Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi
wasikilizaji na karibuni katika kipindi chenu chenye faida tele cha
Ijue Afya Yako. Leo tutazungumzia tatizo la maambukizi katika njia ya
mkojo Urinary Tract Infection ugonjwa ambao unawasumbua sana wanawake
wengi na watoto katika nchi nyingi zinzoendelea.
&&&&&&
Maambukizi katika njia ya mkojo au kama unavyojulikana kwa wengi UTI huathiri mfumo wa mkojo ikiwa ni pamoja na ureter ambayo ni kama bomba linalosafirisha mkojo kutoka kwenye figo, pia kibofu cha mkojo na urethra. Ugonjwa huu unaathiri zaidi kibofu cha mkojo na urethra lakini unaweza pia kuathiri figo. Maambukizi haya yakiathiri sehemu za chini za kibofu cha mkojo kitaalamu huitwa simple cystitis au Bladder infection, na maambukizi hayo yakitokea sehemu za juu za mfumo wa mkojo huitwa pylonephritis au kidney infection. Ugonjwa huu husababishwa na bakteria anayeitwa Escherichia coli (E. coli) na tatizo hili husababishwa kwa kiasi kikubwa na bakteria ambao makazi yao ya kawaida ni kwenye utumbo mpana, na hivyo huwa wanapatikana pia kwenye haja kubwa. Lakini baadhi ya watu wanaweza kupata tatizo hili kutokana na kuingiwa na fangasi ingawa pia zipo sababu nyingine chache. Bakteria wa Escherichia coli hawasababishi peke yao UTI bali huambatana na wengine waitwao staphylococcus, saprophyti cus, pseudom onas, enterobacter na kadhalika. Maambukizi katika njia ya mkojo lazima yawe ni kwenye njia ya mkojo na si pengine popote. Wapo wanawake ambao wamekuwa wakidhani kwamba tatizo la kutokwa na uchafu ukeni ni ugonjwa huu, na hilo si sawa kwani huo ni ugonjwa tofauti kabisa na UTI. Tunapozungumzia maambukizi katika njia ya mkojo, inamaanisha ni kutoka eneo la nje ya utupu hadi kwenye kibofu na kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo. Kama maambukizi yako katika eneo la kutoka kwenye kibofu hadi kwenye figo, kitaalamu huitwa Lower Urinary Tract Infection na yakihusisha eneo la juu ya kibofu jina hubadilika na kuitwa, Upper Urinary Tract Infection. Mara nyingi maambukizi haya kwa wanawake husababishwa na kutojisafisha vizuri sehemu za siri na kuvaa nguo za ndani zilizochafu. Pia huweza kusababishwa na matumizi ya pedi za kike zenye kemikali ya kukata harufu ambazo huua bakteria wa asili wa eneo la uke na kuwapa fursa bakteria wanaosababisha maradhi kuzaliana kwa wingi. Halikadhalika upungufu wa homoni ya wanawake iitwayo Oestrogen husababisha bakteria wanaosababisha maambukizi katika njia ya mkojo kuzaliana kirahisi. Matumizi ya baadhi ya dawa kwa muda mrefu, unywaji wa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu na kutokunywa maji ya kutosha pia huchangia tatizo hili. Uwepo wa mawe katika figo na mirija ya figo pia ni mojawapo ya chanzo cha maambukizi haya katika njia ya mkojo. Sababu nyingine inayosababisha UTI ni matumizi ya maji machafu wakati wa kujisafisha au kuoga ambayo huweza kuweka bakteria kwa urahisi na kupelekea mwanamke kupata ugonjwa huo. Uchafu wa vyoo umetajwa kuwa sababu nyingine, kwani matumizi ya vyoo ambavyo ni vichafu huweza kusababisha mwanamke kupata UTI kwa sababu ndani ya choo kuna bakteria wengi ambao wanaweza kusababisha ugonjwa huo.
&&&&&&
Matatizo haya ya maambukizi licha ya kuwapata zaidi wanawake, huwakumba pia watoto wadogo wa kike kutokana na sababu za kimaumbile ambapo viungo vyao vya uzazi, njia ya mkojo na haja kubwa vipo jirani. Watoto wa kiume ambao hawajatahiriwa nao huweza kupata maambukizi rahisi ya UTI iwapo watajisafisha kwa kutumia maji yasiyo salama ambapo huwa rahisi kwa bakteria kubaki katika ngozi inayoning'inia (govi). Pia wanaume watu wazima ambao hawajatahiriwa wanaweza kupata maambuzi ya UTI kutokana na sababu tuliyoitaja ambapo pia ni rahisi kwao kuambukizwa Ukimwi kama watafanya ngono zembe na ndiyo maana tohara kwa wanaume husisitizwa.
Maambukizi yanayoshambulia mfumo wa mkojo husababishwa zaidi na bakteria wanaoishi katika mfumo wa haja kubwa kwa kuingia na kujikita katika mfumo wa mkojo. Bakteria wengine wanaoleta maabukizo katika njia ya mkojo ni wale watokanao na magonjwa ya zinaa kama kisonono, klamidia, trimonas na fangasi ambapo huwaathiri watu pale wanapojamiiana bila kutumia kinga na watu wenye maradhi hayo. Ili kuepuka kupata maambukizi katika njia ya mkojo, mara kwa mara, ni vyema kutumia kinga na kwa mwanamke wanashauri kila wanapomaliza kufanya tendo la ndoa wakojoe ili kuondoa bakteria walioingia au waliokaa katika tundu ya mkojo wakisubiri kuingia. Baada ya kujua hayo yote hivi sasa tuzijadili dalili za ugonjwa wa UTI.
