. Tulipofika Chalinze tulikuta kizuizi tukakikwepa kwa kupitia
Msata kisha Bagamoyo hadi Dar es Salaam na kumfikisha Muhimbili,”
alisema.
Msemaji
wa familia ya Sheikh huyo, Isihaka Rashid alisema hawaitambui tume
iliyoundwa na polisi kwa kuwa jeshi hilo ndilo linalotuhumiwa.
“Tunachofanya
hivi sasa ni kukusanya ushahidi wetu, kwa bahati nzuri tayari tumepata
mkanda wa tukio lenyewe ambao utatuwezesha kumbaini aliyemshambulia
Sheikh Ponda.
“Hatuwezi kuhitaji majibu ya hiyo
tume yao na hata leo kuna maofisa wa polisi kutoka Makao Makuu na Kituo
cha Kati, Dar es Salaam walifika wakitaka kumhoji eti kuhusu uchochezi
lakini alikataa kuzungumza hadi mwanasheria wake awepo, wakaondoka,”
alisema Rashid.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment