Sitta ahoji harambee za Lowassa Makanisani na sasa misiktini
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amehoji
walipo na majina ya wanaoitwa “Marafiki wa Lowassa” wanaomchangia
mamilioni ya fedha za kusaidia harambee mbalimbali nchini.
Akizungumza na Raia Mwema wiki hii, Sitta alisema ni ajabu
kwamba ‘marafiki’ hao wamekuwa wakitajwa tu bila ya kufahamika ni
akina nani, wana ukwasi kiasi gani na wameupataje ukwasi huo.
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amekuwa akichanga michango
ya fedha katika harambee mbalimbali nchini huku akisema fedha
anazochanga si zake binafsi bali ni michango pia ya rafiki zake.
Na akizungumza kupitia kwa msaidizi wake jana Jumanne, Lowassa alisema
hoja kwamba marafiki zake wanaomchangia hawafahamiki haina ukweli
wowote kwa kuwa amekuwa akiwataja hadharani kwa majina kila
wanapomchangia.
Lakini Waziri Sitta alihoji, alisema ya kuwa, haiingii akilini watu
kumchangia mwanasiasa huyo bila ya kuwa na sababu za msingi za kufanya
hivyo.
“Nyie waandishi mnatakiwa mlisaidie taifa kwenye hili. Mtu anapita
nchi nzima anachanga mamilioni ya fedha na anasema si zake bali ni za
rafiki zake. Lakini hatuambii rafiki zake hao ni akina nani. Hatujui
kama hata rafiki zake hao wanachangia kodi kwa serikali.
“Lakini, swali kubwa la kujiuliza zaidi hapa ni hili; inakuaje
michango ya kwenye taasisi za kidini mtu ampe Lowassa na asiende
mwenyewe kutoa kanisani au msikitini kwake?
“Ninachojua mimi, mbinguni hakuna c/o (kupitia kwa). Ina maana
Wasamaria hawa wanajua kwamba ili uende mbinguni ni lazima mchango
wako utolewe na huyo bwana (Lowassa)?” alihoji Sitta.
Katika mahojiano hayo, Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa
wakati wa kashfa ya Richmond iliyomwandama Lowassa, alisema kizazi cha
Watanzania wa sasa kina shida kubwa kwenye kupata viongozi walio
waadilifu.
Alisema uongozi sasa umekuwa fursa ya kuchuma mali badala ya kutumikia
umma, na kwamba hata katika matukio ya kuongeza heshima kwa taifa,
watu wanayatumia kutia aibu taifa.
Sitta aliyasema hayo akigusia vitendo vya ufisadi vilivyofanyika wakati wa mkutano wa Smart Partnership uliofanyika nchini mapema mwezi huu ambapo ripoti za vitendo vya ufisadi zimeanza kuibuka.
“Mkutano ule ulitakiwa ujenge heshima yetu. Lakini majizi yameingia na
sasa taifa limeingia katika kashfa nzito. Kila kitu sasa ni ufisadi
tu. Tukiendelea hivi hivi hatutafika kokote,” alisema mwanasiasa huyo.
Kauli hiyo ya Sitta imekuja huku Lowassa akizidi kuchanja mbuga katika
kuendesha harambee ndani ya makanisa na misikiti, na mara kwa mara
harambee anazoendesha na kufanikisha ni zaidi ya shilingi milioni 200.
Kwa mfano, hivi karibuni akiwa jijini Mwanza Lowassa alifanya harambee
ya Sh. milioni 590, ikiwamo michango yake na watu anaowaita “rafiki
zake”, lakini pia amewahi kufanya harambee mkoani Ruvuma, wilayani
Nyasa, ambako zilikusanyaswa Sh. milioni 300.
Lowassa pia amewahi kufanya harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa
Katoliki Nyakato Mwanza ambako alichangisha Sh. milioni 200, amewahi
kuchangisha Sh. bilioni moja kwa ajili ya Chama cha Kuweka na Kukopa
(Saccos) cha Walimu wa Moshi Vijijini. Amewahi pia kuendesha harambee na
kukusanya Sh milioni 134 Babati, mkoani Manyara.
Ingawa Lowassa binafsi amewahi kunukuliwa akisema si tajiri wa fedha
isipokuwa ni tajiri wa watu, anatajwa kumiliki biashara kadhaa kubwa
pamoja na mali nyingi kama majumba katika maeneo mbalimbali nchini.
Alipotafutwa Lowassa, ili pamoja na mambo mengine, aweze kutoa
ufafanuzi juu ya baadhi ya hoja hizo zilizoibuliwa na Sitta dhidi yake,
mwanasiasa huyo alimwelekeza mwandishi wetu kuzungumza na Katibu wake,
aliyejitambulisha kwa jina la Boniface Chami.
Akijibu ni kwa nini Lowassa hawataji hadharani marafiki zake hao
wanaodai wanamchangia mamilioni ya shilingi anayoyatoa kwenye harambee
zake, Chami, alisema hoja hiyo haina ukweli wowote kwa kuwa Lowassa
amekuwa akiwataja hadharani kwa majina marafiki zake hao wanaomchangia.
Alitoa mifano ya harambee zilizoendeshwa na Lowassa kwa ajili ya
kuchangia ujenzi wa makanisa katika mikoa ya Morogoro na Shinyanga, na
hii ya hivi karibuni aliyochangia ujenzi wa kituo cha Radio Ikra,
kinachomilikiwa na Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), na harambee
yake kufanyika jijini Mwanza.
“Miongoni mwa marafiki zake waliomchangia katika harambee ya kuchangia
kanisa mjini Morogoro ni Philemon Molel. Huyu alimwinua pale pale na
kumshawishi achangie, na akachanga pesa nzuri,” alisema Chami na
kuongeza:
“Kule Shinyanga, wakati wa harambee ya Kanisa la KKKT, alimtaja
hadharani rafiki yake Mathias Manga. Huyu ni mfanyabiashara mkubwa wa
madini jijini Arusha, lakini pia anamiliki hoteli moja kubwa ya kitalii
jijini Mwanza, inayoitwa Gold Crescent, na hata kwenye harambee ya juzi
jijini Mwanza kuchangia Kituo cha Radio Ikra, rafiki yake huyu huyu
alimtaja pia hadharani, na mbali na kutoa ukumbi wa hoteli yake utumike
kuendeshea harambee ile, alichangia pia shilingi milioni 10.
“Hiyo ni mifano michache tu, lakini wako wengi, na naamini hata
nikiwataja wote hapa, kesho hawatakanusha kama ambavyo marafiki zake
aliowataja (Sitta) kule kwenye harambee yake jijini Mwanza
walivyokanusha. Kila Mtanzania anakumbuka, Sitta alimtaja Magufuli
(John) kuwa ni rafiki yake na alikuwa amemchangia shilingi milioni tano,
lakini kesho yake akakana.”
Kuhusu ni nini wanatarajia kupata kutoka kwa Lowassa marafiki zake hao
wanaomchangia. Chami alijibu: “Hawatarajii kupata chochote kutoka kwa
mheshimiwa zaidi ya mapenzi waliyonayo kwake. Siku zote amekuwa
akisisiza kuwa hana utajiri ila utajiri wake ni watu, watu wanapenda
kuchangia harambee zake kwa sababu ya ushawishi wake tu, basi.
No comments:
Post a Comment