1.0. Libya ni moja kati ya nchi wafadhili
wa Tanzania ambapo, kama ilivyo wafadhili wengineimekuwa ikiipa nchi
yetu misaada na mikopo yenye masharti nafuu. Serikali yetu imekuwa
ikifanya taratibu mbalimbali kulipa madeni ya nchi wafadhili kwa njia
mbalimbali ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kubadili madeni na kuyaingiza
katika miradi n.k, yaani ‘Dept Swap’.
2.0. Katika utaratibu huo wa ‘Dept Swap’, tarehe 20/7/2005,
Serikali ya Tanzania na Libya zilitia sahihi mkataba wa Dept Swap (Dept
Swap Agreement) ambao uliweka utaratibu wa matumizi na urejeshaji wa
fedha za deni la Libya.
3.0. Tarehe 4/3/2009, Serikali ya Libya na Tanzania zilitia
sahihi mkataba wa nyongeza (Addendum to the Dept Swap Agreement) ambao
ulizungumzia, pamoja na mambo mengine, matumizi ya jumla ya dola za
Kimarekani milioni 20 (20,000,000) ambazo zilikuwa zimehifadhiwa katika
akaunti ya Libya No.004-200-0002216-01, Benki ya Rasilimali Tanzania
(Tanzania Investment Bank).
4.0. Nyongeza hii ya mkataba ilitamka bayana katika kifungu
No.4.02, kwamba, fedha zilizokuwa katika akaunti tajwa, zikopeshwe kwa
mwekezaji waliyemteua wao wenyewe, ambaye ni kampuni ya MEIS INDUSTRIES
LIMITED kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Saruji Lindi. Kwa
mujibu wa nyongeza hii, mkopo ulipaswa kulipwa ndani ya miaka sita, na
baada ya hapo, fedha hizo zirejeshwe na ziendelee kukopeshwa Watanzania
kwa ajili ya miradi mingine ambayo Serikali za Libya na Tanzania
zitakuwa zimeridhia.
5.0. Kumbukumbu zinaonyesha mambo mawili:-
5.1 Kwamba, kabla ya Serikali ya Libya kutia sahihi nyongeza hii ya
mkataba iliyotaka fedha zikopeshwe kwa MEIS INDUSTRIES, upembuzi
yakinifu wa mradi husika ulifanywa na serikali ya Libya kupitia vyombo
vyake, na wao wenyewe walishajiridhisha juu ya ubora wa mradi huo
(Viability of the Project)
5.2 Kwamba, baada ya kutia sahihi nyongeza ya mkataba, Serikali ya
Libya kupitia Ubalozi wake hapa nchini iliendelea kusisitiza kwa
maandishi kwamba Serikali ya Tanzania iharakishe mchakato wa kuwezesha
fedha hizo zikopeshwe kwa mwekezaji waliyemteua ili mradi huo muhimu
usiendelee kuchelewa, na pia fedha ziingie katika mzunguko kwa manufaa
ya Watanzania.
6.0. Katika kutekeleza mikataba hii miiwli, yaani Dept Swap Agreement ya
tarehe 20/7/2005 na Addendum Dept Swap Agreement ya Tarehe 4/3/2009, na
kwa kuzingatia umuhimu ambao serikali ya Libya iliuonyesha, Serikali ya
Tanzania kupitia watalaamu wake wa Wizara ya Fedha, Benki ya Rasilimali
(TIB) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, na Mwekezaji (Kampuni ya MEIS),
walikutana chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na kuandaa hadidu za
rejea ambazo zilipelekea kutengenezwa kwa mkataba wa uwekezaji
(Investment Agreement) kati ya serikali ya Tanzania, TIB, Serikali ya
Libya na Mwekezaji.
7.0. Serikali ya Tanzania, TIB na Mwekezaji walitia sahihi mkataba huu
na kuupeleka Libya ili serikali ya Libya ipate kuweka sahihi. Kwa sababu
ambazo hazikufahamika, serikali ya Libya haikutia sahihi mkataba huo.
8.0. Baada ya kufuatilia kwa muda mrefu bila mafanikio, mwekezaji
alimuandikia barua Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania yenye
kumbukumbu No. PC/MEIS/AG/2/10 ya tarehe 1/9/2010 akieleza kusudio la
kuipeleka Serikali ya Libya Mahakamani kwa kitendo chake cha kutokutia
sahihi mkataba.
