JESHI
la Polisi mkoani Katavi limemtia nguvuni Masaga Charles (36) akidaiwa
kuwa muuaji wa kukodiwa. Charles ambaye pia alikuwa bingwa wa mashindano
ya mbio za baiskeli yaliyofanyika Arusha mwaka jana, anatuhumiwa
kufanya mauaji ya ukatili wilayani Mpanda.
Inaelezwa kuwa kwa zaidi ya miaka 15, Charles amekuwa akishiriki katika
mashindano ya mbio za baiskeli katika mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza
na Arusha Oktoba mwaka jana ambako aliibuka mshindi na kujinyakulia Sh
800,000.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi , Dhahiri Kidavashari,
mtuhumiwa huyo ni mkazi wa Kijiji cha Chilalo Wilaya ya Misungwi mkoani
Mwanza.
Charles anatuhumiwa kumuua Moshi Bella (44) wa Kijiji cha Karema kwa
kumkatakata na panga kichwani na shingoni baada ya kuahidiwa kulipwa Sh
milioni tano.
Kamanda Kidavashari alisema tukio hilo la mauaji ya kinyama lilitokea
Julai 21 mwaka huu katika Kijiji cha Kabange Kata ya Simbwesa Tarafa ya
Kabungu mkoani Katavi.
Alisema mtuhumiwa kabla ya kufanya mauaji hayo alionana na Bella akijifanya alikuwa anataka auziwe shamba.
Mazungumzo hayo yalifanyika Julai 20 mwaka huu nyumbani kwa Salumu
Kajimba ambaye ni ndugu wa marehemu Bella, alisema Kamanda Kidavashari.
Kamanda alisema mtuhumiwa na Bella walikubaliana kuuziana ekari mbili za shamba ambalo ni mbuga ya mpunga.
“Walikubaliana kuuziana Sh 300,000 kwa kila ekari na baada ya
makubaliano hayo mtuhumiwa alimuahidi Bella kwamba angerejea siku ya
pili kwa ajili ya kutoa malipo hayo,” alisema Kamanda.
Alisema siku iliyofuata mtuhumiwa Charles alifika nyumbani kwa Salumu
Kajimba ambaye ni ndugu wa Bella ya saa 9.00 alasiri lakini bahati mbaya
Bella alikuwa amekwenda kisimani kuoga.
Mtuhumiwa baada ya kuambiwa Bella alikuwa amekwenda kisimani alimuaga Kajimba na mkewe akisema alikuwa anamfuata Bella.
Kamanda Kidavashari alisema Bella hakuonekana nyumbani tangu alivyowaaga
kuwa anakwenda kuoga kisimani wala Bella aliyemfuata naye hakurejea
hadi hapo mwili wa Bella ulipookotwa mbugani.
Mwili wa Bella ulikutwa umekatwakatwa na panga shingoni kwa nyuma na kichwani.
Kamanda alisema baada ya polisi kuarifiwa na raia wema kuhusu mauaji
hayo waliweza kumkamata mtuhumiwa Masaga Charles katika mtaa wa
Makanyagio mjini Mpanda.
Baada ya kukamatwa mtuhumiwa alikiri kuhusika na mauaji hayo akidai
alitumwa na mkazi mmoja wa Kijiji cha Iroba Tarafa ya Kabungu wilayani
Mpanda aliyemuahidi kumlipa Sh milioni tano.
Kamanda
alisema mtuhumiwa alidai kuwa mtu aliyemtuma amekwisha kukimbilia
mkoani Shinyanga ili asijulikane kuwa ndiye aliyehusika na mpango wa
mauaji hayo.
Mtuhumiwa alidai kuwa kwa mara ya kwanza aliambiwa kufanya mauaji hayo
Oktoba mwaka jana kwa malipo ya Sh milioni mbili lakini alikataa,
alisema. Kamanda alisema mtuhimiwa alidai kuwa Aprili mwaka huu
aliambiwa tena afanye mauaji kwa malipo hayo lakini akaendelea kukataa
hadi alipoongezewa dau na kufika Sh milioni tano na kupewa shamba la
ekari mbili.
Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma za mauaji zinazomkabili, alisema kamanda.
source: Gazeti la mtanzania
No comments:
Post a Comment