Wednesday, 7 August 2013

Wiki ngumu kwa CCM: Meya wao ang'olewa Bukoba, Kigoma hali tete

IMEKUWA wiki ngumu kisiasa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho viongozi wake wa kitaifa wanahaha kila kona kujaribu kunusuru mgawanyiko uliopo.

Mambo matatu makuu yanayokiandama chama hicho ni mgogoro wa meya wao na madiwani mjini Bukoba, uchaguzi wa wenyeviti wa halmashauri mkoani Kigoma na kukwama kwa propanda zao za ugaidi dhidi ya CHADEMA.

Madiwani wa CCM, CHADEMA na CUF, tayari juzi walimfukuza rasmi Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.

Waliopiga kura ya kutokuwa na imani na meya ni madiwani 15 waliosaini fomu ya hati ya kumtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuitisha kikao cha dharura kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya.

Diwani wa 16 ambaye hakusaini lakini aliridhia uamuzi huo ni Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki, ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii.

Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa madiwani hao kufikia uamuzi huo, kwani walikumbana na mikikimikiki ya meya mwenyewe akisaidiana na uongozi wa CCM mkoani na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe.

Habari kutoka vyanzo vya karibu na uongozi wa CCM mkoani Kagera vililiambia gazeti hili kuwa kutokana na uamuzi huo, na kwa kuwa CCM na serikali mkoani humo hawataki meya aondoke, chama hicho tawala kimepanga kuwafukuza madiwani wao walioweka sahihi zao kumfukuza meya.

Tayari taarifa zimevuja kwamba CCM itaitisha kikao Agosti 10, mwaka huu kuwafukuza madiwani wake hao ambao wameapa kwamba liwalo na liwe, hawawezi kuacha ufisadi utumike kama kigezo cha kuleta miradi Bukoba.

Baadhi ya madiwani waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa wanatembea na kadi zao za CCM mfukoni tayari kuzikabidhi iwapo uongozi utaamua kulinda ufisadi wa meya na kuwachukulia hatua wao.

Vyanzo vyetu vya habari vinasema hatua ya madiwani hao kumwondoa meya ilikuwa kama igizo. Mkurugenzi alikataa kuitisha kikao cha baraza la madiwani ambacho ndicho kingemfukuza.

Lakini kwa kutambua kuwa idadi iliyohitajika ili meya aondoke ni madiwani 16 na tayari ilikidhi matakwa hayo, madiwani hao walikusanyika kufanya uamuzi huo mgumu.

Kabla ya hatua hiyo kufikiwa, juzi asubuhi meya na mkurugenzi wa manisapaa hiyo walikwenda mahakamani kuweka pingamizi la kuzuia madiwani kuitisha kikao cha kumwondoa meya, kwa hoja kwamba shauri lao lilikuwa mahakamani.

Hata hivyo, meya na mkurugenzi waligonga kisiki mahakamani, baada ya kuambiwa kuwa shauri lililokuwa mahakamani lilikuwa tofauti na uamuzi waliokuwa wanataka kuchukua.

Taarifa hizo zilisema kuwa uamuzi wa meya na mkurugenzi kwenda mahakamani ulitokana na agizo la mkuu wa mkoa ambaye alimwandikia mkurugenzi huyo akimzuia kuitisha kikao cha baraza la madiwani kama alivyokuwa ametakiwa na madiwani hao kwa mujibu wa kanuni.

Baada ya madiwani hao kuona jitihada za meya na mkurugenzi kuzuia azima yao, na walipogundua mahakama imekataa kutoa hati ya zuio la kikao chao, walikusanyika katika ofisi za manispaa hiyo ili kufanya kikao, lakini mkurugenzi alikataa kufungua.

Badala yake waliamua kufanya kikao nje ya ukumbi wa halmashauri, wakamfukuza meya na kuandika muhtasari ambao wataupeleka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Taarifa zaidi zinasema kabla ya hatua hiyo ya madiwani, CCM ilikuwa imeitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa kujadili hatima ya sakata hili, hasa madiwani wa chama chao.

Uamuzi wa kuita kikao hicho ulitokana na maagizo ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Phillip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, ambao kwa nyakati tofauti Jumamosi iliyopita waliwasiliana na Mkuu wa Mkoa na Mweyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera kuwataka wamalize mgogoro huo “kwa busara.”

Katika kikao hicho cha Jumapili, mara baada ya ufunguzi, wajumbe walikaa kimya kama walioduwaa. Ndipo alipoibuka mjumbe kutoka Karagwe na kutoa hoja kwamba madiwani wa CCM wafukuzwe kwa sababu wanachafua chama.

Hoja yake iliungwa mkono na wajumbekutoka Muleba na Missenyi. Hata hivyo, mkuu wa mkoa alionya kwamba hatua ya kufukuza madiwani hao ingepingana na ushauri aliopewa na Kinana na Mangula, wa kumaliza mgogoro kwa “kutumia busara.”

