Wednesday, 1 July 2015

Membe Arudisha Fomu Ya Urais......Akana Kuhusika Na Ufisadi Wa Mabilioni Ya Libya.

MAKADA maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamerejesha fomu na kufafanua mambo kadhaa ambayo yamekuwa yanazungumzwa juu yao kama njia ya kujiweka sawa kabla ya uteuzi kufanywa na vikao vikuu vya chama hicho.

Mmoja wa waliorudisha fomu ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye wakati akirudisha fomu za kuomba kuteuliwa na kusema kuwa wanaochukulia suala la urais ni la kufa au kupona wana matatizo kwani anayejua Rais wa Tanzania ajaye ni Mungu.

Alisema safari yake ya kutafuta wadhamini ilikuwa na misukosuko mingi ikiwemo kutokea ajali tatu lakini hakuna ambaye alikuwa ameumia sana.

Akiwa ameongozana na mke wake, Tunu Pinda alisema mwana CCM mkomavu ni yule ambaye yuko tayari kukubali matokeo.

Alisema mpaka sasa ni wanachama wa CCM 42 waliojitokeza kugombea lakini katika hatua ya kwanza ni majina matano tu yatakayoteuliwa na kundi kubwa litaondolewa.

“Mimi sitegemei kwenye mchujo wa watu watano watokee watu wa kunung’unika kwani kila mtu aliyefika kuchukua fomu alikuwa anafahamu kuwa kutakuwa na mchujo kama tuko wengi wako watano kisha unakwenda ngazi ya pili, hakuna sababu ya kunung’unika,” alisema.

Alisema baadaye kuna kwenda kwenye Mkutano Mkuu atabaki mmoja. “Utanung’unikia nini? Kuna kushinda na kushindwa na kuna kupata na kukosa na ukisema suala la Urais ni kufa au kupona basi una matatizo, ifike mahali wana CCM wapate mtu ambaye wanadhani anaweza kusaidia kuongoza,” alisema.

Pia alisema waliojitokeza mwaka huu kuchukua fomu ni wengi. “Tuliojitokeza tusinuniane, kwa nini haniungi mimi mkono, na wewe usione jambo hili ni nongwa na usijione mapenzi ya Mungu yako kwako tu,” alisema.

Pia aliwataka viongozi wenzake washirikiane kumuunga mkono mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM. “Anayejua rais wa Tanzania atakuwa nani ni Mungu peke yake,” alisema.

Mwakyembe arudisha fomu
Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe jana alirudisha fomu na kusema CCM itapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu kutokana na kutekeleza ilani yake vizuri na wananchi kuwa na imani kubwa na chama hicho.

Mwakyembe ambaye alirudisha fomu jana mchana alisema katika safari yake ya kutafuta wadhamini mkoani ameweza kuwaona wanachama wengi wa CCM ambao wanaonesha imani kubwa na chama chao.

Alisema kila alipokutana na wana CCM waliojitokeza kumdhamini kwa tathmini aliyofanya tangu kuanza kwa siasa ya vyama vingi nchini CCM, itashinda ushindi wa kimbunga kwani mtaji upo kutokana na kazi kubwa iliyofanya serikali ya awamu ya nne katika utekelezaji wa ilani.

“Tumejipanga kuhakikisha wanaingia kwenye uchaguzi kifua mbele kutokana na kutekeleza ilani,” alisema.

Pia alisema kwa upande wa pili wana kazi ya kuhakikisha yote mazuri yaliyofanywa na CCM yanasemwa.

 “Tuna kazi ya kuhakikisha kuwakumbusha wananchi barabara za lami na mafanikio mengi yamepatikana na serikali ya awamu ya nne ya CCM,” alisema.

Alisema kazi kubwa ni kuhakikisha umma unatambua CCM imefanya mambo mengi kutokana na upotoshaji unaofanywa na wapinzani kuwa CCM haijafanya lolote.

Pia alisema CCM kuwa na wagombea wengi waliojitokeza mwaka huu ni dalili njema za CCM kutoa fursa za kupatikana mmoja ambaye kila moja atamuunga mkono ili kuweza kukivusha chama.

Dk Mwakyembe alisema yuko tayari kumuunga mkono mgombea atakayeteuliwa na chama. Awali alisema amezunguka katika mikoa 15 katika kutafuta wadhamini.

Dk Mwele Malecela
Mwanachama mwingine wa CCM aliyerudisha fomu jana ni Dk Mwele Malecela ambaye alisema pamoja na kazi kubwa iliyofanywa katika uongozi wa awamu nne bado kuna watu wanaoishi kwenye umasikini uliokithiri.

Alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari. Alisema alifanikiwa kupata wadhamini katika mikoa 20 ikiwemo 17 ya Tanzania bara na mitatu ya Zanzibar.

Alisema wananchi wameonekana kufarijika kuona wanafuatwa kwenye maeneo ya kata walipo. Alisema ameweza kuzunguka mikoa tisa kwa siku nne hali inayoonesha kuwa kazi kubwa imefanyika katika ujenzi wa barabara za lami kuunganisha mikoa.

‘Pamoja na maendeleo na kazi kubwa ya awamu zote bado kuna umasikini uliokithiri lazima kuliangalia suala hilo kama kiongozi na kulitafutia ufumbuzi,” alisema.

Alisema aliguswa sana na wanawake waliojitokeza wakiwemo wazee ambao walikuwa wakitaka kumuona ni mwanamke wa aina gani ambaye anataka kugombea Urais.

“Wanawake wamefurahi sana kuona wanawake tunajitokeza hii ni fursa nzuri ya kuwapa moyo akinamama kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika nchi,” alisema.

Membe Ayakana  Mabilioni  ya  Libya
Membe kwa upande wake wakati anarudisha fomu akijibu swali aliloulizwa kuhusu madai ya kuwa anahusika na ufisadi wa fedha za Libya na kama inavyosambazwa na wapinzani wake, alisema akigundulika kuwa alikula hata dola moja yuko tayari kujiuzulu.

“Uvumi kuwa nahusika na mabilioni ya Libya hauna mashiko kabisa baadhi ya wanasiasa wenzangu wanajua ukweli wote huu lakini kwa makusudi wameamua kuniunganisha na kampuni hiyo na kuwaaminisha watu ni yangu au nina hisa maneno hayo ni ya uongo,” alisema.

Alifafanua kuwa Libya ni moja kati ya nchi wafadhili wa Tanzania ambapo, kama ilivyo wafadhili wengine imekuwa ikiipa Tanzania misaada na mikopo yenye masharti nafuu.

Alisema katika utaratibu huo, Tanzania na Libya zilitia sahihi mkataba wa kubadili madeni na kuyaingiza katika miradi ambao uliweka utaratibu wa matumizi na urejeshaji wa fedha za deni la Libya.

Alisema kumbukumbu alizonazo zinabainisha kuwa kabla ya Serikali ya Libya kuweka saini katika mkataba wa nyongeza iliyotaka fedha hizo zikopeshwe kwa kampuni ya Meis, upembuzi yakinifu wa mradi husika ulifanywa kupitia vyombo vyake, na wao wenyewe kujiridhisha juu ya ubora wa mradi huo.

Sumaye na mahakama ya rushwa
 Naye Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye naye alirejesha fomu alisema akichagulia kuwa Rais wa nchi ataanzisha mahakama maalumu ya wala rushwa.

Mbali na rushwa pia vipaumbele vyake ni pamoja na ufisadi, uhujumu uchumi na kwamba ataunda chombo cha uchunguzi katika masuala hayo.

Pia alisema wakati akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania alifanya mambo makubwa na atahakikisha anaunda serikali inayofahamu kutimiza wajibu wake.

‘Uchumi ninaouzungumzia si wa takwimu ni wa hali halisi, nitaangalia pia maeneo kama viwanda vikubwa na vidogo ili watu wengi waweze kujiajiri na kulinda viwanda vya ndani,” alisema.

Alisema atahakikisha uzalishaji wa viwanda vya ndani unaongezeka na kunakuwa na ongezeko la mauzo ya nje ya nchi. Pia alisema ataimarisha huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya upatikanaji wa maji na huduma nyingine muhimu.

Alipohojiwa kama maeneo aliyokwenda kutafuta wadhamini aliombwa rushwa, Sumaye alisema, tangu aanze kazi ya siasa hajawahi kutoa rushwa.

“Hata maeneo ambayo nimekwenda kutafuta wadhamini sijatoa fedha hata zilizodaiwa kwa lugha laini nilikataa kwani nilitaka nidhaminiwe na wale walio na imani na mimi,” alisema.

Alisema wakati akiwa Waziri Mkuu alipambana na wala rushwa ambapo aliweza kuwafukuza kazi watu 3,360 huku wengine 400 walipelekwa mahakamani.

Balozi Mahiga
Balozi Mahiga naye wakati anarejesha fomu alisema ameenda mikoa 15 kwa gari na akawashukuru wana CCM kumlaki na kwamba wamehamasika na wanasubiri kwa hamu uchaguzi.

Alisema kama CCM ikimpitisha kuwa mgombea atahakikisha kuwa anajenga maadili ya uongozi ili kuondokana na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Alisema uongozi mzuri ni ule unaojengwa katika misingi ya maadili na atapambana na rushwa ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikirudisha nyuma wananchi wengi.

“Nitahakikisha ninaimarisha misingi ya umoja na mshikamano katika nchi ikiwa ni pamoja na kudumisha muungano wa Tanzania na Zanzibar,” alisema.

Joseph Chaggama
Mwanachama mwingine wa CCM aliyerudisha fomu jana ni Joseph Chaggama ambaye alisema amezunguka katika mikoa 17 wakati wa kutafuta wadhamini. Alisema anaijua CCM vizuri na jinsi Serikali inavyoendeshwa.

Alisema yeye ni mmoja wa watu wasiofahamika na sababu ya kuchukua fomu ni nia ya dhati kutoka moyoni kuwa anaweza kuongoza nchi.

Pia alisema uwezekano wa yeye kuchaguliwa lazima kutokee muujiza. Alisema yuko tayari kuwatumikia Watanzania ikiwa atapewa ridhaa ya kuwa mgombea wa CCM na akashinda uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Pia alisema yuko tayari kumuunga mkono mgombea ambaye atateuliwa na chama.

Monica Mbega
Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Monica Mbega naye alirudisha fomu na kusema kuwa chama kiliweka utaratibu mzuri wakati wakienda mkoani kupata wadhamini katika mikoa 15 ikiwemo mitatu ya Zanzibar.

Alisema amekamilisha kazi yake kwa ukamilifu bila matatizo na kuwashukuru wanawake wengi waliojitokeza kumuunga mkono.

Alisema suala la rushwa linategemea jinsi mtu alivyokwenda wakati akitafuta wadhamini.

Amos akemea matumizi makubwa ya fedha
Mwingine aliyerudisha fomu hizo jana ni Amosi Siyantemi ambaye ni mtumishi wa CCM wakati ambaye alisema kuwa kwenye mchakato wa kutafuta wadhamini baadhi ya wagombea wameonesha matumizi makubwa ya fedha.

“Ni jambo la kujiuliza fedha hizo wamepata wapi na ni kiasi gani ni lazima wachunguzwe na kuchukuliwa hatua,” alisema Siyantemi.

Pia alisema rushwa ni ugonjwa mbaya unaoiangamiza jamii ni lazima zichukuliwe hatua za haraka na makusudi ili kuweza kukomesha suala hilo kabla nchi haijatumbukia kwenye shimo la machafuko.

Alisema CCM ya sasa si kama ile ya Mwalimu Nyerere. “Tunahitaji kurejesha haraka heshima ya CCM machoni mwa Watanzania na kwenye macho ya Jumuiya ya Kimataifa,” alisema.

Alisema akichaguliwa kuwa Rais atahakikisha kunakuwa na huduma bora za matibabu sanjari na bima ya afya kwa kila Mtanzania, kufanya mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa elimu kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kupunguza idadi ya masomo.

Pia alisema atapiga marufuku mauzo na manunuzi yanayofanyika nchini kwa malipo ya dola ambapo malipo ya dola yatafanyika kwa kibali maalumu.

Pia alisema atakuwa na jukumu la kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya sanaa, michezo na burudani yatakayolenga kuwanufaisha kiuchumi wananchi.

No comments:

Post a Comment