Monday 30 March 2015

Rais Nkurunzinza wa Burundi amfuta kazi msemaji wake mkuu

 

Kufuatia joto la kisiasa ambalo limeendela kupanda nchini Burundi, huku chama tawala Cndd- Edd kikikumbwa na mgawanyiko, rais Pierre Nkurunziza, amemfuta kazi msemaji wake, Léonidas Hatungimana.

Wakati huohuo, Pierre Nkurunziza amewateua wasemaji wake wapya, ikiwa ni pamoja na msemaji wake mkuu, Gervais Habayeho pamoja na naibu msemaji wake Louis Kamwenubusa, aliyekua mkurugenzi wa redio inayomilikiwa na chama cha Cndd-Fdd, Rema Fm. Mkurugenzi mkuu wa redio na televisheni vya serikali (Rtnb), Thadée Siryuyumunsi amefutwa kazi, na nafasi yake, ameteuliwa Jérôme Nzokirantevye, aliyekuwa msemaji wa spika wa Bunge.

Sakata hilo lakuwafuta kazi baadhi ya vigogo katika taasisi mbalimbali za nchi linakuja baada ya vigogo hao wakiwa pia wafuasi wenye ushawishi mkubwa katika chama tawala Cndd-Fdd kutia saini kwenye waraka unaomtaka rais Pierre Nkurunziza kutogombea muhula wa tatu katika uchaguzi ujao wa urais.

Hata hivyo wafuasi hao wa chama tawala wameapa kutotetereka na uamzi huo wa kuwafuta kazi, huku wakibaini kwamba wataendelea na msimamo wao hadi pale rais Nkurunziza atakubali kusitisha nia yake ya kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi wa urais unaopangwa kufanyika mwezi Juni.

No comments:

Post a Comment