PROFESA
Mwesiga Baregu
PROFESA
Mwesiga Baregu, mmoja wa watu wanaoheshimika nchini amesema, aliyepata
kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, anaponzwa na
kibuli cha kujiona hakuna zaidi ya yeye.
Amesema, Zitto ambaye alikuwa naibu katibu mkuu wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tanzania Bara na naibu
kiongozi wa upinzani bungeni, anafanya kazi asiyoifahamu na ambayo haina
mavuno.
“Ninamfahamu
vizuri. Wakati tuhuma hizi za usaliti zilipoanza kuibuka, Kamati Kuu
ilinikabidhi jukumu la kumsaidia mama yake mzazi kumlea kijana huyu.”
Kauli ya Baregu ilitolewa siku moja baada ya Zitto kujiondoa bungeni na baadaye kujiunga na Chama cha ACT – Tanzania.
Prof. Baregu aliwahi kuwa “mlezi wa Zitto” ndani
ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Alikabidhiwa jukumu hilo
na Shida Salum, mama mzazi wa Zitto (marehemu), baada ya mama huyo
kuiomba Kamati Kuu (CC) ya chama hicho “kusaidia kumlea.”
Prof. Baregu ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya
Chadema anasema, “Zitto hamnazo. Amekuwa anajiona yeye ni zaidi ya
chama. Hashauriki.”
Anasema wakati ule alipopewa kazi ya kumlea Zitto
“katikakati ya migogoro, tulikuwa tunazungumza naye mara kwa mara.
Ninamfahamu. Kazi hii ya kumlea tulikabidhiwa mimi na mama yake mzazi,
Bi. Shida Salum,” anaeleza Baregu.
Mama mzazi wa Zitto, alifariki dunia Juni mwaka jana, baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kauli ya Prof. Baregu ilifuatia gazeti hili kutaka
maoni yake juu ya mustakabali wa kisiasa wa Zitto baada ya kuwahi
kujiondoa ndani ya Chadema.