9.0. Terehe 13/9/2010, Mwekezaji alifungua shauri Mahakama Kuu ya
Tanzania, shauri la madai No. 124/2010 dhidi ya serikali ya Libya,
akiiomba Mahakama Kuu itoe tamko kwamba kitendo cha serikali ya Libya
kukataa kutia sahihi mkataba huu hakikuwa kitendo cha haki na kwamba
mahakama itoe amri kwamba fedha hizo zitolewe kwa Mwekezaji ili
kutekeleza mradi uliokusudiwa.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba wito wa Mahakama (Summons) ulipelekwa
Ubalozi wa Libya lakini hapakuwa na majibu wala mwakilishi aliyekuja
mahakamani.
10.0. Mahakama Kuu, kwa kufuata taratibu zake, iliendelea na kusikiliza
shauri na kutoa amri kama ambavyo mahakama yenyewe ilijiridhisha. Amri
ya mahakama, pamoja na mambo mengine, iliagiza kwamba fedha hizo
zitolewe kwa mwekezaji ili kutekeleza mradi husika.
11.0. Zilifanyika juhudi za Benki ya Rasilimali (TIB) pamoja na Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupinga au kupata ufafanuzi zaidi juu ya
amri hiyo ya utekelezaji wake. Mahakama Kuu pamoja na Mahakama ya
Rufana, katika nyakati tofauti, zilishughulikia maombi hayo na
kuyafikisha katika hatima yake kwa mujibu wa sheria. Kwa ajili ya
kumbukumbu, mashauri yaliyofunguliwa ni kama ifuatavyo:-
11.1 TIB ilifungua maombi No. 126/2010 katika mahakama ya Rufaa
kuiomba izuie na kufuta utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu. Maombi haya
ya TIB yalifanyiwa uamuzi wa mwisho mnamo tarehe 7/11/2011, ambapo
maombi hayo yaliondolewa mahakamani kwa kuwa, kwa mujibu wa Mahakama ya
Rufaa, hayakuwa yamefuata taratibu za kisheria.
11.2 Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye akapeleka maombi Mahakama ya
Rufaa. Maombi ya kwanza, maombi namba .146/2010 akiomba Mahakama ya
Rufaa kufuta mwenendo mzima wa kesi pamoja na amri ya Mahakama Kuu, na
maombi ya pili No. 147/2010 ikiiomba Mahakama ya Rufaa izuie utekelezaji
wa amri ya mahakama Kuu (Stay of Execution). Maombi haya yote
yalisikilizwa na kuamuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za
kimahakama.
12.0 Wakati haya yakiendelea, ilijitokeza kampuni ya Mohamed
Enterprises Limited ikidai kwamba ina haki juu ya fedha hizi. Nayo
ikafanya yafuatayo:-
12.1 Ilipelea maombi Mahakama Kuu kuzuia utekelezaji wa hukumu kwa
madai kuwa kampuni hiyo nayo ilikuwa ikiishtaki Serikali ya Libya
katika kesi ya madai No. 110/2010 na kwa hiyo, endapo amri ya Mahakama
Kuu ingetekelezwa kwa kumpa mwekezaji (Kampuni ya MEIS) fedha za Libya,
basi wao (Mohamed Enterprises Limited) wangekosa mahali pa
kutekeleza/kukazia hukumu waliyokuwa wakiitarajia katika kesi yao (no.
110/2010) dhidi ya serikali ya Libya. Maombi haya yalisikilizwa na
Mahakama Kuu na kutolewa maamuzi stahiki.
12.2. Kampuni ya Mohamed Enterprises Limited haikuridhika na
uamuzi wa Mahakama Kuu kwa hiyo kapeleka shauri hili Mahakama ya Rufaa,
kupitia maombi (Civil Revision) No. 2/2011. Maombi haya nayo pia
yalisikilizwa na kutolewa maamuzi.
13 Mwisho wa yote maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa katika
mchakato mzima yakawa kwamba mwekezaji (Kampuni ya MEIS) alikuwa na haki
ya kupewa fedha za mradi wa Kiwanda cha Saruji Lindi kama ilivyoanishwa
katika mkataba kati ya serikali ya Tanzania na Libya. Ni dhahiri
kwamba, mgogoro huu ulichujwa na mahakama mpaka ngazi ya juu kabisa,
tena kwa nyakati tofauti na mbele ya waheshimiwa majaji wa Mahakama Kuu
na Mahakama ya Rufaa.
14.0 Katika Taifa linaloongozwa kikatiba, chini ya utawala wa sheria
kama Tanzania, ambapo Mahakama ndicho chombo kilichopewa mamlaka ya
mwisho kuamua juu ya haki za raia na hata serikali, si rahisi na wala
haitakuwa sahihi kwa mtu yeyote kuhoji uhalali wa mchakato huu kama
ulivyoongozwa, kuelekezwa na kuamuliwa na mahakama, isipokuwa tu kama
sheria inatoa mwanya mwingine kurudi mahakamani kwa mtu yeyote ambaye
hajaridhika au anayetaka kuhoji maamuzi haya kwa namna yoyote.
