Maelfu wajitokeza kuandamana tena Misri
Maelfu ya wafuasi wa Rais wa Misri aliyeondolewa
madarakani Mohammed Morsi wameanza maandamano mengine mjini Cairo, huku
kukiwa na hofu ya kuzuka makabiliano zaidi. Maafisa wa usalama
wamezingira barabara kuelekea medani ya Ramses ambapo maandamano hayo
yalipangwa kufanyika. Maandamano ya sasa yanajiri siku mbili baada ya
jeshi kuvunja kambi ambapo wafuasi wa vuguvugu la Muslim Brotherhood
walikua wamesalia kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Makabiliano yalizuka na zaidi ya watu 600
wakauawa, maelfu walijeruhiwa.Maandamano zaidi yanaendelea nje ya mji
mkuu Cairo na taarifa zinasema watu wanne wameuawa kwenye makabiliano
eneo la Ismailia. Polisi wa Misri wameamrishwa kutumia risasi za moto
kulijinda na kulinda majengo ya serikali dhidi ya kushambuliwa.
Huku utawala wa mpito ukitangaza hali ya
hatari, mwandishi wa BBC aliyeko Cairo amesema taharuki imetanda mji
mzima.Maelfu walikusanyika nje ya msikiti mmoja baada ya Muslim
Brotherhood kuwaomba wafuasi wao kuandamana baada ya sala ya ijumaa
wakiitaja kama siku ya hasira.
Magari ya kijeshi yanashika doria mjini Cairo,
na njia ya kuingia medani ya Tahir kitovu cha maandamano ya mwaka 2011
yaliyomuondoa madarakani Hosni Mubarak imefungwa. Huku haya yakiarifiwa
wapinzani wa Mohammed Mosri pia wamepanga kuandamana dhidi ya mahasimu
wao. Wakati huo huo watu wameombwa kulinda makaazi yao, makanisa na
biashara. Wakristo nchini Misri wamekuwa wakilengwa katika siku za
karibuni na makundi ya kiisilamu yenye misimamo mikali. Jumla ya
makanisa 25, makaazi na biashara yalishambuliwa hapo Jumatano na
Alhamisi.
chanzo;BBC
No comments:
Post a Comment