Tuesday, 13 August 2013

Mbeya wataka Z’bar iwe mkoa

Kyela. Imependekezwa kuwa Katiba Mpya itamke kuwepo kwa muundo wa Serikali moja ili kuweza kuulinda Muungano na kuondoa migogoro na migongano ya kimaslahi katika mgawanyo wa rasilimali.

Mapendekezo hayo yametolewa na Wajumbe wa Baraza la Katiba la Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya waliokuwa wakijadili ibara ya 57 iliyohusu muundo wa muungano.

Diwani wa Kata ya Ngonga, Kileo Kamomenga alisema muundo wa Serikali mbili au tatu ni hatari, kwani unahatarisha Muungano na pia unatoa mwanya kwa Serikali moja kufanya uhusianona nchi nyingine ambazo hazitakuwa na nia njema na Watanzania .

“Kwa mfano katika ibara 62 kifungu kidogo cha (2) kinatoa uhuru kwa kila mshirika wa Muungano kuwa na uwezo wa kuanzisha uhusiano au ushirikiano na jumuiya au taasisi yoyote ya kikanda au kimataifa kitu ambacho mimi naona ni hatari kwa taifa letu, ni vema tukawa na Serikali moja, Zanzibar iwe ni moja ya mikoa ya Serikali moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”alisema

Alisema kitendo cha Zanzibar kuwa na bendera yake, wimbo wake wa Taifa, Rais wake ni kuifanya kuwa nayo ni nchi inayojitegea na watu wake kujiita wao ni Wazanzibari na siyo Watanzania “Hivyo kama tuna lengo la kudumisha Muungano ni lazima tuwe na Serikali moja kuliko ilivyo hivi sasa,”alisema

Naye mjumbe, Clifford Mwaikinda alisema kuwa muundo wa Serikali moja utapunguza kubeba nzigo mkubwa kiuchumi na madaraka na kuwepo kwa usawa katika kugawanya rasilimali za nchi na kuondoa upendeleo kwa Serikali ya Zanzibar ambayo ilikuwa inanufaika na mambo mengi kutoka Tanganyika.

CHANZO:Mwananchi

No comments:

Post a Comment