Baadhi ya dalili za mtu kuambukizwa bakteria katika njia ya mkojo kubwa ni maumivu wakati wa kukojoa, mkojo kuwa na rangi ya njano kupindukia na kuwa na harufu kali ijapokuwa siyo kila mwenye dalili hizo ana maambukizi katika njia ya mkojo. Dalili nyingine za UTI ni maumivu, kutokwa na usaha wakati wa kukojoa, kabla au baada ya kukojoa kukiambatana na maumivu na kuhisi moto wakati mkojo ukitoka. Baadhi ya wanaume wakati mwingine hutokwa na majimaji katika njia ya mkojo wakati wa kujisaidia haja kubwa. Wengine wenye maambukizi hujikuta wakipata vichomi katika njia ya mkojo, au kuhisi kuwashwa sehemu hiyo, kuumwa kiuno au tumbo na kadhalika. Mgonjwa anaweza pia kukumbwa na homa kali mara kwa mara na mwili kuwa mchovu, kwa watoto hupoteza hamu ya kula na mwili huonesha kuchoka.
Wagonjwa wengine hupata maumivu kwenye kibofu cha mkojo ambapo husikia maumivu ya chini ya tumbo usawa wa kitovu na huwa hayaishi. Matatizo haya ya mfumo wa mkojo kama tulivyoona kabla huwapata watu wote wanawake na wanaume. Watu wenye matatizo haya kila wakipima huambiwa wana UTI. Kwa wanaume huhisi hata nguvu za kiume kupungua na wanawake hupoteza hamu ya tendo la ndoa.
Kwa wajawazito ugonjwa unaweza kuhatarisha maisha yao na mtoto aliye tumboni. Bakteria wanaweza kuingilia mfumo wa damu na kusababisha madhara mengine kama vile shinikizo la damu kuwa kubwa kwenye figo na hata kusababisha ufanyaji kazi mbovu wa figo.
&&&&&
Maambukizi katika njia ya mkojo hutibika kwa dawa mbalimbali za kisasa baada ya kufanyiwa vipimo na kuthibitika kuwa mgonjwa ana maambukizi hayo. Dawa ambazo anaweza kupewa ni kama vile Ciprofloxacin, Monurol, Furadantin, Sulfam ethoxazole, co-trimax, ampicillin, gentamicin na kadhalika. Mgonjwa anayesumbuliwa na UTI hapaswi kutumia dawa yoyote bila kwanza kupata ushauri wa daktari.
Wanawake wanashauriwa kuepuka kujisafisha sehemu za siri na maji machafu na yasiyo salama, pia kuepeuka kupaka marashi sehemu hizo, ama kutumia pamba zenye kemikali ya kukata harufu kwani hizo huua bakteria wa asili wa ukeni hali ambayo hukaribisha bakteria wa maradhi kuzaliana kwa wingi. Pia wanashauriwa wanapojisafisha baada ya kujisaidia kuanzia mbele kwenda nyuma, ili kuepusha kuhamisha bakteria walio eneo la haja kubwa na kuingia njia ya mkojo. Kwa wale walio katika kipindi cha ukomo wa hedhi, wanaweza kushauriana na daktari juu ya kutumia oestrogen ya ukeni ili kuwasaidia kujikinga na maambukizi ya UTI. Kwa mwanaume maambukizi haya huathiri nguvu za kiume na kujipenyeza hadi katika korodani na huathiri uzalishaji wa mbegu za kiume na kunaweza hata kusababisha mgumba. Hivyo wanashauriwa kuhakikisha wanatibu bila kuchelewa ugonjw ahuo. Pia maambukizi ya njia ya mkojo huweza kusababisha matatizo ya tezi ya kiume (prostate) kwani husababisha mrija wa mkojo kuziba, kutopitisha mkojo vizuri na kuruhusu bakteria kujenga makazi. Hali hiyo ikitokea mgonjwa lazima akamuone daktari ili awekewe mrija wa kutolea mkojo.
Mpenzi msikilizaji madaktari wanatueleza kuwa, tunaweza kuudhibiti au kuponya ugonjwa huu kwa kunywa maji mengi pamoja na juisi itokanayo na matunda halisi, iwapo tutawahi kabla tatizo halijawa sugu. Kwa maana nyingine, unaweza kujikinga na ugonjwa huu kwa kuwa na mazoea ya kunywa maji ya kutosha kila siku. Ukinywa maji ya kutosha yatakufanya uende haja ndogo kila mara na kwa njia hiyo wale bakteria watakuwa wakitoka na hatimaye kuisha kabisa. Katika hali ya kawaida, ugonjwa wa UTI hutoweka ndani ya siku tatu mara baada ya kuanza kutumia tiba asili ya kunywa maji mengi na juisi ya matunda halisi, iwapo ugonjwa utaendelea kuwepo baada ya siku hizo, hiyo itakuwa na maana ugonjwa wako umeshakomaa na hivyo hauwezi kutibika kwa tiba hii ya nyumbani na itakuwa inapaswa kwenda hospitalini na kuonana na daktari ambaye atafanya uchunguzi na kutoa dozi sahihi ya kutibu ugonjwa huo.
Wasikilizaji wapenzi tutaendelea kujadili ugonjwa wa maambukizo katika njia ya mkojo kwenye kipindi chetu kijacho. Hadi wakati huo tusisahau kuzilinda afya zetu na kwaherini.
CHANZO: IRAN SWAHILI REDIO
No comments:
Post a Comment