Kufuatia kauli za Serikali magazetini kuhusu mimi na kodi ya umiliki wa kadi za simu; nijibu tu kwa ujumla kwamba SITAACHA. Badala yake naomba kuwapatia namba zao: Makamba 0767783996 na Mgimwa 0754/0684765644, tunachohitaji ni kauli ya Serikali kuwa kodi imesitishwa na itaondolewa na sio siasa chafu.
Kwa
 mliotaka  msimamo wangu juu ya kauli ilinukuliwa  jana tarehe 18 Julai 
2013 na Gazeti la Majira kwamba  Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
 Teknolojia Januari Makamba kwamba; “Mnyika anaangalia upepo unakoelekea, akiona watu wanalalamika ndipo anaongea namsihi aache kufanya siasa katika jambo hili”, naomba kutumia mtandao huu kutoa majibu ya ujumla kwa maswali na masuala yote kama ifuatavyo:
Nieleze kwamba sitaacha kufanya siasa kwenye jambo hili mpaka kodi hiyo 
itakapofutwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kubaki na fedha 
walau kidogo kwa maendeleo. 
Sitaacha kufanya siasa kwa sababu ndio kazi yangu ambayo wananchi 
walinichagua kuifanya ya kuwawakilisha na kuisimamia Serikali ambayo 
yeye Makamba ni sehemu yake. Sitaacha kufanya siasa kwa sababu Mwalimu 
Nyerere alisema ili nchi yetu iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi
 na uongozi bora.
Ambacho sitafanya ni siasa chafu kama hizo ambazo Makamba amefanya za 
kusema uongo, kwa kuwa naamini anafahamu kabisa kwamba sijaanza kuongea 
kuhusu suala hili baada ya malalamiko ya wananchi bali jambo hili 
nilianza kulishughulikia bungeni mara baada ya Waziri wa Fedha 
kuwasilisha jedwali la marekebisho la kuanzisha kodi lukuki za simu 
ikiwemo hii. Katika mchango wangu bungeni, nieleza kwamba muswada huo wa
 sheria ya fedha kwa kupandisha kodi kwenye mafuta na simu ni ‘muswada 
wa majanga ya kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi. 
Aidha, sikuishia kusema tu kwa niaba ya wananchi bali nilichukua hatua 
kwa mujibu wa kanuni za Bunge nami kuwasilisha jedwali la marekebisho ya
 kupinga kodi ya umiliki wa kadi za simu pamoja na kodi nyingine zote 
zenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi sio kwenye sekta 
ya mawasiliano bali pia kwenye sekta zingine ikiwemo sekta ndogo (sub 
sector) nyeti ya mafuta. 
Mlioniuliza kwa SMS katika simu na kwenye mitandao ya kijamii sasa ni wakati wa Makamba kuhojiwa kwa njia hizo hizo (Simu yake ya Mkononi ni 0767783996)
 kwa kuwa yeye ni sehemu ya Serikali na Serikali ndiyo ambayo iliingiza 
suala hili kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge kupitia hotuba ya
 Bajeti Serikali na ikalirudia kuliingiza kupitia jedwali la marekebisho
 ya Sheria ya Serikali; ni wakina nani hasa kwa majina ndani ya Serikali
 na Bunge walioingiza kodi hii? Na ni wakina nani hasa waliopigia kura 
ya ndio kuipitisha? 
Aidha, amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la leo tarehe 19 Julai 2013 
akieleza kwamba hakubaliani na suala hili na kupita kwake ilikuwa na 
kuzidiwa nguvu. Hivyo, ataje kwa majina hayo waliozidi nguvu serikali 
kinyume na matakwa yake. Amenukuliwa akisema pia kwamba anajua kuwa 
suala hili haliwezi kutekelezwa na kwamba ni lazima litabadilishwa kwa 
kuangalia eneo lingine la kutoza kodi. Ni vizuri akahojiwa, ikiwa huo ni
 msimamo wa Serikali; mwenye mamlaka ya kusitisha kodi hiyo ni nani na 
kwanini hajitokezi kutoa agizo la kusitisha wakati maandalizi 
yakiendelea ya kupeleka muswada bungeni wa kuifuta kabisa kodi hiyo 
katika mkutano ujao? 
Wakati Naibu Waziri akisema hayo, Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa  
katika Serikali hiyo hiyo yeye ametoa kauli tofauti siku hii hii ya leo 
ambapo kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania amewataka watumiaji wa mitandao
 ya simu nchini na watanzania kwa ujumla kuwa na subira kuhusu tozo ya 
sh 1000 kwa mwezi kwa kila laini ya simu za kiganjani.
Na kwa kuwa amesema kwamba Serikali inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau, natoa mwito kwa wananchi kumtumia maoni kupitia namba zake za simu za mkononi  0754/0684-765644.
 Aidha, ni vizuri aeleze subira hiyo ivutwe mpaka lini? Na ni wakina 
nani hasa kwa majina waliomfanya akaingiza kodi hiyo katika kitabu cha 
Hotuba yake aliyosoma bungeni kuhusu bajeti ya Serikali na wakina na 
hasa kwa majina waliomfanya arejeshe kodi hiyo ya kadi za simu kwenye 
jedwali la marekebisho ya muswada wa sheria ya fedha alilowasilisha 
bungeni.
Nasisiza kuwa kauli za ujumla za Serikali bila kuwataja kwa majina 
wahusika ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko ya wananchi 
kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa wabunge. Ni 
muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Rais ama 
kiongozi mwingine mwenye mamlaka ajitokeze kusitisha kutozwa kwa kodi 
hiyo na kuanzisha mchakato wa muswada wa kufuta kodi hiyo kuwasilishwa 
katika mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 27 Agosti 2013. 
Majina ya wahusika yasipotajwa au mamlaka zinazohusika zisipotoa 
kauli katika mkutano wa hadhara nitakaoshiriki  jumapili tarehe 21 Julai
 2013 katika Uwanja wa Sahara kata ya Mabibo kuanzia saa 8 Mchana mpaka 
saa 11 Jioni nitatoa mrejesho kuhusu yaliyojiri katika mkutano uliopita 
wa Bunge na kueleza hatua zaidi zinazopaswa kuchukuliwa kuwezesha majina
 ya wabunge hao kutajwa hadharani na hatua za kuondoa kodi hiyo 
kuchukuliwa. 
Uongozi bora na uraia mwema wenye uwajibikaji ni chimbuko na chachu ya 
ukuaji endelevu wa uchumi wa nchi na ustawi wa maisha ya wananchi. 
Twende kazi.
John Mnyika (Mb)
19 Julai 2013

 
No comments:
Post a Comment