HAYA NDO MASHITAKA ALIYOSOMEWA SHEIKH PONDA AKIWA HOSPITALINI
KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda
Issa Ponda (54), amesomewa shtaka akiwa kitandani katika Kitengo cha
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI).
Katika shtaka hilo, Ponda anadaiwa kuwahamasisha wafuasi wake kufanya kosa.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Riwa, Mwendesha
Mashtaka wa Serikali, Tumaini Kweka, alidai kuwa uhamasishaji huo
ulifanyika sehemu mbalimbali nchini kuanzia Juni 2 hadi Agosti 11 mwaka
huu.
Kweka alidai kuwa kosa hilo ni kinyume cha sheria ya makosa ya jinai kifungu 390 na 35 ya kanuni za adhabu.
Kutokana na shtaka hilo, Hakimu Riwa aliahirisha kesi hadi Agosti 28
na kutoa agizo Sheikh Ponda aendelee kuwa chini ya uangalizi wa vyombo
vya dola wakati akiendelea na matibabu.
Baada ya Hakimu Riwa kuahirisha kesi, wakili wa mshtakiwa Nasoro
Jumaa, alilaumu utaratibu uliotumika na kusema kuwa mahakama imefanya
kazi nje ya muda wa kawaida wa saa za kazi za kiserikali.
Alisema mawasiliano ya awali ilikuwa askari na Tume ya Haki Jinai ya
Jeshi la Polisi kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kufanya mahojiano
na Sheikh Ponda.
Aliongeza kuwa baada ya maofisa hao kufika hali ya Sheikh Ponda
haikuruhusu mahojiano kufanyika na ilipofika saa kumi jioni kila mmoja
alitawanyika.
Jumaa alisema kuwa wakiwa wanakaribia geti la kutokea Muhimbili,
walipigiwa simu kuwa Sheikh Ponda anasomewa mashtaka, hatua aliyodai
kuwa iliwashangaza.
“Kama walikuwa na dhamira ya kumsomea mashtaka wangetuambia, kwa kuwa
ni haki ya msingi kwa mtuhumiwa kuwa na mwanasheria wake kwa ajili ya
kujua taratibu zilizotumika,” alisema.
Alisisitiza kuwa baada ya kupata hati ya mashtaka wanajiandaa kupinga
kosa hilo kwa kile alichoeleza kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
haina uwezo wa kusikiliza kosa la aina hiyo.
Aliongeza kuwa kabla ya kufikiwa kwa hatua ya kumsomea shtaka Sheikh
Ponda, walishaandika barua ya kutokuwa na imani na Tume ya Haki Jinai ya
Jeshi la Polisi katika uchunguzi wao kwa kile alichoeleza kuwa ni
watuhumiwa wa kwanza katika tukio la kujeruhiwa kwa mteja wake.
Awali kabla ya kesi hiyo kusomwa maeneo mbalimbali ya Hospitali ya
Muhimbili hususan jirani na jengo alilolazwa Sheikh Ponda, yalikuwa
yamezingirwa na makachero wa polisi wakiwa na magari matano ya Kikosi
cha Kutuliza Ghasia.
Magari mawili yenye namba PT 2072 na PT 2061 yalikuwa jirani na mlango
wa kuingilia katika kitengo cha mifupa huku askari wakiwazuia wananchi
wasiende kumuona Ponda kwa kile walichoeleza kuwa kuna shughuli za
kiserikali zinaendelea.
Miongoni mwa watu waliozuiwa ni wakili maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari.
-Tanzania daima
No comments:
Post a Comment