SHILOLE MATATANI WIZI SIMU ZA DIAMOND 
 
Stori:Shakoor Jongo na Musa Mateja
STAA
 wa filamu na muziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ ameingia 
matatani akidaiwa kuingia mitini na simu tatu za mkononi alizoaminiwa 
nchini Afrika ya Kusini alikokwenda kufanya shoo.
Msanii huyo 
alikumbwa na kasheshe hilo Julai 19, 2013 nyumbani kwa mwanamuziki wa 
Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Sinza Mori, Dar.
Siku hiyo 
Diamond alikuwa akifuturisha na aliwaalika watu mbalimbali wakiwemo 
mastaa lakini nusura futuru iingie doa kufuatia zogo hilo.
ISHU ILIKUWAJE?
Ndugu
 wa Diamond aitwaye Majaliwa Majuto ‘Q Boy’ alidai ndiye mwenye simu 
hizo. Alisema miezi kadhaa iliyopita, Shilole alikwenda nchini humo 
kufanya shoo ya muziki. Wakati wa kuondoka alimpa simu tatu, Ipad, 
Samsung Galaxy na Blackberry ili akifika Bongo ampe Diamond lakini 
msanii huyo hakufanya hivyo.
“Alikuja Sauzi kufanya shoo, wakati 
wa kuondoka nilimpa simu tatu amletee Diamond lakini nashangaa hakufanya
 hivyo na mimi tangu nirudi Bongo simpati, kila nikimpigia simu hapokei,
 leo ndiyo tumekutana hapa kwa Diamond,” alilalama Q Boy.
DIAMOND ALIAMBIWA SIMU ANAZO SHILOLE
Alisema
 awali akiwa nchini humo baada ya kumkabidhi mali hizo, alimpigia simu 
Diamond na kumtaarifu kuwa ‘mzigo’ anao Shilole, akashangaa staa huyo 
kujibu kwamba hajazipata wala hajamwona Shilole.
SHILOLE AJITETEA
Katikati
 ya mzozo huo, Shilole alijitetea kwa kusema: Mi namdai rafiki yake 
fedha yangu ya shoo iliyobaki, kama shilingi laki nane hivi ndiyo maana 
nikaamua kuzizuia simu za huyu (Q Boy) hadi nimaliziwe pesa yangu.
Hata
 hivyo, katika sakata hilo ilielezwa kuwa Shilole na Q Boy hawakuwa na 
makubaliano yoyote kuhusu shoo hiyo na simu hizo hivyo madai ya 
mwigizaji huyo ni ‘usanii’ tu.
MAMA DIAMOND AINGILIA KATI KUOKOA
Zogo
 hilo lilipopamba moto na kuashiria kuvurugika kwa amani, mama mzazi wa 
Diamond, Sanura Kasim ‘Sandra’ aliamua kuingilia kati na kuagiza suala 
la kudaiana simu lifanyike kesho yake (Jumamosi) kwa vile siku hiyo 
haikuwa muafaka.
“Jamani! Jamani! We nani, Shilole na we Majaliwa, 
naomba kwa leo muepusheni shetani kwani hapa si mahali pake, ila kesho 
tutaitana na kumaliza suala hili, mimi mwenyewe nitalisimamia,” alisema 
bi mkubwa huyo na kumaliza henyahenya iliyoibuka.
JUMAMOSI YAFIKA, KIKAO VIPI?
Jumamosi,
 mapaparazi wetu walifuatilia ishu hiyo nyumbani kwa akina Diamond na 
kuulizia ili kujua kama kikao cha usuluhishi kilifanyika kama mama 
Nasibu alivyoagiza.
“Mh! Sijaona kikao chochote, kwanza Shilole 
mwenyewe akipigiwa simu hapokei,” alisema ndugu mmoja wa Diamond huku 
akiomba hifadhi ya jina lake.
MSIKIE DIAMOND
Juzi, Diamond alipopigiwa simu na kuulizwa kama anaijua ishu ya simu, alikubali.
Staa huyo alisema anashindwa kuingilia kati sakata hilo kwa sababu wahusika wote ni watu wake wa karibu kikazi.
“Yeah!
