Tuesday 23 July 2013

Tsvangirai aandamwa na kashfa huku uchaguzi ukikaribia

Morgan Tsvangirai, waziri mkuu wa Zimbabwe anayeandamwa na kashfa za kimapenzi
Kituo cha Televisheni cha taifa cha Zimbabwe kimeanzisha kampeni ya kumchafulia jina Morgan Tsvangirai, mpinzani wa rais Robert Mugabe katika uchaguzi mkuu wa tarehe 31,Julai, 2013, na tayari athari zimeanza kuonekana.
Katika matangazo yanayorushwa na kituo hicho cha televisheni ya taifa, kituo hicho kinawaonyesha wapenzi wa zamani wa Morgan Tsvangirai, wakisimulia jinsi alivyowatelekeza. Baada ya simulizi zao huingia maafisa wa chama cha ZANU-PF cha Rais Robert Mugabe, wakiwahimiza wapiga kura kuepuka kumchagua Tsvangirai, ambaye ni waziri mkuu katika serikali ya mpito, wakisema hafai kuliongoza taifa.
Ingawa yapo maswali kadhaa juu ya lugha na mtindo vinavyotumiwa katika matangazo hayo yanayomlenga Tsvangirai, hususan kwa kuzingatia kuwa Zimbabwe ni nchi inayodai kuzingatia maadili, tayari athari zake zimeanza kuonekana. Hata wale watu ambao siku za nyuma walikuwa wafuasi sugu wa Morgan Tsvangirai, wameanza kumuona waziri mkuu huyo kama mtu ambaye kajitafutia matatizo mwenyewe, na hana mtu mwingine wa kumlaumu.
Baadhi wajiengua
Morgan Tsvangirai akiendesha kampeni ya urais Morgan Tsvangirai akiendesha kampeni ya urais
Mmoja wa wafuasi hao, Gerald Mlambo, amesema miaka mitano iliyopita alikuwa tayari kufa kwa ajili ya Tsvangirai, na alikuwa hawezi kuvumilia mtu aliyemkashifu kiongozi huyo. ''Leo hii'', amesema Mlambo, ''Nimeingiwa na mashaka kiasi kwamba sitaki kushiriki katika kampeni kali zinazoendelezwa na chama cha Morgan Tsvangirai, dhidi ya rais Mugabe''.
Kashfa za kingono, na kushindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi akiwa waziri mkuu, vimeishusha hadhi aliyokuwa nayo Morgan Tsvangia miongoni mwa wafuasi wake, ambayo ilitokana na ujasiri wake wa kusimama kidete dhidi ya utawala wa kimabavu wa miongo mitatu wa rais Robert Mugabe.
Mke wa kwanza wa Morgan Tsvangirai, Susan, alikufa katika ajali ya gari mwaka 2009, mwaka mmoja tu baada ya mumewe kuingia katika serikali ya umoja wa kitaifa, akiwa na wadhifa wa waziri mkuu. Tangu wakati huo, Tsvangirai mwenye umri wa miaka 61 amezaa mtoto na binti mwenye umri wa miaka 22, na ameburuzana mahakamani na mpenzi mwingine waliyeachana.
Vile vile, vyombo vya habari vya Zimbabwe vilisheheni habari kutoka kwa mpenzi mwingine wa Morgan Tsvangira raia wa Afrika Kusini, ambaye alisema kuwa waziri mkuu huyo wa Zimbabwe alimtosa kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu, baada ya miaka miwili ya mahaba yaliyoambana na starehe zenye gharama kubwa.
Hata Mugabe sio malaika
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Je yeye ni safi? Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Je yeye ni safi?
Lakini wafuasi wa Morgan Tsvangirai wanasema kuwa hata Mugabe mwenyewe siyo malaika, kwani amezaa watoto wawili nje ya ndia yake na mkewe wa sasa Grace, ambaye kabla ya kumuowa alikuwa katibu muhtasi wake. Mugabe anamzidi miaka 41 Grace ambaye ni mke wake wa pili.
Chama cha MDC cha Morgan Tsvangirai, kimesema kampeni inayoendeshwa na Mugabe na Chama chake kumchafulia jina mgombea wao, ni ushahidi tosha kwamba ZANU-PF kimekosa mwelekeo ulio na msingi katika masuala muhimu kwa taifa.
Hata hivyo, kashfa zinazomkabili Tsvangirai juu ya uhusiano wake wa kimapenzi, pamoja na kushindwa kuzitekeleza ahadi muhimu za serikali yake, kama vile kuimarisha uchumi na kupunguza idadi ya wasio na ajira, vimedidimiza mng'aro wa nyota yake kisiasa.
Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu
CHANZO: .dw.de

No comments:

Post a Comment