- AHOFIA NCHI KUONGOZWA NA WAUZA DAWA ZA KULEVYA
- ASEMA HAKUNA TAJIRI ANAYETOA FEDHA BILA MASHARTI
WAZIRI Mkuu Mstaafu wa
Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, amewataka Watanzania kutambua
kwamba hakuna mtu tajiri anayetoa fedha na mali
zake bila masharti; na kuwa iwapo Watanzania watawaweka madarakani viongozi kwa
rushwa, wasitegemee Katiba Mpya itajibu matatizo yao ndani ya jamii.
"Tukumbuke kuwa
anayekuhonga ili umpigie kura akishaingia madarakani mkataba wake na wewe
uliishia pale ulipomuuzia kura yako na yeye kazi atakayofanya akipata hiyo
ofisi au madaraka ni kusaka rushwa na kufisadi mali za umma ili arudishe fedha
zake alizotumia kukununua wewe na wenzako," alisema Sumaye.
Sumaye alitoa kauli hiyo mjini Morogoro jana wakati
akifungua maadhimisho ya 20 ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania
(MVIWATA).
Alisisitiza kuwa; "Kama
huamini wewe nenda ukamwombe fedha iwapo hana kura anayokuomba halafu usikie
jibu atakalokupa."Alisisitiza kuwa kiongozi wa
aina hiyo ataongeza nyingine (fedha) nyingi zaidi za kukununua tena safari
ijayo. "Mtu wa aina hiyo kipaumbele chake si jamii na umma,
bali ubinafsi wake na wale marafiki zake waliomfadhili wakampa zile
fedha,"alisema Sumaye.
Sumaye alisema
hata katiba iwe nzuri namna gani na ikatamka kuwa rushwa ni adui wa haki na
hata ikatoa adhabu kali sana kwa kosa hilo, kama tutaweka viongozi madarakani
kwa rushwa, hiyo katiba wala haitasaidia.Kiongozi huyo
mstaafu alisema ni lazima katiba nzuri mpya iambatane na serikali safi yenye kusimamia
masilahi ya umma.
"Huwezi
kumweka madarakani mwenyekiti wa kijiji au diwani au mbunge au hata rais kwa
rushwa ya kuwanunua wapigakura halafu utegemee katiba mpya itajibu matatizo ya
jamii," alisisitiza Sumaye.Alisema yeye
ukimuuliza kuhusu katiba tuliyonayo sasa atasema ni ni nzuri tu na tungeweza
kufanya marekebisho katika maeneo machache kama
pana haja ya kufanya hivyo.
"Tatizo
letu liko katika kutekeleza na kusimamia sheria zetu tulizozitunga kutokana na
maelekezo ya jumla ya katiba yetu. Baada ya katiba Bunge hutunga sheria mbali
mbali kukidhi matakwa fulani fulani katika jamii," alisema na kuongeza;
"Kwa hiyo
pamoja na kutengeneza katiba mpya, jambo muhimu sana ni kuwa na serikali itakayosimamia na
kutekeleza sheria zetu ili kulinda yale yaliyoelekezwa katika katiba."
Alisema kuwa
katiba itatamka haki ya mtu kuwa na mali
na itatamka wajibu wa serikali kulinda mali ya mtu. Alisema katiba haiwezi
kumzuia mwizi kwenda kuiba na sheria haitamzuia mwizi kwenda kuiba ila itatamka
adhabu ya kupewa huyo mwizi.
Alisema kuwa ili vyote hivyo
viwe na maana ni lazima awepo mtu au chombo cha kumkamata mwizi na kumfikisha
katika mikono ya sheria na chombo hicho ni serikali.Alisema kama serikali haiwezi kufanya hiyo kazi kwa
ukamilifu, tutaishia kulalamika tu maonevu na maumivu yataendelea kuumiza
jamii.
Alisema Katiba
Mpya bila kuwa na watu madhubuti, watu waadilifu, wanaochukia rushwa na ufisadi
kwa dhati kuongoza nchi yetu haitakuwa na msaada wowote katika kuboresha maisha
ya Watanzania."Nataka
nieleweke vizuri kuwa mimi sizungumzii serikali yangu iliyoko madarakani, bali
nazungumzia Katiba Mpya na serikali itakayozaliwa baada ya hapo, alisema Sumaye
na kuongeza;
"Nazungumzia
uchaguzi ulioko mbele yetu mwakani na mwaka 2015, simzunguzii mtu yeyote bali
naizungumzia tabia mbaya. Najua hata hapa wapo watu wametumwa nendeni
mkamsikilize huyo Sumaye leo (jana) atasema nini.Hakuna haja ya kutafiti nitakachosema
maana kinaeleweka. Nimesema mimi sitanyamaza kupambana na rushwa na ufisadi na
maovu mengine hata siku moja. Wala sitaacha kukemea tabia hizi mbaya
zinazoangamiza jamii yetu na taifa letu."
Sumaye alisisitiza; "Kama wewe ni mhusika una tabia zinazofanana na hizo dawa
ni kuziacha au uvumilie tu haya maneno yaendelee kukuchoma moyoni."Aliwataka Watanzania wote kupitia
wakati huu wa kutengeneza Katiba Mpya waanze kutengeneza v i c hwa n i mwa o s
e r i k a l i itakayosimamia utekelezaji wa katiba hiyo kwa masilahi ya umma,
yenye uwezo na yenye uadilifu usiotiliwa shaka.
Alisema, kazi ya kukemea uovu na hasa
uovu wa rushwa za uchaguzi lazima ifanywe na kila Mtanzania mwadilifu ili waovu
hao wasipate uongozi wa kununua maana wataifanya kazi ya kutunga Katiba Mpya
ambayo ni kazi ya gharama kubwa iwe imepotea bure.
Dawa za kulevya
Akizungumzia dawa za kulevya, Sumaye
alisema tatizo hilo
kwa sasa ni kubwa ndani na nje ya nchi na vijana wengi wameathirika.Alisema biashara hiyo ni haramu
inayohusisha fedha nyingi na mitandao mipana. Alibainisha kwamba katika baadhi
ya nchi duniani, biashara hiyo hukithiri mpaka wahusika huweza kujenga majeshi
ya kupambana na majeshi ya serikali ana kwa ana.
"Nchini mwetu hatujafikia hatua
hiyo, lakini ikiachiwa ikaendelea yaweza kufika huko. Biashara hii huharibu sana vijana wetu na
kugeuka zezeta au wakawa wahalifu wa kutisha," alisema Sumaye na kuongeza; "Kama mtu anaweza kuhonga sehemu
kubwa ya wapigakura katika jimbo la uchaguzi au hata katika nchi kama nafasi anayosaka ni urais, tumeshajiuliza hizo fedha
nyingi hivyo anapata wapi?
Kama anajihusisha na
biashara hizo chafu akipata nafasi hiyo watoto wetu watapona? Haya ni maswali
muhimu ya kujiuliza tunapoelekea mwaka kesho kwenye uchaguzi wa serikali za
mitaa na mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu
CHANZO:MAJIRA
No comments:
Post a Comment