15. Mahakama iliamua kwa mujibu wa sheria. Na kwa kuwa hakuna
aliyeendelea kupinga kimahakama, suala hili lichukuliwe kwamba limefikia
mwisho na limefungwa. Lakini hata kiuongozi, na hasa kwa mtu yeyote
mwenye kutazama maslahi ya Taifa hili, ni dhahiri kwamba suala la
utekelezaji wa mikataba ya kubadilishana madeni ni jambo lenye manufaa
kwa Tanzania na linapaswa kila fursa inapojitokeza kutekelezwa haraka.
Wenzetu, nchi wafadhili, wanapotoa fursa za kutupunguzia mzigo wa madeni
katika utaratibu wenye manufaa kama huu, tutaendelea kuonekana wa ajabu
kama tutaendelea kulumbana badala ya kuchangamkia fursa ya maendeleo.
Tukwepe mazingira yanayopelekea taifa letu kuonekana kama wale watoto
watukutu waliokabidhiwa zawadi ya nyumba, badala ya kuishi kwa shukrani
ya nyumba ile, wakagombana na kunyang’anyana fito na kuzitumia kupigana
bila kujali kwamba nyumba inaanguka maana fito ndizo zilizo ishikilia.
16.0 Mimi kama Mbunge kutokea Mkoa wa Lindi, na kama Waziri mwenye
dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, nalifuatilia kwa
karibu suala hili kwa sababu mbili:-
(i) Kwanza, kuanzishwa kwa mradi huu kutawanufaisha wapiga kura wangu,
na Watanzania kwa ujumla kwa kuinua uchumi wetu na kuongeza ajira hasa
wa Mikoa ya Kusini ambayo imeachwa nyuma kwa muda mrefu. Utafiti
unaonyesha kuwa Mikoa ya Lindi na Mtwara ina utajiri mkubwa wa mali
ghafi ya Saruji, na kwa hiyo upo uhakika wa kupata saruji bora na kwa
bei nafuu sana.
(ii) Pili, suala hili linagusa mahusiano ya Nchi mbili kwa hiyo lazima
Wizara yangu ilisimamie kwa nguvu, umahiri na umakini wote.
17.0 Kama nilivyosema huko nyuma, fedha zote zilizotolewa kwa amri ya
Mahakama ni Mkopo. Hazikuchukuliwa kama fedha za EPA au ESCROW. Ni mkopo
uliotolewa kwa Kampuni ya MEIS kwa mujibu wa Mkataba wa Makubaliano
(Investment Agreement) yenye Masharti Kibenki. Na Masharti hayo ya
Kibenki yanamtaka Mwekezaji kuweka dhamana, kulipia riba, kuwekewa muda
wa kurudisha mkopo, na anawekewa hatua za kuchukuliwa endapo Mwekezaji
huyo atashindwa kulipa mkopo. Kwa lugha nyingine, Kampuni ya MEIS
ikishindwa kulipa mkopo huo, itafilisiwa mali zake na TIB itarudishiwa
fedha zake. Iacheni benki ifanye kazi yake. Mkopo unageukaje kuwa
ufisadi?
18.0 Mimi sina Kampuni hapa nchini. Sina ubia na kampuni yoyote ikiwemo
Kampuni ya MEIS. Sina hisa katika Kampuni ya MEIS. Na sijafaidika na
mkopo huo ambao unasimamiwa na Benki ya Uwekezaji nchini (TIB). Ndiyo
maana uvumi kuwa nahusika na ufisadi wa mabilioni ya Libya hauna mashiko
kabisa. Baadhi ya wanasiasa wenzangu wanajua ukweli wote huu lakini kwa
makusudi wanaamua kuwafanya watu waamini wapinzani!
19.0 Ujenzi wa kiwanda cha simenti cha Lindi unaendelea vizuri na
mitambo yote inayotakiwa katika ujenzi huo imekwisha wasili. Asilimia 45
ya ujenzi wa kiwanda hicho umekamilika na ni mategemeo ya kampuni ya
MEIS kuwa kiwanda hicho kitakamilika ifikapo mwezi Disemba mwaka huu wa
2015.
20.0 Ni matumaini yangu kuwa nimeeleweka vya kutosha. Kama kuna mtu
anahitaji taarifa zaidi basi awe huru kuihoji kampuni ya MEIS na Benki
ya TIB ambayo imetoa mkopo huo, au kumpata Msajili wa Mahakama Kuu na
Mahakama ya Rufaa ambazo zote ziliamua Kampuni ya MEIS ipewe mkopo huo
kwa mujibu wa sheria za kibenki.
Bernard K. Membe (Mb)
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
No comments:
Post a Comment