Vurugu Misri: Cairo kimya baada ya vifo.
Mji mkuu wa Misri Cairo umeripotiwa kuwa kimya, baada
ya operesheni ya kinyama dhidi ya waandamanaji wanaomuunga mkono rais
aliyepinduliwa Mohammed Morsi kupelekea vifo vya mamia ya raia. Mauaji
hayo yamezua shutuma kutoka jamii ya kimataifa.
Zaidi ya watu 278 waliuwawa wakati maafisa wa
usalama waliposhambulia kambi mbili za wafuasi wa Bwana Morsi. Kambi
hizo zilianzishwa mwezi uliopita kupinga hatua ya jeshi kumng'oa rais
huyo anayezingatia itikadi za kiislamu.
Hali ya hatari imetangazwa na amri ya kutotoka nje nyakati za usiku kutolewa katika miji mikuu ya Misri.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani
John Kerry amesema matukio ''mabaya'' yaliyotokea ni ''pigo kubwa kwa
juhudi za maridhiano''.
Afisa wa mashauri ya kigeni katika Muungano wa
Ulaya, EU, Catherine Ashton na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-moon kadhalika wamekosoa hatua ya maafisa wa usalama kutumia nguvu
dhidi ya raia.
Raia wa Misri wanaamkia siku nyingine yenye
shaka juu ya mustakabal wao, anasema mwandishi wa BBC Bethany Bell
aliyepo mjini Cairo.
Hata baada ya amri ya kutotoka nje kuondolewa
Alhamisi asubuhi, kumekuwa na magari machache katika barabara za
katikati mwa Cairo na madaraja yanayovuka mto Nile, anasema mwandishi
wetu.
'Pigo kubwa'
Waandamanaji wamekuwa wakiitisha bwana Morsi aliyetimuliwa na jeshi tarehe 3 Julai, kurejeshwa madarakani.
Vuguvugu la undugu wa Kiislamu, Muslim
Brotherhood, ambalo lilifadhili maandamano ya hivi punde katika medani
ya Nahda na pia karibu na muskiti wa Rabaa al-Adawiya, limesema kuwa
idadi ya kweli ya watu waliouwawa siku ya Jumatano inazidi 2,000.
Kwa mujibu wa serikali ya mpito inayoungwa mkono
na jeshi, raia 235 waliuwawa kote nchini, pamoja na maafisa wa polisi
43. Tarakimu hizi haziwezi kuthibitishwa kwa njia iliyo huru.
Bwana Kerry amesema juhudi za maridhiano ya kisiasa nchini Misri zimepata "pigo kubwa".
"Hii ni hatua muhimu kwa Wamisri wote,"
akaongeza bwana Kerry. " Mkondo wa vurugu utaelekea tu kwa msukosuko
zaidi, mkasa wa kiuchumi na mateso."
Afisi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-moon imesema kuwa ''anasikitika kwamba maafisa wa Misri waliamua
kutumia mabavu wakati Wamisri wengi wanataka taifa lao kusonga mbele kwa
amani katika mfumo utakaoongozwa na Wamisri wenyewe ili kuafikia
maendeleo na demokrasia".
"Akilaani vikali" vurugu zilitokea Bi. Ashton
amesema kuwa " ni juhudi za pamoja pekee kati ya Wamisri wote pamoja na
jamii ya kimataifa ndizo zitakazorejesha taifa hilo katika demokrasia
inayowashirikisha wote na kukabili changamoto zinazokabili Misri"
CHANZO:BBC
No comments:
Post a Comment