
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameagiza Wizara za Serikali zinahusika 
na kodi na mawasiliano pamoja na makampuni ya simu za mikononi nchini 
kukutana mara moja kutafuta jinsi gani ya kumaliza mvutano wa kodi mpya 
ya kadi za simu hizo za mikononi.
Rais
 kikwete ametoa maelekezo hayo jioni ya leo, Jumanne, Julai 23, 2013 
wakati alipokutana na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya 
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa makampuni ya simu 
ya TTCL, Airtel, Vodacom, Tigo na Zantel katika kikao cha pamoja 
kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Rais
 Kikwete amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo wa pamoja kati ya Wizara 
hizo za Serikali na makampuni ya simu yawe ya kupendekeza jinsi gani ya 
kuziba pengo la Sh. Bilioni 178 ambazo zitapotea katika Bajeti iwapo 
kodi hiyo kwa kadi za kuongelea za simu za mikononi italazimika kufutwa 
na Serikali kupitia marekebisho kwenye Muswada wa Fedha wa Bajeti ya 
Mwaka 2013/2014.
Rais
 Kikwete amewaambia wawakilishi wa pande hizo mbili kuwa huwezi tena 
kuifuta moja kwa moja kodi hiyo bila kutafuta njia nyingine za kupata 
fedha za kujaza pengo hilo la Sh. Bilioni 178 ambazo tayari Bunge 
limezipangia matumizi.
“Nawaombeni
 kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja 
tutafute namna gani tunaweza kujaza pengo hili la Sh. Bilioni 178 endapo
 tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito na kuwa 
pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu,”Rais Kikwete amewaambia wawakilisho hao.
Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014, Serikali imeweka kodi ya Sh. 1,000/= kwa mwezi kwa kila mtumiaji simu kwa ajili ya kufanya mawasiliano kwa kutumia simu ya mkononi
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
23 Julai, 2013
 
No comments:
Post a Comment