pAPA AWATAKA WAKRISTO KUTOPENDA MALI NA MADARAKA
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, amewataka 
Wakristu Wakatoliki kuachana na kile alichokiita kupenda mali na 
madaraka. 
Wito huo ameutoa wakati akiadhimisha Ibada ya Misa katika Pango Takatifu
 huko Aparecida, kwenye jimbo la Sao Paulo nchini Brazil.
Akihubiri wakati wa Ibada ya Misa yake ya kwanza kuadhimisha tangu 
awasili Brazil, katika Kanisa Kuu la madhabahu ya Mama Bikira Maria wa 
Aparecida, Baba Mtakatifu Francis, amewasihi Wakatoliki na hasa vijana 
wajiepushe kufata njia zinazopotosha na hatimaye kuwaweka njia panda.
Amesema siku hizi watu wamekuwa wakivutiwa zaidi na starehe, mafanikio, 
utajiri na madaraka na hivyo kuwasihi wazingatie suala zima la imani na 
ukarimu, ili kurejesha matumaini yanayoanza kupotea miongoni mwa jamii.
Mahujaji vijana wanaohudhuria kongamano lao Brazil
 
Amesema amemuomba Mama Maria aliyempenda na kumtunza Yesu awasaidie watu
 wote wakiwemo viongozi wa Kanisa, wazazi na walimu, ili waweze 
kufikisha ujumbe wa maadili mema kwa vijana, ambao utawasaidia kulijenga
 taifa na dunia itakayozingatia haki, usawa, umoja na udugu.
Maelfu wabarikiwa
Baada ya Ibada ya Misa, Baba Mtakatifu alisali tena kwenye Pango la Mama
 Maria wa Aparecida na kisha akawabariki maelfu ya waumini waliokuwa nje
 ya Kanisa Kuu na kutangaza kwamba atarejea tena Aparecida mwaka 2017, 
wakati wa kuadhimisha miaka 300 ya mvuvi aliyeiokota picha nyeusi ya 
Mama Maria, karibu na mto.
Kisha Papa huyo, alirejea mjini Rio de Janeiro, ambapo alifungua 
hospitali ya Mtakatifu Francis wa Asizi kwa ajili ya wagonjwa wa akili 
na hasa waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya, iliyopo mjini Rio de 
Janeiro.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amesema kuwa tatizo la biashara
 na matumizi ya dawa za kulevya ni janga kubwa katika eneo la Amerika ya
 Kusini. Amesema jukumu kubwa lililoko sasa ni kuwaelimisha vijana maana
 na tunu za maisha ya pamoja, pamoja na kuendelea kuwasaidia 
walioathirika na dawa hizo.
Shughuli za Papa siku ya leo (25.07.2013)
Leo, Baba Mtakatifu ambaye yuko nchini Brazil kwa ziara ya wiki nzima, 
ataianza siku yake kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye makaazi
 yake ya muda huko Sumare, Rio de Janeiro na kisha atapewa ufunguo wa 
mji huo pamoja na kubariki bendera za Olimpiki.
 
Aidha, Papa atatembelea eneo la mitaa ya mabanda na baadae jioni 
atawakaribisha zaidi ya vijana milioni moja kutoka sehemu mbalimbali 
duniani katika ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Vijana wa Kikatoliki 
Duniani kwa mwaka wa 2013. Shughuli hiyo itafanyika katika ufukwe wa 
Copacabana, huko Rio de Janeiro.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu ametoa pole kwa familia za watu 
waliopoteza maisha katika ajali ya treni iliyotokea nchini Uhispania 
jana. Abiria wengi katika treni hiyo, walikuwa mahujaji wanaoelekea 
Santiago de Compostela, kuhudhuria sherehe za mtakatifu msimamizi wa mji
 huo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,DPAE
Mhariri: Josephat Charo
 
source:dw.de
 
 
 
          
      
 
  
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment