Tuesday 14 July 2015

Hisia kutoka Marekani na Iran

Rais wa Marekani Barrack Obama amesifu makubaliano baina ya Mataifa sita makubwa yenye nguvu duniani na Iran kuhusiana na mradi wake wa kinyuklia.
Rais Obama amesema kuwa hii ndiyo nafasi ya pekee na ya hakika itakayoizuia Iran isitengeze silaha za kinyuklia.
Obama ameonya kuwa atazima jaribio lolote la bunge la Congress la Marekani kupinga kupitisha makubaliano hayo kuwa sheria.
''Nataka kutoa onyo kwa bunge la Congress la Marekani, Nitatumia kura ya turufu kuzima jaribio lolote la kuzima kutekelezwa kwa mapatano hayo ya kihistoria.''alisema Obama.
Katika hotuba ya moja kwa moja kwenye televisheni, Rais Obama amekaribisha makubaliano hayo akisema kwamba jumuiya ya kimataifa sasa itaweza kuhakikisha kuwa Iran haiwezi kutengeneza silaha hizo za nyuklia.
Amesema vikwazo vitaondolewa taratibu na Iran ni lazima itimize baadhi ya hatua na masharti kabla ya vikwazo vyote kuondolewa.

Kwa upande wake Rais Rouhani amesema kuwa wamefurahi kuwa hatimaye vikwazo vyote vitaondolewa na fedha za Iran zilizofungiwa ng'ambo zitafunguliwa.
katika hotuba ndefu rais Rouhani amesema kuwa hawakuwa wanaomba washirikika wao kuwaondolea vikwazo bali walishirikiana.
'' hatukutaka kupewa msaada tuliwataka wenzetu tuwasiliane kwa heshma haki na usawa''

''Tulikuwa tunatafuta vitu vinne vikuu katika mawasiliano yetu na washirika wa kimataifa nayo ni
1,utafiti wa kinyuklia uendelee,
2,kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi
3,kuondolewa vipengee tuliyodhania kuwa ni ukiukwaji wa haki zetu katika umoja wa mataifa.

4, Sera kali za baraza la usalama la umoja wa mataifa dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran kufutiliwa mbali
''Kwetu tumepata kila kitu tulichokuwa tumepangia na hivyo naona kuwa tumefaulu'' alisema rais huyo katika taarifa iliyopeperushwa katika runinga ya taifa.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Javad Zarif, ameuambia mkutano huo kwamba majadiliano hayo ya muda mrefu yamaefanikisha kukabiliana na vikwazo vyote vigumu vya miaka kumi iliyopita.
Amesisitiza kwamba Iran haijakuwa ikijaribu kuunda silaha za nyuklia

 
Bwana Zarif amesema yaliyomo kwenye makubaliano hayo ni magumu mno, lakini hayakuwa makubaliano tu bali ni njia ya kuelekea kutatua uhasama wa muongo uliopita.
Vikwazo vya kiuchumi ikiwemo mabilioni ya fedha mali ya Iran iliyokuwa imefungiwa katika mabenki ya nje ya nchi inatarajiwa kuachiliwa katika siku za hivi karibuni.
Vikwazo hivyo vilivyozuia Iran kuuza mafuta na gesi yake katika soko la kimatifa vilevile ilizuia usafiri wa ndege na meli taifa hilo kuingiza bidhaa ambazo sio muhimu.
Awali Katika mkutano wa waandishi habari huko Vienna mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini alisema makubaliano hayo yanadhihirisha uwajibikaji wa pamoja kwa amani na kuifanya dunia kuwa salama.
Bi Mogherini Alisema mapatano hayo yamechangia kufikia masharti na malengo ya jamii ya kimataifa ya kuunda uhusiano.
Rais wa Iran kwa upande wake amesema kuwa ''mapatano hayo yamezuia taharuki ilikuwa bila sababu dhabiti''

No comments:

Post a Comment