Monday, 29 June 2015

Makamu wa Pili wa Rais Burundi akimbia nchi



Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, amemshambulia vikali Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo na kukimbia nchini akimlaumu Nkurunziza kwa kutaka kuendelea kubakia madarakani kinyume cha katiba. Inaaminiwa kwamba hivi sasa Gervais Rufyikiri amekimbilia nchini Ubelgiji kuomba hifadhi ya kisiasa. Ofisi ya Rais wa Burundi imeviambia vyombo vya habari kuwa Rufyikiri alitumwa kwa kazi maalumu huko Ubelgiji siku chache zilizopita kabla ya kurejea nyumbani na baadaye kutoroka nchini humo. Jana Jumatano Rufyikiri aliiambia kanali ya televisheni ya France 24 kwamba anapinga kile alichokiita jaribio la rais la kuwania urais kwa mara ya tatu "kinyume cha sheria." Burundi imetumbukia kwenye machafuko ya kisiasa tangu mapema mwaka huu baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea urais kwa kipindi cha tatu. Jambo hilo limezusha machafuko nchini Burundi hususan jijini Bujumbura yaliyoambatana na jaribio lililoshindwa la mapinduzi. Tarehe 13 Mei mwaka huu, baadhi ya maafisa wa kijeshi wa Burundi walifanya jaribio la mapinduzi, lakini walishindwa nguvu na maafisa watiifu kwa Rais Nkurunziza.

No comments:

Post a Comment