Friday, 9 August 2013

WAJINGA NDIO WALIWAO

Paliondokea mtu katika kisiwa cha Unguja, enzi za Seyid Majid Bin Said, naye akikaa mjini. Na mtu huyu alikuwa hana kazi maalum, kazi yake ilikuwa ni kuwafuata Waarabu wakubwa wakubwa, na kupata manufaa yake kwao. Na kazi zamani hizo ilikuwa watu kufunga bidhaa na kwenda bara kufanya biashara, na kulima vyakula na kuuza.


Na yeye alikuwa mtu mmoja asiyetaka kazi ya namna hii. Hata hatima akaonelea mji haumweki. Akatafuta kanzu yake njema akavaa, na kilemba chake cheupe, na msahafu wake kwapani, akashika njia kwenda pande za mashamba kutarazaki. Na kazi aliyoichagua ni kazi ya ualimu kusalisha watu. Lakini yeye hajui kusoma hata herufi moja. Alichagua kwenda shamba kwa Wahadimu kwa kuwa huko ndiko walikokuwa wajinga wasiojua kusoma, na hata dini ya Kiislamu ilikuwa haijaingia kwao bado.


Basi Mwalimu akawasili Unguja Ukuu. Wahaimu walipomwona mgeni wakamkaribisha sana. Hata waliposikia kuwa yeye ni mwalimu wakazidi kumkaribisha na kumheshimu. Na yeye mwenyewe ikawa mchana kutwa kufunua msahafu, kutazama tu, watu wanadhani anasoma! Akapewa nyumba bure na chakula kwao. Hatima akawaambia, Jengeni msikiti nikusalisheni. Wahadimu wakajenga msikiti. Hata wakati wa kusali ulipojiri mwadhini hapana, maana wale wenyeji hawajui.


Basi ikawa kazi ya mwenyewe Mwalimu kuadhini. Lakini naye vilevile hajui kitu. Akasimama akaadhini hivi:- Allah Akbar! Allah Akbar! Wajinga ndio waliwao, Wajinga ndio Waliwao. Allah Akbar ! Watu wakajaa msikitini. Huyu mwalimu kama nilivyosema hajui kusoma, si kukuambia kusalisha! Lakini watu wamekwisha kuwamo msikitini, ikawa hana hila ila kusalisha. Akaenda panapo Kibla, akasalisha hivi:- M, m, m,m ,m,m Wajinga ndio waliwao, Amin.


Ikawa kila akisema M,m,m ,m,m ,m ,m Wajinga ndio waliwao, Wajinga ndio Waliwao, Wahadimu huitikia Amin! Ikawa kila akiinama na kuinuka maneno ni hayo hayo. Na Wahadimu wakidhani asema Kiarabu, wakawa wamekazana tu, Amin! Zilipokwisha sala wakatoka nje. Wahadimu wakamsifu sana mwalimu wao jinsi anavyosalisha vizuri. Ikawa hivi hali ya mambo kwa siku nyingi kupita. Wakamfanyia mshahara mwema.


Siku moja akatoka Malimu wa kweli mjini anayejua kusoma na kusalisha ili kwenda kutembea shamba. Akafika Unguja Ukuu. Akapata habari kama mjini pana Mwalimu mmoja arifu sana, ndiye anayesalisha msikitini. Na huyu mwalimu mgeni asiende kumtazama, akangoja mpaka wakati w sala.


Wakati wa sala ulipojiri akamsikia mwadhini anaadhini. Lakini maneno yake yakamstusha sana. Allah akbar! Allah akbar! Wajinga ndio waliwao. Allah akbar! Yule mgeni asiseme neno, akaenda msikitini, akakuta watu wamejaa. Na mbele yao panapo kibla yuko mtu anayemjua tangu mjini, naye kumjua kwake hajui kitu. Basi akamsogelea kule kule mbele ili amsikilize vema. Na mwalimu alipomwona huyu mgeni akastuka sana maana naye amjua tangu mjini. Akawaza kuwa leo uongo wangu utabainika. Lakini mara akili zikamjia hivi:- M,m,m,m,m Mwalimu usinibaini, nikipata sita, tatu zangu, tatu zako, Wajinga ndio waliwao Amin! Na maneno haya wakisikiana wao wawili tu, maana walikaaa karibu karibu. Akashika kusalisha kwa maneno yale yale. M, m,m,m,m,m Mwalimu usinibaini, Wajinga ndio waliwao, nikipata nane, nne zangu na nne zako, Amin.


Akasalisha hivi mpaka mwisho, wakatoka. Walipotoka nje wale walimu wakaamkiana kwa vicheko sana. Watu walipowaona wanacheka,wakidhani wanacheka yao ya huku nje, maana wanajuana. Kumbe wanacheka yaleyale ya Msikitini: Mwalimu usinibaini, wajinga ndio waliwao, nikipata nane, nne zangu, nne zako. Wakakaa katika hali hii wakiwala wajinga, mpaka walipochoka, wakaja zao mjini na wingi wa mapesa.


Hadithi hii inatufundisha nini? na hali ya Tanzania tukiangalia hali halisi ya uwekezaji feki pamoja na mambo mengine. JE sisi pia sio miongoni mwa hao wajinga ndio waliawao?


No comments:

Post a Comment