Akapendekeza kwamba wapewe siku saba za “kujirudi,” waondoe barua yao ya kutokuwa na imani na meya; na kwamba baada ya hapo kama watakataa ndipo wafukuzwe.

Inadaiwa kuwa mjumbe mwingine akasema kuwa hata ushauri wa mkuu wa mkoa una dosari, kwa kuwa madiwani hao walikuwa wameshaandika barua kwa mujibu wa kanuni, na zilikuwa zimepita siku nne, huku wakihesabu.

Kwa mujibu wa kanuni za halmashauri, barua kama hiyo ikishaandikwa, mkurugenzi analazimika kuita kikao ndani ya siku saba baada ya kumpa meya taarifa hizo ili ajiandae kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mjumbe huyo alimuonya mkuu wa mkoa kwamba halmashauri haiongozwi na amri au maelekezo ya mkuu wa mkoa bali kanuni za halmashauri.

Kikao hicho cha Jumapili kiliahirishwa kwa mkanganyiko huo juu ya hatua wanayopaswa kuchukuliwa madiwani hao.

Hali tete Kigoma

Nako mkoani Kigoma hali ni tete kwa CCM, ambapo Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amelazimika kutua kimya kimya kutuliza mgogoro unaofukuta.

Baadhi ya madiwani wa CCM wametishia kuachia ngazi na kujiunga na upinzani kwa kile wanachodai kutoridhishwa na uamuzi wa vikao vya uteuzi wa wagombea wa uenyekiti wa halmashauri.

Kigoma ni ngome kubwa ya upinzani, ambapo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, kambi hiyo ilizoa viti vitano vya ubunge huku CCM ikiambulia vitatu.

Madiwani wanne wa CCM, Elisha Bagwaya (Kibande), Alois Ntilluhoka (Biharu), Wilson Ruzibila (Kishanga) na Venance Mporogonyi, wamejaza fomu za kuomba nafasi za uenyekiti katika halmashauri mpya ya Buhingwe.
Baada ya madiwani hao kujaza fomu, kikao cha kamati ya siasa ya mkoa kilikaa na kurudisha majina mawili ya Bagwaya na Mporogonyi.

Habari za ndani zilidai kuwa madiwani watano kati ya 12 hawakupiga kura kumpata mgombea, ambapo kati ya hao saba waliopiga kura, watano walimchagua Bangwanya na wawili walipiga kura za hapana.

Hali hiyo iliibua hofu ya CCM kushinda kiti hicho, hatua iliyolazimu chama kuwaita madiwani ambao hawakumuunga mkono mgombea kwenye kamati ya maadili ngazi ya mkoa kuhojiwa.

Pamoja na vitisho na ukali kutoka kwa baadhi ya wajumbe, madiwani hao walionesha msimamo wao na kusababisha kikao hicho kukosa muafaka.

Mgogoro kama huo umejitokeza katika kikao cha baraza la madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, ambalo lina madiwani wengi wa CCM, ingawa mgombea wao alipigiwa kura ya hapana hivyo kufanya mshindi kutopatikana.

Halmashauri ya Kibondo ilikuwa inaundwa na halmashauri za Wilaya ya Kibondo na Kakonko, ambapo nafasi ya mgombea wa unyekiti alikuwa pekee kutoka CCM, Ally Gwanko, aliyepigiwa kura nane za ndiyo na kumi za hapana huku makamu mwenyekiti, Emily Mfanye, akipigiwa kura nyingi za hapana.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Leopard Ulaya, ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi huo alisema kuwa kulingana na matokeo hayo kwa mujibu wa utaratibu uchaguzi utarudiwa baada ya siku 60.

Hali hiyo imeleta ‘sintofahamu’ ndani ya CCM kutoka na chama hicho kuwa na madiwani 12, ilikinganishwa na sita wa CHADEMA na NCCR-Mageuzi.

Tukio jingine lililoinyong’onyesha CCM wiki hii ni uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kulitupilia mbali shitaka la ugaidi lililokuwa likiwakabili vijana watano wa CHADEMA.

Uamuzi huo wa mara ya pili baada ya ule wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kufuta mashtaka kama hayo kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, utakuwa pigo kwa CCM kutokana na viongozi wake kutumia propaganda za ugaidi kukichafua CHADEMA.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba na Nape Nnauye walitumia tuhuma hizo za ugaidi dhidi ya CHADEMA kuwatisha wananchi wa Arusha wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani hivi karibuni.

Mwigulu amekuwa akitamba ndani na nje ya Bunge kuwa anao ushahidi kuwa CHADEMA inajihusisha na vitendo vya kigaidi na kwamba angetoa mahakamani wakati ukifika.

Kwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu ambayo pia imeuonya upande wa Jamhuri kuacha michezo ya kugeuza mashtaka ya jinai kuya ya ugaidi, CCM itakuwa imenyong’onyeshwa na propaganda zao hizo.


Source: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment