Monday, 13 July 2015

Mzungu mchochezi anaswa Loliondo


Sweden, Susanna Nordlund, anayetambuliwa kama mmoja wa wachochezi wakuu wa migogoro katika eneo la Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha, amekamatwa na kufukuzwa nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ngorongoro, Hashim Shaibu, ndiye aliyeongoza Kamati hiyo kwenda kumkamata.
Sussana alikamatwa saa 2 usiku katika hoteli maarufu ya Onesmo iliyopo Wasso, akiwa anakula chakula.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa alifikia katika nyumba ya kulala wageni inayomilikiwa na aliyekuwa Mbunge wa Ngorongoro, ole Mathew Timan pamoja na mkewe, Tina.
Tina ni Mkenya aliyepata uraia wa Tanzania mwaka 2010. Ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa amepata nafasi hiyo kabla ya kuwa raia wa Tanzania. Anatuhumiwa kuwa miongoni mwa wachochezi wakuu wa migogoro katika Loliondo na Ngorongoro kwa jumla.
Susanna amekuwa akijiamini mno, hasa kutokana na kile anachosema kwamba endapo Serikali itaendelea kumfuata fuata, atahakikisha Sweden inakata misaada yake nchini.

“Tumesema sisi si maskini kiasi cha mtu kuvuruga nchi yetu kwa kigezo kuwa atatucongea ili tusipate misaada kutoka kwao. Ina maana tunapewa misaada kwa kigezo cha kutuvuruga?” Amesema mmoja wa viongozi walioshiriki kumkamata.
Hii si mara ya kwanza kwa Susanna kuingia nchini licha ya kuwa na PI. Kwenye mtandao wake wa Just Conservation, anatamba na kuonyesha namna alivyoweza kurejea nchini, kuzunguka na kufanya kilichomleta bila kuguswa. Hiyo ilikuwa Julai, 2013.
Shaibu amezungumza na JAMHURI na kuthibitisha kukamatwa kwa Mswiden huyo na kusema familia ya Timan inahojiwa kwa kumhifadhi Susanna.

Shaibu amesema mahojiano hayo yanalenga hasa kujua sababu za kumhifadhi Susanna ambaye kina Timan wanatambua kuwa alishapewa hati ya kufukuzwa nchini (PI) tangu mwakja 2010.
“Tulimkamata Juni 23 usiku. Alipohojiwa alikutwa na viti vingi ambavyo vingine ni hatari kwa usalama wa nchi. Alikuwa na questionnaire (maswali) mengi sana aliyopanga kuwauliza wanavijiji wa Oloipir, Mondorosi, Sukenya na vingine. Ni maswali ya uchochezi kabisa,” amesema DC Shaibu.
Amesema kwenye upekuzi huo ilibainika aliingia nchini kupitia mpaka wa Namanga akiwa na hatia ya kusafiria ikimwonyesha kuwa ni mtalii.
“Tulikaa naye hapa Loliondo (rumande) kwa siku tatu tukaona ni busara kumpeleka katika ngazi za juu mkoani. Mimi kama DC niliishia hapo,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Tibenda Kijiko, hakuweza kupatikana kuelezea hatima ya mchochezi huyo.

Hata hivyo,  Kamishna wa Huduma za Uhamiaji na Udhibiti wa Mipaka, Abdallah Abdullah, ameliambia JAMHURI kwamba Susanna baada ya kushikiliwa Loliondo na Arusha, alifukuzwa nchini.
Alipoulizwa imekuwaje mtu aliyepewa PI akaweza kurejea nchini bila kutambuliwa kwenye mifumo ya utambuzi ya kisasa, Kamishna Abdullah amesema: “Alipofukuzwa nchini mwaka 2010 mfumo wa utambuzi wa kutumia kompyuta ulikuwa bado. Ilibidi tufukue nyaraka kuweza kutambua kuwa alishafukuzwa.
“Hivi sasa baada ya kubaini hilo taarifa zote zinazomhusu tumeshaziingiza kwenye mtandao. Akiingia tu, akigusa dole gumba kwenye mashine mara moja atatambulika.”
Amesema wenyeji waliotumika kumhifadhi wanaendelea kuhojiwa na sheria za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Hapa tumesema hatuna huruma kwa watu wanaoshirikiana na wageni kuihujumu nchi yetu. Wananchi waendelee kutupatia taarifa za wageni na watu wanaowahifadhi.
“Mtu anajua kabisa huyu mgeni hatakiwi nchini, badala ya kumzuia yeye anamkaribisha. Mbaya zaidi hata kwenye hoteli hakuandika jina lake kwenye kitabu cha wageni. Hii ni kuonyesha kwamba walijua kinachofanywa na huyo mgeni,” amesema.
Kamishna Abdullah amemwagia sifa DC Shaibu kwa kusema muda mfupi alioshika madaraka hayo, Ngorongoro imekuwa na mabadiliko makubwa kwenye Uhamiaji.
“Amefanya kazi kubwa na nzuri sana kwa muda mfupi. Kazi yake imetusaidia sana, ni msikivu na anaonekana ana dhamira ya kuifanya Ngorongoro iwe sehemu salama,” amesema Kamishna huyo.
Awali, Susanna alifanya mikutano ya siri katika maeneo ya Kertalo na Karkamoru akiwa na Tina.

Mmoja wa wananchi wanaokerwa na uchochezi unaofanywa na asasi zisizo za serikali (NGO) amesema: “Nadhani kwa upeo wangu hizi ni harakati za kijasusi za wazungu na ukoloni mamboleo kutikisa Serikali ya Tanzania (To destabilize Tanzania Government wakimtumia Susanna Nordlung, wafadhili wa mataifa ya Magharibi, na mashirika ya kimataifa.
Wanazijengea uwezo NGOs zote za Wamasaai wa Kenya na Tanzania ili baadaye waweze kurudisha ardhi za Wamasai zilizochukuliwa na wakoloni wa Kiingereza na baadaye serikali za Tanzania na Kenya.

“Ardhi hizi kwa upande wa Tanzania ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, na Pori Tengefu la Loliondo kama sehemu za kuanzia na baadaye Hifadhi za Mikumi, Tarangire, nk.
“Mikakati ni kuunganisha umoja na NGOs za Kimasai ili wote wa Tanzania na Kenya waungane. Hawa watu (wafadhili wa Magharibi) siyo wazuri sana. Sasa hivi chunguza mabilioni ya fedha ambazo mashirika haya inazo pamoja na blogs. Ni hatari.”
Kwa muda sasa, Susanna na wadau wenzake wamekuwa wakikusanya mabilioni ya fedha kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa kile anachosema ni kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji na wenyeji “wanaonyanyaswa” katika maeneo yao.
Kupitia ufadhili wake, amekuwa akizimwagia NGOs fedha nyingi, huku silaha kuu ya kuhakikisha shughuli hiyo inaendelea ni kupandikiza migogoro ya mara kwa mara.
CREDIT: JAMHURI MEDIA

No comments:

Post a Comment