 Ishu ni kweli ipo, lakini mimi nilijiweka kando mapema, nikamwambia 
dogo (Q Boy) afuatilie mwenyewe baada ya kuona Shilole haeleweki.
“Unajua
 Shilole ni mwanamuziki mwenzangu, dogo yupo ndani ya Kampuni ya Wasafi 
Entertainment (ya Diamond), sasa kukomaa na ishu za simu tu nahisi 
itanishushia hadhi, napiga shoo za hela nyingi halafu leo nakomaa kwa 
hela ndogo, inakuwa siyo,” alisema Diamond.
SHILOLE TENA
Baada
 ya kuzungumza na Diamond, Shilole alipigiwa simu na kuomba kufafanua 
kwa undani ishu hiyo ambapo katika hali isiyotarajiwa, alimlalamikia 
paparazi wetu akidai anapendelea katika sakata hilo.
“Nyiye mnamtetea
 tu yule dogo, mimi sina tatizo, kama rafiki yake (aliyemuitia shoo 
Afrika Kusini) akinilipa hela yangu nawapa simu zao,” alisema Shilole.
Msanii
 huyo alikwenda mbele zaidi kwa kumwambia paparazi kuwa atatia timu 
kwenye Ofisi za Global Publishers ili kuzungumzia suala hilo na 
viongozi.
Baadaye Shilole alifika ofisini kwetu na kufafanua juu ya 
sakata hilo ambapo alirudia kukiri kuzuia simu hizo akidai kwamba 
anamdai Q Boy hivyo mpaka atakapomlipa ndiyo atampa simu zake.
Q BOY NAYE TENA
Kwa
 upande wake, Q Boy alipozungumza na paparazi wetu siku hiyo alisema 
amekusudia kwenda kufungua kesi kituoni ili apewe msaada zaidi wa 
kisheria kwa vile simu hizo zinamuuma hasa ukizingatia kuwa yeye siye 
aliyempeleka Shilole Afrika Kusini kufanya shoo.
“Mimi leo (Jumatatu)
 nimebanwa sana, kuna sehemu nakwenda na Diamond, nadhani nitamaliza 
jioni. Lakini kesho (Jumanne) nitaamkia polisi kufungua kesi nione 
watanisaidiaje?” alisema Q Boy.
POLISI AGUSIA ISHU
Risasi 
Mchanganyiko lilizungumza na askari mmoja kutoka Kituo cha Polisi cha 
Oysterbay na kummegea mtiririko wote, kisha kumuuliza kama kuna kesi 
ambapo alijibu:
“Japokuwa mimi si msemaji wa jeshi (la polisi), 
lakini ishu kama hiyo shitaka lake lipo, ni wizi wa kuaminiwa. Unajua 
wengi wanadhani kuibiwa lazima mtu uwe hujui, lakini mtu akifanya kama 
hivyo alivyofanya huyo msanii nani sijui (Shilole), kama ni kweli, kosa 
linakuwa wizi wa kuaminiwa endapo atafikishwa polisi.”
DIAMOND, Q BOY WALIFANYA MCHEZO?
Hata hivyo, baadhi ya watu walioshuhudia sakata hilo walikuwa na maswali kibao yaliyokosa majibu.
Swali
 la kwanza: Shilole alikwenda kufuturu kwa mwaliko wa Diamond na alijua 
staa huyo na Q Boy ni wamoja na simu alizopewa ilikuwa amletee msanii 
huyo, kwa nini alikwenda huku akijua ana msala?
Swali la pili: Kama 
Shilole alikwenda akijua Q Boy hayupo Bongo, je! Si kwamba ulikuwa 
mpango wa wawili hao kumwita ili wampe kibano ateme simu zao?
Swali 
la tatu: Je, ni kweli Shilole alizuia simu ili amaliziwe deni lake kwa 
mtu aliyemuitia shoo Afrika Kusini au shetani alimwingia baada ya kutua 
Bongo na kuamua kuzitumia hasa ikizingatiwa kuwa siku hizi mambo ya 
Instagram ndiyo habari ya mjini? 
CHANZO: GPL 
 
 
 
          
      
 
  
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment