UGOMVI
 wa kisiasa kati ya ndugu wawili wa familia moja, Naibu Waziri wa 
Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba(ccm) na kaka yake Adrian Tizeba(Chadema) 
umechukua sura mpya baada ya kutishiana kifo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Adrian alisema kuwa tangu ahame CCM na 
kujiunga na CHADEMA, mdogo wake huyo amekuwa akimbambikizia maneno 
mabaya yaliyoleta uhusiano mbaya katika familia yao.
Alidai kuwa naibu waziri huyo aliwahi kumwambia mama yao mzazi aseme kwamba Adrian aliwahi kumbaka.
Alisema kuwa hayo yote yanasemwa ili afunguliwe mashtaka na kufungwa.
Adrian aliongeza kuwa baada ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika ya kata
 ya Lugata ambapo naibu waziri huyo alimtumia mama yake kuendesha 
propaganda chafu dhidi yake, sasa amebambikiziwa tuhuma mpya.
Alisema baada ya uchaguzi huo alibakia katika kata hiyo iliyo kisiwani 
kwa lengo la kuendelea na kazi za kisiasa, lakini naibu waziri 
amembambikizia kesi kuwa anazuia mgambo kufanyika katika eneo hilo.
Hali hiyo imesababisha polisi na wanajeshi kumsaka kwa nguvu ikiwemo kumtengenezea shtaka la wizi wa kutumia silaha.
Alifafanua kuwa siku za karibuni kwenye kata hiyo kumekuwa na kitendo cha kulazimisha vijana kushiriki mgambo bila hiari yao.
Alisema kuwa katika kutengeneza sababu ya kuwabana, polisi walitumia 
vurugu za tukio la kijana Emanuel Joseph kunyang’anywa baiskeli yake na 
wakufunzi wa mgambo wakidai kuwa vijana walimpiga mkufunzi na kuchaniwa 
sare za jeshi.
Alipotafutwa Naibu Waziri Tizeba kujibu tuhuma hizo za kutishia kumuua 
kaka yake alisema hayo ni masuala ya familia ambayo hayana nafasi ya 
kuandikwa katika vyombo vya habari.
“Ninashangaa kila kunapotokea kutoelewana kati yetu huyu kaka yangu 
anakimbilia kwenye vyombo vya habari wala sio kwenye familia wakati bado
 tunaye mama yetu mzazi ambaye anaujua vema mgogoro wetu.
“Mimi naona anafanya hayo akidhani kuwa angeweza kuniua mimi kisiasa lakini suala hilo halitawezekana,” alisema Tizeba.
Source: Tz Daima.
 
No comments:
Post a Comment