Sitta ahoji harambee za Lowassa Makanisani na sasa misiktini
 
WAZIRI  wa  Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amehoji 
walipo na  majina ya  wanaoitwa “Marafiki wa Lowassa” wanaomchangia 
mamilioni ya  fedha za kusaidia  harambee mbalimbali nchini.
 Akizungumza na Raia Mwema wiki hii, Sitta alisema ni  ajabu 
kwamba ‘marafiki’ hao  wamekuwa wakitajwa tu bila ya kufahamika  ni 
akina nani, wana ukwasi kiasi gani  na wameupataje ukwasi huo.
 
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward  Lowassa, amekuwa akichanga michango  
ya fedha katika harambee mbalimbali nchini  huku akisema fedha  
anazochanga si zake binafsi bali ni michango pia ya rafiki  zake.
 
Na  akizungumza kupitia kwa msaidizi wake jana Jumanne, Lowassa  alisema
 hoja kwamba marafiki zake wanaomchangia hawafahamiki haina  ukweli 
wowote kwa kuwa amekuwa  akiwataja hadharani kwa majina kila  
wanapomchangia.
 
Lakini Waziri Sitta alihoji, alisema ya  kuwa, haiingii akilini watu 
kumchangia mwanasiasa huyo bila ya kuwa na sababu za msingi za kufanya  
hivyo.
 
“Nyie waandishi mnatakiwa mlisaidie  taifa kwenye hili. Mtu anapita  
nchi nzima anachanga mamilioni ya fedha na  anasema si zake bali ni za  
rafiki zake. Lakini hatuambii rafiki zake hao ni  akina nani. Hatujui  
kama hata rafiki zake hao wanachangia kodi kwa serikali.
 
“Lakini, swali kubwa la kujiuliza zaidi  hapa ni hili; inakuaje  
michango ya kwenye taasisi za kidini mtu ampe Lowassa na  asiende  
mwenyewe kutoa kanisani au msikitini kwake?
 
“Ninachojua mimi, mbinguni hakuna c/o (kupitia kwa). Ina  maana 
Wasamaria  hawa wanajua kwamba ili uende mbinguni ni lazima  mchango 
wako utolewe na huyo  bwana (Lowassa)?” alihoji Sitta.
 
Katika mahojiano hayo, Sitta ambaye  alikuwa Spika wa Bunge la Tisa  
wakati wa kashfa ya Richmond iliyomwandama  Lowassa, alisema kizazi cha 
 Watanzania wa sasa kina shida kubwa kwenye kupata  viongozi walio  
waadilifu.
 
Alisema uongozi sasa umekuwa fursa ya  kuchuma mali badala ya  kutumikia
 umma, na kwamba hata katika matukio ya  kuongeza heshima kwa  taifa, 
watu wanayatumia kutia aibu taifa.
 
Sitta aliyasema hayo akigusia vitendo  vya ufisadi vilivyofanyika wakati wa mkutano wa Smart Partnership uliofanyika nchini mapema mwezi huu ambapo ripoti  za vitendo vya ufisadi zimeanza kuibuka.
 
“Mkutano ule ulitakiwa ujenge heshima  yetu. Lakini majizi yameingia  na
 sasa taifa limeingia katika kashfa nzito. Kila  kitu sasa ni ufisadi  
tu. Tukiendelea hivi hivi hatutafika kokote,” alisema  mwanasiasa huyo.
 
Kauli hiyo ya Sitta imekuja huku Lowassa  akizidi kuchanja mbuga katika 
kuendesha harambee ndani ya makanisa na misikiti, na mara kwa mara 
harambee anazoendesha na kufanikisha ni zaidi ya shilingi milioni 200.
 
Kwa mfano, hivi karibuni akiwa jijini  Mwanza Lowassa alifanya  harambee
 ya Sh. milioni 590, ikiwamo michango yake na  watu anaowaita  “rafiki 
zake”, lakini pia amewahi kufanya harambee mkoani  Ruvuma,  wilayani 
Nyasa, ambako zilikusanyaswa Sh. milioni 300.
 
