Friday, 9 August 2013

ABUNUWASI KAMA KADHI

Abunuwasi alikuwa mshairi maarufu katika mahakama ya khalifa Haruni Rashidi. Siku moja Khalifa alimteua Abunuwasi kuwa Kadhi mkuu wa jiji, Asubuhi moja mpishi wa keki akaenda kuonana na Kadhi na kulalamika kuhusu bwana mmoja masikini. Mpishi analalamika: 'huyu ombaomba anasimama tuu karibu ya kibanda changu pale sokoni ninapo oka keki zangu tamu. ananusa tuu harufu nzuri bila kunilipa, kwahiyo mimi ninakuwa nikifanya kazi bure.'
Abunuwasi kama Kadhi mwenye busara akalifikiria swala hili kwa muda kidogo, kisha akatoa hukumu: akamwambia mpishi ''unachosema ni kweli kabisa. huyu ombaomba amefaidi harufu ya keki zako na kwa kufanya hivyo ametumia matunda ya kazi yako. Kwa hilo itabidi akulipe fidia. Nafikiri dinari mbili za dhahabu zitakuwa ni fidia inayofaa kabisa.'' Macho yampishi yakang'aa aliposikia dinari mbili, lakini masikini akalalamika: "Mungu mkubwa, mimi ni masikini, sina pesa, hata ukinitingisha hutasikia mlio wa njuga. Unaweza ukakamua maji ya matunda kwenye zabibu lililo kauka? Abunuwasi akalifikiria tena hili kwa muda alafu akasema: ikiwa wewe ni masikini, nitakulipia hii fidia toka mfukoni kwangu.' Abunuwasi akatoa sarafu mbili, mpishi akanyoosha mkono wake wa kulia kwa shauku kubwa ili apokee fidia yake.
Mara moja Abunuwasi akabadilika na kuanza kumuhoji mpishi,
Abunuwasi: Je huyu masikini alikula keki zako?
Mpishi: Hapana Mkuu
Abunuwasi: Je alizinyofoa?
Mpishi: Hapana Mkuu
Abunuwasi: Labda aliziharibu kwa kuzipumulia?
Mpishi: eeh, Hapana Mkuu
Abunuwasi: Kwa hiyo unaweza ukaziuza ama umeshaziuza?
Mpishi: Ndio Mkuu ninaweza nikaendelea kuziuza na zingine nimeshauza
Abunuwasi: Kwa hiyo basi kama huyu bwana hajala, hajanyofoa wala kuzipumulia keki zako, zaidi ya kuvuta harufu nawe basi utafidiwa na sauti. fungua masikio yako kwa makini ili nawe ufurahie sauti za dinari mbili za dhahabu. ikabidi mpishi afanye hivyo kwa sababu hii ndio ilikuwa fidia pekee ambayo angeweza kupata

No comments:

Post a Comment