Wakati Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari akisema 
anashindwa kuamini kilichotokea na kunusurika katika ajali ya helikopta 
juzi, mmiliki wa chopa hiyo, Philemon Ndesamburo amesema atanunua 
nyingine haraka kabla ya kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu. 
Kauli hizo zilitolewa jana ikiwa ni siku moja baada ya 
helikopta hiyo inayomilikiwa na Ndesamburo kupitia kampuni yake ya Keys 
Aviation kupata ajali wakati ikitumiwa na Nassari na baadhi ya viongozi 
wa Chadema.
 
Wakati ikipata ajali, ilikuwa imekodishwa na Kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd inayomilikiwa na Kapteni William Slaa.
 
Katibu wa Ndesamburo, Basil Lema alisema ilipata ajali 
baada ya kupigwa na kimbunga wakati anga likiwa limefunikiwa na wingu 
zito.
 
“Mheshimiwa Ndesamburo amemshukuru Mungu kwa kuwanusuru 
watu waliokuwa kwenye ndege hiyo ambao ni pamoja na Mbunge Joshua 
Nassari.
 
“Ameweka wazi kwamba atalazimika kununua nyingine mapema
 kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 
huu,” alisema Lema akimnukuu Ndesamburo.
 
Lema alisema rubani aliyekuwa akiendesha helikopta hiyo 
alifanikiwa kuielekeza juu ya miti alioutumia kupunguza kasi ya kushuka 
chini na kusaidia abiria kutoka salama.
 
“Imeharibika lakini abiria wote ni wazima. Walikuwamo wanne,” alisema
 na kuongeza kuwa helikopta hiyo ndiyo iliyotumiwa na Chadema katika 
Uchaguzi Mkuu wa 2010 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana na 
chama hicho kilitegemea kuitumia katika Uchaguzi Mkuu ujao.
 
Pia, imewahi kutumiwa na makada mbalimbali wa CCM akiwamo 
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba na kada maarufu wa Moshi 
mjini, Buni Ramole.
 
Kauli ya Nassari
Akizungumza na waandishi wa habari katika wodi alikolazwa 
kwenye Hospitali ya Seliani – Arusha, Nassari alisema waliporuka kutoka 
Leguruki, hakukuwa na dalili zozote za kuchafuka kwa hali ya hewa, 
lakini dakika chache baada ya kuruka angani wingu zito lililoambatana na
 upepo mkali liliwafunika ghafla.
 
“Wingu lile na upepo ule sijawahi kuona katika maisha 
yangu yote zaidi ya kusoma kwenye vitabu vya simulizi vya mambo ya 
ushirikina. Namshukuru Mungu wote tuko salama kwani hatukuwa na 
matumaini ya kupona ajali ile,” alisema Nassari.
Mbunge huyo aliyekuwa katika ziara ya kuhamasisha wananchi 
kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura, alimwagia sifa rubani Slaa 
kwa uwezo na ustadi aliouonyesha hadi wakanusurika.
 
“Kama siyo ustadi wake, naamini watu wangeokota vipande 
vya nyama tu kwenye eneo la ajali, ila Mungu ni mkuu leo tuko hai wote 
licha ya madhara madogo,” alisema.
 
Nassari alisema muda mfupi kabla ya kuruka saa kumi na moja
 jioni, wakati akihutubia mkutano huko Leguruki, alipokea simu kutoka 
kwa mchungaji mmoja akimtaarifu kupata maono kuwa anakabiliwa na hatari 
ya kukutwa na jambo kubwa na baya akimtaka adumu katika sala.
 
“Dakika 15 baadaye nikaruka na kupata ajali. Naamini 
kilichotuokoa ni nguvu ya sala niliyosali baada ya kupokea ujumbe wa 
mchungaji na maombi ya wachungaji wangu wanaoniombea kila siku,” alidai Nassari.
 
Rubani Slaa alisema alishangaa lilipotokea wingu na upepo 
uliosababisha ndege kuanguka ikiwa njiani kuelekea Ndoombo na 
Ngureserosambu.
 
“Kabla ya kurusha ndege nilijiridhisha na hali ya hewa. 
Hakukuwa na kiashiria chochote cha hali ya hatari kama maeneo mengine 
ambako tulishindwa kutua kutokana na mvua zilizokuwa zikinyesha."
 
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Seliani, Dk Paul Kisanga 
alisema hali za majeruhi si mbaya, isipokuwa Eva Kayaha aliyevunjika 
mbavu mbili.

 
No comments:
Post a Comment