Islamic Banking - NBC yawatoa hofu wananchi kuhusu akaunti ya Kiislamu
Baadhi ya wateja wa Benki ya NBC, wakifuturu katika hafla ya futari
iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wateja wake jijini Dar es Salaam,
mwishoni mwa wiki.
Dar es Salaam. Serikali imewatoa hofu Watanzania ikiwataka kutosita
kujiunga na kutumia huduma za kifedha zinazofuata kanuni za Kiislamu kwa
kuwa huduma hiyo ni mkombozi kwa wananchi wengi.
Akizungumza wakati wa hafla ya futari kwa wateja iliyoandaliwa na Benki
ya Taifa ya Biashara (NBC) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Naibu
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema bidhaa hiyo imeletwa katika
muda mwafaka.
Huduma hii hufuata sheria na kanuni za Kiislamu. Ni huduma inayojali na
kufuata maadili na ni furaha kwa Serikali kuona kwamba hatimaye maadili
sasa yanaingia hadi kwenye huduma za kifedha.
Maadili yakiwa imara katika jamii, tunatarajia pia kupata uchumi
imarawenye kukua na viwanda vyenye kuzalisha bidhaa na huduma zenye
kukidhi mahitaji ya wote, alisema.
Saada aliiomba NBC kuendelea kubuni na kuwaletea Watanzania huduma
nyingine zenye kukidhi mahitaji mbalimbali ya wateja, wakubwa kwa
wadogo, hususan mikopo kupitia Huduma ya Kibenki ya Kiislamu.
Aliitaka pia benki hiyo kutoa elimu kwa Watanzania ili waweze kufahamu
kwa undani faida ya huduma hiyo ambayo iko wazi kwa yeyote bila kujali
itikadi au imani yake ya kidini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Mizinga
Melu alimuahidi Naibu Waziri kwamba benki hiyo haitaacha mipango yake ya
kuisaidia Serikali kutekeleza kauli mbiu yake ya maisha bora kwa kila
Mtanzania .
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma ya Kibenki ya Kiislamu, Yassir Masoud
alisema kuwa muda si mrefu NBC itaanzisha huduma za mikopo kupitia
bidhaa hiyo, akisisitiza kwamba wanaelewa kuwa watu wengi wanaisubiri
kwa hamu kubwa.
Huduma ya Islamic Banking ya Benkiya NBC ilizinduliwa Mei 2010
source:MCL
No comments:
Post a Comment