Lowassa pia amewahi kufanya harambee kwa  ajili ya ujenzi wa Kanisa  
Katoliki Nyakato Mwanza ambako alichangisha Sh.  milioni 200, amewahi 
kuchangisha Sh. bilioni moja kwa ajili ya Chama cha Kuweka  na Kukopa 
(Saccos) cha Walimu wa Moshi Vijijini. Amewahi pia kuendesha harambee na
 kukusanya Sh milioni 134 Babati, mkoani Manyara.
 
Ingawa Lowassa binafsi amewahi  kunukuliwa akisema si tajiri wa fedha  
isipokuwa ni tajiri wa watu, anatajwa kumiliki biashara kadhaa kubwa 
pamoja na mali nyingi kama majumba katika maeneo  mbalimbali nchini. 
 Alipotafutwa Lowassa, ili pamoja na  mambo mengine, aweze kutoa 
ufafanuzi juu ya baadhi ya hoja hizo zilizoibuliwa  na Sitta dhidi yake,
 mwanasiasa huyo alimwelekeza mwandishi wetu kuzungumza na Katibu wake, 
 aliyejitambulisha kwa jina la Boniface Chami.
 
Akijibu  ni kwa nini Lowassa hawataji hadharani marafiki zake hao  
wanaodai wanamchangia  mamilioni ya shilingi anayoyatoa kwenye harambee 
zake, Chami, alisema hoja hiyo  haina ukweli wowote kwa kuwa Lowassa  
amekuwa akiwataja hadharani kwa majina  marafiki zake hao wanaomchangia.
 
Alitoa  mifano ya harambee zilizoendeshwa na Lowassa kwa ajili ya  
kuchangia ujenzi wa makanisa katika mikoa ya Morogoro na Shinyanga, na 
hii ya hivi karibuni aliyochangia ujenzi wa kituo cha Radio Ikra,  
kinachomilikiwa na Baraza la  Waislamu Tanzania (BAKWATA), na harambee  
yake kufanyika jijini Mwanza.
 
“Miongoni  mwa marafiki zake waliomchangia katika harambee ya  kuchangia
 kanisa mjini Morogoro ni Philemon Molel. Huyu alimwinua pale  pale na 
kumshawishi achangie,  na akachanga pesa nzuri,” alisema Chami  na 
kuongeza:
 
“Kule  Shinyanga, wakati wa harambee ya Kanisa la KKKT, alimtaja 
hadharani rafiki yake  Mathias Manga. Huyu ni mfanyabiashara mkubwa wa 
madini jijini Arusha, lakini  pia anamiliki hoteli moja kubwa ya kitalii
 jijini Mwanza, inayoitwa Gold Crescent, na hata kwenye harambee ya juzi
 jijini Mwanza kuchangia Kituo cha Radio Ikra, rafiki yake huyu  huyu 
alimtaja pia hadharani, na mbali na kutoa ukumbi wa  hoteli yake utumike
 kuendeshea harambee ile, alichangia pia shilingi milioni 10.
 
“Hiyo ni mifano michache tu, lakini wako wengi, na naamini hata 
nikiwataja wote hapa,  kesho hawatakanusha kama ambavyo marafiki zake 
aliowataja (Sitta) kule kwenye harambee yake jijini Mwanza 
walivyokanusha. Kila Mtanzania anakumbuka, Sitta alimtaja Magufuli  
(John) kuwa ni rafiki yake na alikuwa amemchangia shilingi milioni tano,
 lakini kesho yake akakana.”
 
Kuhusu ni nini wanatarajia kupata kutoka kwa Lowassa marafiki zake  hao 
wanaomchangia.  Chami alijibu: “Hawatarajii kupata chochote kutoka  kwa 
mheshimiwa zaidi ya  mapenzi waliyonayo kwake. Siku zote amekuwa  
akisisiza kuwa hana utajiri ila  utajiri wake ni watu, watu wanapenda  
kuchangia harambee zake kwa sababu ya ushawishi  wake tu, basi.
 
 
 
          
      
 
  
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment