Monday, 13 July 2015

Wachina wabuni uhujumu uchumi mwingine


Kwa sasa kumetokea mchezo mchafu unaofanywa na raia wa China na Singapore walio hapa nchini. Mchezo huu umeshamiri baada ya baadhi ya Wachina wasio waaminifu kushiriki biashara ya pembe za ndovu.
Wameanzisha utaratibu wa kusajili kampuni za kusafirisha samaki hai aina ya kaa na kamba kochi kwenda nje kwa kutumia kampuni zenye majina ya wazawa.
Wanachofanya ni kutafuta Mtanzania, wanampa pesa anakwenda idara zote zinazohusika na biashara hii. Wanasajili kampuni kwa kutumia majina ya Watanzania. Akishamaliza taratibu zote anakabidhiwa raia wa nje kinyume cha sheria ya Wizara ya Maendeleo Mifugo na Uvuvi, inayosema leseni haitakiwi kuazimishwa kwa mtu yeyote; na raia wa kigeni hawatakiwi kufanya hii biashara.

Wanatumia mawakala kuwanunulia kaa na kamba kochi hai, maana wao hawataki waonekane kwa sababu wanavunja sheria za nchi. Hata kwenda uwanja wa ndege watumia mawakala.
Mazao ya baharini yaliyovamiwa sana ni kamba kochi hai na kaa hai maana ndiyo yenye soko kubwa kwao. Nchi zinazoongoza kwa kununua kaa na kamba kochi hai wadogo sana na wenye mayai ni China na Hong Kong. Kwa wanavyonunua kwa wingi tusitarajie baada ya miaka miwili kutakuwa na viumbe hivyo hapa nchini. Kampuni vinara wa kusafirisha mizigo ya Wachina ni KN Marine, Marine Food Products Ltd, Sasha Marine Enterprise na NF Trading Co. Zote zina majina ya Watanzania, lakini zinatumiwa na Wachina. Kinara mkuu wa hii biashara haramu ni (jina tunalihifadhi kwa sasa). Amejenga mtandao mkubwa kuanzia Idara ya Uvuvi hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Amesajili kampuni zaidi ya nne kwa kutumia majina ya jamaa zake na marafiki zake wazawa, lakini zote zinatumiwa na Wachina na Wasingapore. Kinara mwingine yupo (jina tunalihifadhi kwa sasa).

Wachina hawa wananunua kaa na kamba kochi hai, wanakaa nao makwao walikopanga na wengine watumia viwanda walivyosajili kimagendo. Siku ya kusafirisha mzigo wanafunga kwenye maboksi, wakimaliza kufunga na kuweka lebo kuonesha anayesafirisha na kupokea mzigo huko nje kuendana na kampuni zilizosajiliwa hapa nchini, wanamtaarifu wakala kwamba anazo kilo ngapi na maboksi mangapi.
Wakala anakwenda Idara ya Uvuvi kukata vibali vya huo mzigo, kisha dereva anapeleka uwanja wa ndege. Dereva akitoka uwanja wa ndege na wakala anapeleka karatasi alizosafirishia mzigo kwa Wachina wanalipana pesa za uwakala. Kazi anayobaki nayo Mchina ni kutuma karatasi za mzigo kwao kwa faksi au kwa barua pepe ili mzigo ukachukuliwe uwanja wa ndege unakofikia.

Wakati wa kufunga mzigo wanaokuwapo ni Wachina na baadhi ya wafanyakazi wa Wachina wenye uelewa mdogo. Kinachofungwa humo wanakijua wao chini ya maboksi. Wakala (mzawa mwenye kampuni) anapokea tu uwanja wa ndege. Na kwa kuwa wana mtandao mkubwa, uwanja wa ndege wanapitisha hata kama kuna kaa wadogo, majongoo bahari na vitu vingine ndani.
Bei zao na zenyewe zinatia shaka kama kweli wanafanya hii biashara pekee, au wanatakatisha pesa wanazopata kwenye biashara nyingine, maana wananunua bei kubwa mno hapa nchini kiasi kwamba ukitoa na gharama za kuendesha kampuni, huwezi kupata kitu chochote.
Baadhi ya maafisa wa uvuvi wanawajua, lakini kutokana na kukithiri kwa rushwa, hawachukui hatua kali kukomesha hii hali, au kutotoa leseni holela za kusafirisha mazao ya baharini.

Watanzania waliosajili hizi kampuni wanachopata ni pesa ndogo wanayokubaliana kwa mwezi, kwa mwaka au kila mzigo unaposafirishwa.
Wanasafirisha kaa na kamba hai – wakubwa hadi wadogo kuanzia gramu 150 ambao hawaruhusiwi kisheria – kaa ambao hawajaanza kuzaa. Hao raia wa kigeni hawana uchungu na haya mazao ya bahari kwa sababu wanajua yakiisha watakwenda nchi nyingine ambako yanapatikana.
Kisheria wanaoruhusiwa ni kuanzia gramu 500 na kuendelea ndiyo wasafirishwe au kuvuliwa baharini.
Wazawa waliokuwa wanafanya biashara hii kihalali wameshindwa kwa sababu wananunua kuanzia wadogo sana mpaka wakubwa, wavuvi wanawakimbilia Wachina kwa sababu wananunua kaa wao wote. Sababu ya pili, wametumwa na kampuni zao kuja kukusanya na kuuza kule kwao kwa bei ya rejareja, hivyo ni ngumu kwa wazawa kushindana nao maana hatuna kampuni kwao. Wanatoa bei ndogo kwetu ili kampuni zetu zife wabaki wao kwenye soko la kununua na kusafirisha.

Faida yote inabaki kwao. Kinachorudi hapa ni pesa ya kununulia mzigo na kuendesha ofisi. Wengine wanatumia pesa wanayopata kwenye biashara nyingine kama Kariakoo ndiyo wanayonunulia samaki na nchi inakosa mapato ya kigeni.
Wanachama wa Chama cha Kusafirisha na Kuagiza nje Samaki (DAFIE) yaani Dar es Salaam Association of Fish Importers and Exporters wameshalalamika sana kuhusu hiyo biashara haramu na kuwaonya wahusika, lakini haikomi. Idara ya Uvuvi inatoa ushirikiano mdogo.
Badala ya hawa wazawa kuacha kubeba Wachina, wengine sasa wana Wachina zaidi ya watatu wanatumia leseni moja maana wameshanogewa. Miaka ya nyuma walipobanwa kwenye mkutano, kuna baadhi walikiri hadharani kwamba wanafanya hivyo kwa sababu hawana mitaji. Lakini kwa kadiri siku zinavyozidi kwenda hata baada ya kupata mtaji wamenogewa na hii biashara haramu hawataki kuiacha. Wanawaumiza wazawa wanaofanya biashara halali.

Ushahidi uko wazi kabisa. Ukienda Mbagala, Kigamboni, Soko la Samaki Ferry hadi Mkuranga wanakopokea mzigo kutoka Kusini, madalali wa kaa na kamba kochi wote wanajua kampuni zipi zinatumiwa na Wachina na zipi za wazawa. Hao ndiyo wapimaji na walipaji wa mzigo. Ukienda uwanja wa ndege ukafungua maboksi ya kaa na kamba wanaopelekwa China na Hong Kong, lazima utakuta kaa wadogo na wenye mayai. Kila siku mizigo inapita hapo.
Hii biashara haramu inafanywa kwa siri. Ukienda Idara ya Uvuvi wanakwambia aliyepeleka maombi ya leseni ni Mtanzania na ametimiza vigezo vyote ndiyo maana amepewa. Hata ukiwaambia kampuni fulani inafanya hivi au vile, wanataka ushahidi usiokuwa na shaka. Wakati mwingine wanasema sisi hatutaki au tunaogopa ushindani.

Hatukatai ushindani ila tushindane kwa njia sahihi na biashara endelevu. Baadhi  ya maafisa wanajua ila hawataki kutoa ushirikiano.
Tuna ushahidi mwingi. Mamlaka za juu zikitaka ushahidi tupo tayari kuzisaidia. Tulilo na hakika nalo ni kwamba Idara ya Uvuvi kwa sababu ya rushwa iliyokithiri, haiwezi kutoa ushirikiano.
Mwandishi wa taarifa hii amejitambulisha kuwa ni Mtanzania mzalendo. Ameomba jina lake lihifadhiwe, lakini amesema yupo tayari kuisaidia Serikali. Mawasiliano yote yapitie kwa Mhariri wa Gazeti la JAMHURI.

No comments:

Post a Comment