Monday, 29 June 2015

Waangalizi wa UN Burundi wamefuatilia uchaguzi

 

Uchaguzi wa Bunge na serikali za mitaa ulifanyika jana nchini Burundi, licha ya shinikizo la jamii ya kimataifa la kutaka uahirishwe kutokana na mazingira ya kisiasa na kiusalama.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kufuatilia uchaguzi nchini Burundi, MENUB umesema waangalizi wake 36 wamefanikiwa kufuatilia uchaguzi bila kutishiwa usalama wao.
Msemaji wa MENUB Vladimir Monteiro, akihojiwa jana, alisema waangalizi wa MENUB wametembea kwenye majimbo yote ya Burundi ili kufuatilia utaratibu huo na kuandaa ripoti kwa ajili ya Katibu Mkuu na Baraza la Usalama.

Serikali ya Burundi ilishikilia msimamo wake wa kufanya uchaguzi jana tarehe 29 Juni, kinyume na mapendekezo ya timu ya uhamasishaji iliyohusisha Umoja wa Mataifa na mashirika ya kikanda, ya kuhairisha uchaguzi hadi Julai, tarehe 30.

Monteiro ameeleza msimamo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuhusu uamuzi huo.Ameongeza kuwa Katibu Mkuu amesikitishwa kwamba mapendekezo ya timu ya uhamasishaji kuhusu kuhairishwa kwa uchaguzi hayakusikilizwa, lakini kwamba anaendelea kuwaomba wadau wa Burundi waendelee kufanya kazi ili kupata suluhu kupitia mazungumzo, bila ghasia.

No comments:

Post a Comment